
Miaka mingi nyuma nilikuwa nimehajiriwa na tajiri mmoja kuwa mlinzi wa getini katika jumba lake la kifahari.
Maisha kwa upande wangu hayakuwa mazuri hata kidogo, kilichokuwa
kikiniweka na kuendelea kufanyakazi nyumbani kwake ni kwa kuwa nilikuwa
nikipata baadhi ya vitu ambavyo viliniwezesha kupata mlo wangu wa kila
siku.
Kila siku nilitakiwa kufika kazini saa kumi na mbili jioni na kualiza kazi saa mbili asubuhi.
Kazi yangu kubwa ilikuwa ni kumfungulia bosi wangu mlango wa geti kila
anapotoka na kurudi kwenye miangaiko yake. Tatizo ambalo lilikuwa
likinisumbuwa ni kwamba kila nikimsalimia alikuwa hajibu salamu yangu.
Hali ya nyumbani kwangu kwa kweli haikuwa nzuri hata kidogo. Na haswa
kwenye maswala ya chakula, ukizingatia nilikuwa nina mke na watoto.
Hali ilikuwa mbaya nikamua kupekuwa pipa la taka lilokuwepo nje ya geti
la nyumba ili kutafuta tafuta mabaki ya chakula kilichobakia kutoka kwa
bosi wangu.
Bosi wangu aliniona, lakini hakusema chochote akaendelea na shughuli
zake kama siyo yeye. Nami wala sikumjali kwa sababu mtu mwenyewe hata
salamu haitikii, vipi anaweza kusikiliza shida ya mtu masikini kama
mimi.
Siku ya pili yake nikaona kikapu cha sokoni pembeni ukutani kama hatua tatu toka kwenye lile pipa la takataka.
Nikiwa ni mlinzi wa getini nikaingiwa na udadisi wa kutaka kujuwa kuna
nini ndani labda kuna mtu kasahahu kapu lake naweza kumuifadhia.
Kuangalia ndani ya lile kapu nikakuta kuna bidhaa za sokoni, inaonyesha
kama vile huyu aliyesahau kapu lake alikuwa ametoka sokoni kununua
bidhaa na kwa bahati mbaya kasahau kapu lake.
Muda wa kumaliza kazi ulipowadia nikaondoka na kapu lile hadi nyumbani
kwangu na kwa kuwa tulikuwa na shida ya vyakula tukavipika vilivyoko
kwenye lile kapu na kuvistiri matumboni mwetu, tukashukuru MwenyeziMungu
na kumuombea dua mwenye lile kapu.
Lakini ajabu ikawa kubwa zaidi, kwa maana siku ya pili yake nikakuta
tena kikapu kama kile kimejaa bidhaa za sokoni tele, sehemu ile ile.
Safari hii sikujiuliza mara mbili kama ni mtego na ninase maana shida ya nyumbani kwangu aijuwae ni MwenyeziMungu tu.
Hali hii ikaendelea karibia miezi miwili hivi kiasi mimi na familia
yangu tukawa tumeanza kuizoea ile hali ya kapu la chakula kuwepo pale
nami kulichukuwa maana siku taka kujua ni mjinga gani ambaye alikuwa
akiweka lile kapu pale, maana kila nikifanya uchunguzi sikupata hata
kumjuwa aliyeliweka pale.
Nikawa nahisi labda mama mwenye nyumba anamuwekea hawala yake, au baba
mwenye nyumba anamuwekea mwanamke wake na mimi nachukuwa na wao bila
kujuwa wanaendelea kuweka pale kwa kudhani labda kinachukuliwa na huyo
waliyemkusudia.
Mwishoni nikajifariji kama wanamuwekea mtu ambaye wanamtaka basi ndio wamekosa nami najifaidia vya bure.
Siku moja nilipoingia kazini kwangu, nikakuta watu ambao nilikuja
kuwajuwa kuwa ni ndugu jamaa na marafiki wa bosi wangu, na nikaambiwa
kuwa bosi wangu amefariki ghafla kwa presha.
Nilisikitika japo si sana kwa sababu nilijuwa kuwa labda mama mwenye
nyumba au watoto zake wanaweza kuniachisha kazi kwa kuwa baba mwenye
nyumba amekwisha fariki.
