0
Polisi mkoani Morogoro, wameanza upelelezi wa tukio la mwanamke mmoja, Amina Mbunda kujifungua nje ya kituo cha Polisi, Mang’ula Morogoro baada ya kuwekwa mahabusu kwa madai kuwa mume wake, Abdallah Mrisho amenunua kitanda cha wizi.

Akizungumza jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Asifiwe Ulime alisema wameanza uchunguzi wa tukio hilo.

Alisema wanazo taarifa hizo na watakapokamilisha upelelezi watatoa taarifa kamili.

Mwanamke huyo, mkazi wa Mang’ula alikamatwa na Polisi Juni Mosi na aliwekwa mahabusu akiambiwa hadi mume wake atakapojitokeza ndipo atakapoachiwa.


Akizungumza jana Amina alisema mgambo walifika kwake mchana wa siku hiyo wakamhoji kwa madai kuwa mumewe amenunua kitanda cha wizi lakini baada ya kuwaambia kuwa hayupo waliondoka.


“Lakini saa chache baada ya kuondoka, mwenyekiti wa kitongoji, mwanamume mmoja na polisi walifika nyumbani kwangu na wakanikamata,” alisema.


Amina alisema baada ya kukamatwa aliwekwa mahabusu na siku ya sita, alijisikia uchungu.


“Nilipojisikia kuumwa, nilimuomba polisi ambaye nilimtambua kwa jina moja la Sele anisaidie lakini hakusikia, baada ya uchungu kuzidi, ndipo aliponitoa nje,” alisema.


Alisema baada ya kutoka nje uchungu ulimzidi na akakaa chini kwenye majani na kujifungua.


“Niliomba msaada kwa mwanamke mmoja aliyekuwa hapo jirani hakutaka kunisaidia, lakini nikajifungua mwenyewe na baadaye Polisi mmoja alinipeleka hospitali,” alisema

Na Lilian Lucas, Mwananchi

Post a Comment

 
Top