Bado hakieleweki kati ya kocha Jose Mourinho na mshambuliaji wa klabu ya Chelsea Diego Costa mara baada ya jana katika mchezo dhidi ya Tottenham Hotspur mshambuliaji huyo kuonekana akirusha nguo ya mazoezi ‘bibs’ kuelekea usawa wa kocha wake Jose Mourinho.
Diego Costa alionekana kukasirishwa na kitendo cha kocha huyo kumuweka benchi katika mchezo huo uliomalizika kwa sare tasa ya bila kufungana huku Chelsea wakipiga shuti moja tu golini.
Kocha Jose Mourinho alimpanga Eden Hazard kama mshambuliaji pekee huku akisaidiwa na Pedro Rodriguez na Willian huku akijaza wachezaji wengi katikati ya kiwanja kuzima mashambulizi ya Totenham.
Diego Costa ambaye alikula chakula peke yake tena ndani ya basi, alionekana mwenye hasira alipoinuka kwa ajili ya ‘warm up’ na kurusha nguo hiyo ya mazoezi kwa kocha Jose Mourinho ambapo ilimkosa na kuishia karibu na Mikel Obi.
Wawili hao wamekua katika mawasiliano yasiyo ya afya tangu walipogombana katika mchezo wa klabu bingwa Ulaya Jumatano hii dhidi ya Maccabi Tel Aviv baada ya kocha Jose Mourinho kutoridhishwa na kiwango cha Diego Costa. Tayari kocha Jose Mourinho amepotezea kitendo cha Costa, kwamba hakua na lengo la kumuumiza.
Post a Comment