0


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kupungua kwa mizigo bandarini hakusababishwi na sera ya serikali ya awamu ya tano, bali ni suala la kidunia linalosababishwa na kushuka kwa sekta ya usafirishaji wa mizigo duniani kote, na siyo Tanzania pekee.

Majaliwa ameyasema hayo bungeni leo mjini Dodoma wakati akijibu maswali ya papo kwa papo kutoka kwa wabunge, ambapo Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Freeman Mbowe ameuliza swali kuhusu kupungua kwa mizigo bandarini na athari zake kwa uchumi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali ya awamu ya tano itaongoza nchi kwa mafanikio makubwa na katika sekta zote, kazi ambayo imeshaanza katika baadhi ya maeneo.

“Kamati ya Bunge ya Biashara na Uwekezaji ilikwenda bandarini na kubaini kuna upungufu wa mizigo hivyo serikali inataka ipate wadau gani wakati wadau wenyewe wanalalamika kuhusu mizigo yao , na watalii wamepungua hivyo serikali inataka ione nini ili ijue kwamba uchumi umeshuka? Ameuliza Mbowe.

Akijibu swali hilo Waziri Mkuu amesema serikali haijashindwa kuongoza nchi na kuwataka watanzania kuendelea kuiamini.

“Serikali hii haijashindwa kuongoza nchi hii nataka niwahakikishie wabunge na wananchi wote tutaongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa sana kwenye sekta zote kazi hiyo imeanza katika maeneo ambayo tunadhani taifa hili litapata maeneleo makubwa.

Kuhusu suala la kupungua mizigo bandarini Waziri Mkuu amesema suala la mdororo kwa usafirishaji wa mizigo kwa njia ya meli umeshuka duniani kote kwa sababu ya kuporomoka kwa bei ya gesi na mafuta.

Wiki moja iliyopita serikali imepata barua kutoka kwa wafanyabiashara wa DRC ikisema kwamba wataanza kupitisha mizigo yao kupitia bandari ya Dar es salaam, Rwanda nao wameihakikishia serikali kwamba mizigo yao pia itapitia Bandari ya Dar es Salaam hasa kwa mkakati wa pamoja wa ujenzi wa reli ya ‘Standard Gauge’ inayotoka Dar es Salaam, Tabora hadi bandari ya Isaka na kuunganishwa na reli hiyo hadi Rwanda.

Aidha Waziri Mkuu amesema suala la uchumi ni suala endelevu na serikalI inaendelea kulifanyia kazi kubwa ya kufanya kampeni ya kupata wafanyabiashara wengi zaidi ili kuimarisha uchumi.

Post a Comment

 
Top