Nikaenda kuangalia ile sehemu ambayo nakuta lile kapu, siku hiyo
sikuliona, nikahisi labda mmoja kati wa wageni walio udhuria mazishi
kalibeba au mama mwenye nyumba hakuweza kumuwekea hawara wake kwa sababu
ya msiba, basi ilihali fikra zote zilikuwa zikipita mara nikiwaza hili
mara lile.
Siku ikapita, siku ya pili hali kadhalika, sikuona kapu, zikapita wiki
mbili hali haikuwa kama nilivyoanza kuizoea. Sikuona kapu wala kikapu.
Hali ilipoanza kuwa mbaya, nikaona ni bora nionane na mama mwenye nyumba, ili aniongeze mshahara kwa sababu hali si nzuri tena.
Mama mwenye nyumba akanisikiliza ombi langu na kuniuliza, kama hali ni
mbaya siku zote hizo kwanini niongezwe mshahara sasa, kwanini sikuwahi
kumuomba Baba mwenye nyumba ambaye ni marehemu sasa aniongeze mshahara
wakati alipokuwa hai?
Nikampa sababu hii na ile, lakini yule mama hakuridhika na majibu yangu,
mwishowe nikaamua kumwambia ukweli na hali halisi ilivyokuwa.
Nikamwambia kuwa wakati ule nilikuwa nikiokota kapu lilowekwa nje ya
nyumba likiwa na bidhaa mbalimbali za sokoni, na likinitosheleza mimi na
familia yangu, kwa hiyo sikuona sababu ya kuomba kuongezwa mshahara,
lakini sasa sioni tena kapu na hali uko kwangu si nzuri. Na ninaomba
msamaha kwa kuchukuwa mali ambayo haikuwa halali yangu, shida ndio
zilinipelekea kufanya vile.
Akaniuliza mara ya mwisho ni lini kuto ona kapu lile, nikamfahamisha ni siku ile ya msiba wa bosi.
Kwa mara ya kwanza ndipo nilipo baini kuwa, inawezekana kuwa marehemu
ndio alikuwa akiweka kapu lile kwa sababu kama angekuwa ni mkewe au
mtoto wake basi kapu lingendelea kuwekwa pale. Lakini hata hivyo nikawa
nastaajabu, vipi mtu ambaye hata salamu yangu kuitikia alikuwa haitikii
aweze kuwa mwema kiasi kile?
Nikashtushwa na kilio cha mke wa marehemu, nikamuomba msamaha kama
nimemkumbusha mumewe mpenzi, akanambia lah hasha, siku zote hizi alikuwa
anamtafuta mtu wa saba ambaye alikuwa akipewa bidhaa za sokoni na
mumewe, kwa sababu mumewe alikuwa kila siku akilisha watu saba kwa
kuwanunulia bidhaa mbali mbali za sokoni.
Watu sita Alisha wapata, ila mtu wa saba, ndio alikuwa akimtafuta na leo
ameweza kumgundua, kumbe ni mlinzi wao wa getini. Binafsi machozi
yalinitoka na sikuweza kuficha huzuni yangu na machozi yakawa yananitoka
kama mtoto mdogo.
Tangia siku hiyo nikaanza kuletewa kikapu cha bidhaa za sokoni kama
alivyokuwa akiniwekea bosi wangu marehemu, ila safari hii, si getini
tena, bali aliyekuwa akiniletea ni mtoto wa bosi wangu na akiniletea
nyumbani kwangu.
Siku ya kwanza nilipoletewa kapu na mtoto wa marehemu nilipomshukuru kwa
ukarimu wake, nikastaajabu kwa kuto itikiwa nikawa najiuliza isije kuwa
huyu mtoto karithi tabia za marehemu baba yake za kutowajibu watu
wanaposalimiwa.
Lakini yule kijana kabla ya kuondoka akanifahamisha kuwa ninapo zungumza
naye basi nijaribu kuongea nae kwa sauti ya juu kidogo kwa sababu, yeye
ana matatizo ya kutosikia vizuri, kama alivyokuwa marehemu baba yake,
tena yeye ana afadhali maana baba yake kusikia kwakwe kulikuwa ni kwa
shida sana.
Kwa kweli nilijisikia vibaya sana na kujilaumu, ni vipi tunaweza
kuwadhania watu vibaya, tena bila ya kuwauliza au kutaka kujuwa sababu
yake.
Ama kweli kapu lile lilikuwa si limeweka bidhaa za sokoni tu, bali
lilikuwa limeweka ukarimu na upendo ambao sikuweza kuugundua, mpaka
aliyeliweka kuaga dunia.
Post a Comment