Na
Saleh Ally
KATIKA
makala zangu Sita, nilizungumzia mambo mbalimbali kuhusiana na timu ya
taifa ya Tanzania, Taifa Stars nikigusa
sehemu kadhaa na nyingi nilijifunza baada ya kuwa katika kamati ndogo iliyokuwa
ikifanya uhamasishaji wa watu kwenda uwanjani kuishangilia timu ya taifa
ikicheza mechi ya kuwania kucheza Kombe la Dunia dhidi ya Algeria.
Niliomba leo ndiyo iwe sehemu ya mjumuisho wa yale niliyoyazungumza
kutokana na nilivyojifunza kwenye kamati, niliyoyaona nikiwa na kambi ya Taifa
Stars kule Afrika Kusini.
Wakati
najumuisha, nitarudi ninapita sehemu nilizoanza kupita mwanzo, lakini safari
hii nitakuwa nikieleza ninachoamini kifanyike, kama kweli hasa tuna nia ya
kuukomboa mpira wa Tanzania.
WAKOSOAJI:
Nilieleza
njia ambazo walipita baadhi ya wakosoaji, waliokuwa wakiipinga kamati ya
kuihamasisha Taifa Stars. Tena kamati ikageuka kuwa gumzo kuliko chochote kile,
jambo ambalo nilieleza wazi kwamba lilikaa kimaslahi zaidi.
Nilitoa
mifano kadhaa kuhusiana na namna ambavyo wakosoaji walionyesha wazi (hasa kama
ungetulia na kuzipitia hoja zao) kwamba, kuhubiri soka la vijana wiki moja
kabla ya Taifa Stars haijacheza dhidi ya Algeria, kilikuwa ni kichekesho
kikubwa.
Sikuamini
kama wachezaji wangekuzwa ndani ya siku mbili na kuanza kuisaidia Stars baada
ya wiki.
Kamwe
siwezi kupinga kuhusiana na soka ya vijana, huenda nimeililia au kuipigia
kampeni vilivyo kuliko mwingine yoyote. Lakini najua wakati wake ni upi lakini
si wakati timu ya taifa inakwenda kupambana mimi naanza kulia kuhusu vijana.
Kikubwa,
hata kunapokuwa na maslahi, lazima tukubali suala la uzalendo libaki namba
moja. Kama kila mmoja akiangalia maslahi yake akiamini yeye ni
“mfanyabiashara”. Kamwe hatuwezi kuukomboa mpira wa Tanzania.
Kukosoa
ni sahihi, kuwa huru ni haki lakini kulikandamiza taifa, bado haiwezi kuwa
sahihi hata kama wengine si wepesi kuelewa na kujua unachokosoa ni kwa ajili ya
maslahi yako.
Viongozi
TFF:
Hakika
nilieleza mengi kuhusiana na TFF, shirikisho ambalo ndani yake limeoza na watu
wengi sana walio ndani yake kama watendaji, niliwaona si watu wanaotaka
maendeleo kwa ajili ya mpira wa Tanzania.
Wengi
walio katika nafasi nyeti wanaonyesha si wenye uwezo wa kutusukuma kwenda
mbele. Lakini wamezipata nafasi hizo kwa kuwa tu ni washkaji wa bosi au
wamekuwa wakimsaidia bosi na wako tayari ‘kufa naye’ kwa lolote.
Tanzania
si mtu mmoja, bosi wa TFF hawezi kuwa kila kitu katika maendeleo ya mpira na
anapaswa kukubali kuingiza watu wenye uwezo ndani ya shirikisho hilo ili kuleta
changamoto.
Kama
Jamal Malinzi atakuwa mwoga kukosolewa, kuwa mwoga kupewa changamoto za
kiungozi au kuwa na watu walioamka wanaoweza kuona anakwenda taratibu, basi
hata mchezo wa soka hauwezi kuwa na mabadiliko.
Viongozi
wengi walio katika nafasi nyeti, kamwe hawana uwezo, huenda siku moja
nikasimama na kuwachambua zaidi. Lakini TFF lazima ikubali kwamba wanapaswa
kukaa kando na kuacha watendaji sahihi wasimame na kuusaidia mpira wetu.
