Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda,
amesema kuwa tatizo la rushwa katika mchezo wa soka nchini limekuwa
likionekana kufanyika 'waziwazi' na kueleza kwamba jambo hilo
linachangia kurudisha nyuma maendeleo ya mchezo huo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa jezi
mpya za timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mtanda ambaye alikuwa
mgeni rasmi, alisema kuwa umefika wakati wale wanaojihusisha na vitendo
hivyo kuacha na kulitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kukemea kwa
nguvu zote.
Mtanda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mchinga (CCM) Mtwara, alisema
kuendelea kuruhusu rushwa iendelee kutawala katika mchezo huo, timu
hazitaendelea na matokeo yake kila siku Tanzania itabaki kuwa
wasindikizaji kwenye mashindano mbalimbali.
Alisema pia tatizo jingine linalorudisha nyuma maendeleo ya soka
Tanzania ni kitendo cha waamuzi kupanga matokeo na kusababisha timu
isiyostahili kushinda kuibuka na ushindi.
"Waamuzi wanapanga matokeo. Tuwe na waamuzi wenye ubora wa juu ambao
watasaidia nchi yetu kusonga mbele. Ninaamini hatua mnazichukua, lakini
ni lazima zionekane wazi. Wale ambao wanaonekana wanataka kuchafua
taswira ya TFF maamuzi yachukuliwe na yaonekane," alisema.
Kiongozi huyo aliitaka pia TFF kuhakikisha inaandaa programu ya mafunzo
kwa ajili ya makocha wazalendo ili pale wale wageni watakapoondoka,
makocha hao waweze kufundisha katika kiwango cha juu.
"Sikatai makocha wageni wanasaidia kwa sababu ni wataalam, ila mpango
huo uwepo na uandaliwe utaratibu wa kuweka muda maalumu wa kuhakikisha
makocha hao wa kigeni wanaondoka na wale wazalendo wanakuwa tayari
kufanya kazi," aliongeza.
Alisema pia ili mchezo huo upate maendeleo, ni vyema mpango wa kuboresha
viwanja vinavyotumika na akakubaliana na hoja hiyo iliyotolewa na
mshambuliaji wa Taifa Stars, John Bocco, kwamba miundombinu haiko katika
viwango vinavyotakiwa.
NDOLANGA AUNGURUMA
Aliyekuwa Rais wa shirikisho hilo zamani likiitwa FAT, Muhiddin
Ndolanga, ambaye alikuwa mmoja wa wadau 194 waliotunukiwa tuzo maalumu
ikiwa ni ishara ya TFF kutimiza miaka 50 tangu ijiunge na FIFA, alimtaka
Mtanda kupitia Kamati yake ya Maendeleo ya Jamii kutunga sheria ambazo
zitawafanya wachezaji kukatwa kodi na kuweka akiba zao ili zije
kuwasaidia uzeeni.
Ndolanga alisema kwa kufanya hivyo itawasaidia wachezaji hao baadaye na
kwa utaratibu huo serikali itapata pato na uchumi wake kuongezeka
kupitia wachezaji hao wa soka.
Aliitaka pia serikali kuchukua hatua kwa kusaidia maandalizi ya mchezo wa soka kuanzia ngazi ya chini.
Aliwashukuru pia viongozi wa TFF kwa kutambua na kuheshimu mchango wao
na kuongeza kwamba kama kuna atakayebeza basi ni yule aliyekosa
kunufaika na kakosa kwa sababu hastahili.
Leodegar Tenga, Rais wa zamani wa TFF na Mwenyekiti wa Shirikisho la
Soka la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), alishukuru kwa kupata tuzo
tatu lakini akaweka wazi kuwa ile aliyoifurahia zaidi ni ya kuwamo
kwenye kikosi cha kwanza na cha mwisho hadi sasa cha Taifa Stars
kilichoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 1980.
Tuzo nyingine alizopata Tenga ni ya kuiongoza TFF kwa muda wa vipindi
viwili na vilevile kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa.
CHANZO: IPP MEDIA
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.