SERIKALI
imetangaza kutoa msaada wa awali wa mabati 20, mifuko mitano ya saruji,
mablanketi na mikeka kwa kila muathirika ambaye nyumba yake imebomoka
kabisa kutokana na tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Aidha, wapangaji
katika nyumba hizo wametengewa kodi ya pango ya miezi sita ili wapate
mahali pa kujihifadhi.
Hayo
yalisemwa bungeni jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa
anahitimisha Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 uliofanyika kwa wiki mbili
kuanzia Septemba 6, mwaka huu mjini hapa.
Bunge
lijalo litaketi kuanzia Novemba mosi, mwaka huu. Waziri Mkuu pia
alitangaza kujengwa kwa miundombinu ya muda ya shule kama vile madarasa,
mabweni na vyoo hususani katika Shule za Sekondari za Ihungo na Nyakato
zilizofungwa kwa muda wa wiki mbili kuanzia mwishoni mwa wiki
iliyopita.
Alisema
tathmini za kitaalamu zikikamilika, mpango wa ujenzi wa miundombinu ya
kudumu itafanyika na maandalizi yanaendelea kupata rasilimali kwa ajili
hiyo.
Katika
hotuba yake hiyo ambayo alizungumzia tukio hilo kwa kina, alisema tangu
kutokea kwa tetemeko hilo lenye nguvu ya mtetemo wa kipimo cha Ritcher
5.7, kwa alasiri ya Jumamosi iliyopita, Serikali kwa kushirikiana na
wadau imechukua hatua kadhaa, ikiwa ni pamoja na juhudi za kurejesha
hali ya utulivu miongoni mwa waathirika.
Katika
tetemeko hilo ambalo lilisikika katika mikoa ya Kanda ya Ziwa,
liliathiri zaidi mkoa wa Kagera ambako licha ya kusababisha vifo vya
watu 17, limejeruhi wengine 253, kuharibu nyumba, vituo vya afya, shule,
nyumba za ibada na miundombinu mbalimbali.
Mbali
ya kugawa vyakula, kutoa matibabu, Waziri Mkuu alisema serikali imetoa
hifadhi za muda za mahema na maturubai kwa wananchi waliokosa kabisa
hifadhi ya makazi kutokana na uharibifu mkubwa uliozikumba nyumba zao.
“Serikali
imeshiriki katika kuwafariji wafiwa na pia kushiriki mazishi kwa
kusaidia kutoa jeneza, sanda, usafiri na kutenga fedha Sh milioni 20 za
rambirambi kwa wafiwa ambazo zitatolewa kwao muda wowote kuanzia sasa.
Waziri Mkuu Majaliwa pia alisema serikali imejipanga kuhakikisha kuwa
taasisi za umma, ikiwemo majeshi ya ulinzi na usalama na rasilimali zake
vinatumika kutoa huduma zote muhimu kwa waathirika katika kipindi hiki.
Pia
Waziri Mkuu alisema serikali inaendelea kufanya tathmini ya kitaalamu
kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Chuo cha Madini Dodoma na Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam kubaini chanzo cha tukio, kiasi cha athari
zilizotokea chini ya miamba na juu ya ardhi. “Tathmini hii ya kitaalamu
itatupa picha na mwelekeo wa kushughulikia urejeshaji wa miundombinu
iliyoharibika,” alisema.
Alitumia
fursa hiyo kuwashukuru wabunge kwa namna walivyoshirikiana na Serikali
kushughulikia janga hilo la kitaifa la tetemeko la ardhi, lakini pia
Jumuiya ya Wafanyabiashara Nchini, Mabalozi, Wawakilishi wa Mashirika ya
Umma na ya Kimataifa waliopo nchini, viongozi wa vyama vya siasa na
wananchi kwa ujumla kwa kuitikia mwito wa Serikali wa kushiriki na
kusaidia juhudi za Serikali za kuwasaidia waaathirika wa tetemeko la
ardhi.
Pamoja
na kuhimiza wananchi kuendelea kusaidia waliokumbwa na tetemeko hilo,
alisisitiza ya kuwa, Serikali itaendelea kuratibu michango yote
itakayotolewa na kuifikisha kwa walengwa, huku akionya watu kutojaribu
kujinufaisha binafsi kupitia janga hilo.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu jana alipokea msaada wa Sh milioni 121.7 ili
kusaidia wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Msaada huo umetolewa na wadau mbalimbali ikiwemo Kampuni ya Caspian,
iliyokabidhi Sh milioni 100 kupitia Meneja Rasilimali Watu wake, Omid
Karambech.
Wengine
ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Bordar Limited, Wu Yahui aliyetoa
Sh milioni 20 na Mariam Kitembe aliyetoa Sh milioni 1.679 kwa niaba ya
wauguzi walioshiriki mafunzo ya utafiti wa viashiria na matokeo ya
ukimwi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).
Akipokea
msaada huo katika viwanja vya Bunge mjini hapa, Waziri Mkuu
aliwashukuru kwa michango yao ya fedha na kuwaomba wananchi wengine
wajitokeze kwa wingi ili kuwasaidia watu walioathirika na tetemeko hilo
ambalo ni kubwa na halijawahi kutokea nchini.
Kutoka
Bukoba, Mwandishi Wetu Angela Sebastian anaripoti kuwa Mkuu wa Mkoa wa
Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu amesema mkoa huo umeunda
kamati maalumu kwa ajili ya kugawa misaada iliyokwisha kabidhiwa.
Kijuu
alisema hayo jana wakati akipokea misaada mbalimbali kutoka kwa wadau
waliofika mjini Bukoba akiwemo mfanyabiashara Saidi Salim Bakhresa (SSB)
ambaye amekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya ujenzi vyenye thamani
ya Sh milioni 100 ambavyo ni mabati, saruji, mablanketi na magodoro.
Alisema
utaratibu umeandaliwa vizuri wa kukabidhi misaada hiyo ambapo hivi sasa
kamati hiyo tayari imeanza kujenga mahema kwa baadhi ya wananchi
wanaolala nje na kugawa vifaa mbalimbali vilivyopokewa ikiwemo vyakula,
mablanketi na magodoro kwa waathirika.
Aliwashauri
wananchi kuwa wavumilivu kwani misaada itamfikia kila mmoja na kwamba
hakuna ujanja wowote utakaofanyika huku akisema makundi maalum kama
wazee, walemavu, wajane na waliopoteza makazi kabisa watapewa
kipaumbele.
Wakati
huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera ameitisha harambee kwa wadau mbalimbali
wa mkoa huo wakiwemo wafanyabiashara wakubwa, taasisi na mashirika
mbalimbali ambapo wamechangia kiasi cha Sh milioni 14 taslimu na ahadi
Sh milioni 700.
Naye
Lucy Ngowi anaripoti kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
kimepeleka wataalamu wa majengo, umeme, matetemeko na saikolojia mkoani
Kagera kwa ajili ya kufanya tathmini ya kutoa ushauri na wa kitaalamu
kwa wananchi waliokumbwa na majanga ya matetemeko.
Ofisa
Habari chuoni hapo, Jackson Isdory alisema hayo alipokuwa akizungumza
na gazeti hili kuhusu mchango wa chuo hicho kwa wananchi walioathirika
na tetemeko hilo. Alisema wataalamu hao baadhi yao wameshaondoka na
wengine wanaondoka leo kuelekea mkoani Kagera, na itakapoonekana
waliokwenda hawatatosheleza, wataalamu wengine watakwenda.
|
Post a Comment