TFF
si ya mtu binafsi, ni taasisi ya umma, inawakilisha Watanzania wote kwa kila
kitu. Hivyo tabia ya “Umwinyi” ife. Malinzi akubali kubadilika na kuangalia
njia sahihi na watu wenye uwezo ili tuisaidie Tanzania.
Hata
kama analenga kukuza vijana au vinginevyo, basi lazima kuwe na wataalamu sahihi
wenye uwezo wa kusaidia hasa mbio hizo. La sivyo tutaendelea kupoteza miaka
rundo huku tukishauriana na kulaumiana halafu hakutakuwa na lolote.
Wachezaji:
Hili
ndiyo lilikuwa jambo la mwisho ambalo nililigusa, hii pia ni sehemu nyeti sana.
Kwani kama wachezaji watapata kila kitu, halafu mwisho wao wakawa hawajitambui,
hakika tutaendelea kutwanga maji kwenye kinu.
Wale
wakosoaji niliowamba kuwa wazalendo wa nchi yetu, wakaamua kuwa wazalendo.
Malinzi akaamua kunisikiliza na kufanya mabadiliko kwa kupata watendaji sahihi
ndani ya TFF, lakini kama tukawa na wachezaji wasiojitambua, hakuna
kitakachofanikiwa.
Kama
ingekuwa ni utengenezaji wa bidhaa, basi wachezaji ndiyo wanaopeleka bidhaa
sokoni kwa mnunuzi. Maana ndiyo inakuwa mwisho baada ya kila kitu, pale
uwanjani, ndiyo wanaotupa majibu.
Wachezaji
lazima watambue umuhimu wa timu ya taifa, waitofautishe na klabu na ikiwezekana
mioyo yao iwe wazi na si kufanya mzaha au kuamini mitandao ya kijamii kama
Facebook, Instagram na mingine ni kitu muhimu hata kuliko kazi ambayo wametumwa
na Watanzania.
Wachezaji
wengi wa Taifa Stars wanaanza kuonyesha hawajui lolote kuanzia machoni mwao.
Wanaoamini hata wakifeli kwao si hofu na haiwaumizi.
Binadamu
mshindani ni yule anayeumizwa au kukerwa vibaya na kufeli. Lakini hakuna
aliyefanikiwa bila nidhamu ya anachokifanya na ikitokea amebahatisha
kufanikiwa, basi hatadumu siku nyingi, lazima ataporomoka.
Lakini
bado nilipata picha kwamba makosa mengi ya wachezaji walio Taifa Stars, yanatoa
picha ya malezi mabovu na ya hivyo kabisa kutoka katika klabu zao.
Hata
klabu nazo zinahitaji watu sahihi wa kukaa na wachezaji. Meneja awe mtu sahihi
katika nafasi yake. Viongozi, sijui waratibu wa timu wawe watu ambao watawapa
malezi bora wakienda katika timu za taifa wawe wanajitambua.
Tunaona
malezi ya TP Mazembe yalivyowabadilisha au kuwafanya wawe bora kabisa Thomas
Ulimwengu na Mbwana Samatta. Wanakuwa bora kinidhamu, ni kwa kuwa wanaishi
katika malezi bora.
Malezi
ya kupeana vyeo kishikaji katika klabu au waliopewa uongozi kuishi kishikaji na
wachezaji kuliko kikazi, ni tatizo jingine kubwa.
Ubora
na nidhamu ya wachezaji haiwezi kutengenezwa katika timu ya taifa. Klabu
zinapaswa kujua utovu wa nidhamu au kufeli kwa wachezaji wao katika timu ya
taifa ni picha mbaya kwao.
Najua
wachezaji wataumia kwa kuwa wasingependa kuelezwa. Lakini lazima wakumbuke,
kama tunataka mafanikio lazima kubadilika kutoka hapo tulipo. Kumbukeni,
ukililia nguvu za tembo basi lazima ukubali kuwa na mkonga.
Post a Comment