MKUU
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amezindua rasmi programu
maalumu, inayolenga kuboresha sekta ya usafiri wa pikipiki maarufu kama
bodaboda pamoja na bajaji, ambao sasa watasajiliwa kwa namba zao
maalumu, zitakazokuwa zimeandikwa katika sare watakazokuwa wamevaa.
Programu
hiyo itafahamika kama Mwonekano mpya wa Pikipiki na Bajaji Dar es
Salaam. Itakapoanza, hakutakuwa na ulazima wa polisi kukimbizana na
bodaboda na itakuwa rahisi kupunguza vitendo vya uhalifu.
Akizungumza
wakati wa kuzindua programu hiyo, Makonda alisema itamsaidia abiria
endapo itatokea jambo lolote, mtu atakuwa na uwezo wa kutumia simu yake
ya mkononi kwa kuingiza namba maalumu, kama za huduma za kifedha na
kwenda katika kipengele cha huduma ya Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dar es
Salaam, kisha kuingiza namba iliyoko katika sare ya dereva.
Makonda
alisema baada ya kuingiza namba hiyo, ataweza kupatiwa jina halisi la
dereva, namba ya usajili wa pikipiki yake, eneo analoegesha, kiongozi wa
eneo lake kwa upande wa bodaboda na namba zake za simu pamoja na za
kiongozi huyo.
Pia bodaboda na madereva bajaji wote mkoani humo, watakuwa na sare maalumu ambazo watagawiwa bure pamoja na kofia ngumu.
Alisema
amekusudia kuboresha sekta hiyo ili iwe ya kuaminika pamoja na kuepusha
usumbufu wanaokumbana nao madereva hao. Aliongeza kuwa kuzinduliwa kwa
programu hiyo kutaepusha bughudha katika usafiri hasa baina ya madereva
na Polisi, hali iliyojenga uhasama.
“Maboresho
haya yamekusudia pia kutaka kuwaondoa kabisa wakamataji wa pikipiki na
bajaji jijini Dar es Salaam,” alisema na kuwataka madereva hao, kufuata
sheria zilizowekwa ili kuepuka ajali zisizo za lazima pamoja na makosa
yanayoweza kuepukika.
Aliagiza
Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani mkoani humo, kuongeza
idadi ya askari katika barabara zote kuanzia leo ili kuhakikisha kwamba
sheria zinafuatwa na kuheshimiwa.
Katika
hatua nyingine, Makonda amezindua rasmi Chama cha Madereva na Wamiliki
Bodaboda na Bajaji mkoani humo, ambapo alipongeza hatua hiyo na kuwataka
wanachama kukitumia ili kujitelea maendeleo.
Awali,
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Bodaboda na Bajaji mkoani humo,
Daud Laurian alimpongeza mkuu huyo wa mkoa kwa ubunifu huo na kwamba
hatua hiyo itaiongezea heshima kubwa sekta ya usafiri huo ambayo ilikuwa
ikitafsiriwa kuwa ni ya uhalifu na uhuni.
Alisema,
bodaboda na bajaji kwa kila wilaya yaani Temeke, Kinondoni, Ilala,
Ubungo na Kigamboni watakuwa na rangi zao za sare pamoja na namba zao.
Aliongeza
kuwa pamoja na mambo mengine, mwonekano huo mpya umelenga kuongeza
fursa za kibiashara katika usafiri huo, ambapo mtu, taasisi au shirika
litakalohitaji kubandika tangazo katika kofia ngumu au pipiki
atalazimika kulipia.
“Lakini
pia, sekta hii sasa inachangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa,
ambapo kwa mkoa wa Dar es Salaam kwa mwaka inaweza kuingiza zaidi ya
shilingi bilioni mbili,” alisema Laurian.
Uzinduzi
huo uliandaliwa kwa ushirikiano mkubwa baina ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini
(SUMATRA), Chotec Limited, Jeshi la Polisi, Shell Advance, Clouds FM,
Event Master na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na madereva wa
bodaboda na bajaji.
|
Post a Comment