WANANCHI
wamehamasishwa kujitokeza kusaidia uongozi wa Rais John Magufuli, kwa
kutoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria, vinavyofanya uchunguzi kuhusu
mali za maofisa na vigogo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Ushauri
huo kwa wananchi umetolewa baada ya Waziri Mkuu Majaliwa Kassim, kuagiza
mali za maofisa waliosimamishwa kwa upotevu wa zaidi ya Sh bilioni 80
za kodi, baada ya kupotea kwa makontena 349 yaliyopaswa kutoa mapato
hayo ya Serikali.
Akizungumza
na gazeti hili jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Bashiru Ally alisema hatua hiyo ni vema izingatie misingi ya haki na
uwajibikaji kwa kushirikisha wananchi, kwa kuwa wanajua yanayoendelea
kwa watendaji wa mamlaka hiyo.
Alisisitiza
kuwa ushiriki wa wananchi ni muhimu, kwani wanajua mbinu zote
wanazotumia maofisa hao katika ukwepaji kodi, makontena yanavyotoroshwa
na mali walizonazo.
Ally
alisema wananchi wanajua majengo makubwa wanayomiliki watendaji hao,
magari na mali zingine kwa kuwa baadhi yao ni vijana wadogo
waliosomeshwa na Serikali kwa kutumia fedha za umma kwa lengo la kufanya
kazi, lakini wamegeuka na kudhulumu watu.
Mhadhiri
huyo alishauri uchunguzi unaofanyika uwe wa kina na mapana na washiriki
wote, wakiwemo watumishi wa umma na wafanyabiashara, wachukuliwe hatua
kwa kuwa huo ni mtandao unaohusisha watu wengi.
Alisifu
hatua hiyo ya Serikali, akisema itaongeza nidhamu na heshima kwa
Serikali na kuongeza kuwa watendaji hao wasipokuwa na maelezo ya kutosha
ya mali walizonazo kwa kuzingatia mshahara wao na muda waliofanya kazi,
ni sahihi mali zichukuliwe kwa kuzingatia sheria. Mbali na watumishi
hao, Ally alishauri na wafanyabiashara watakaobainika kushirikiana na
watumishi hao, wachukuliwe hatua pia kwa kuwa nao ni wahusika.
“Hawa
wafanyabiashara wakubwa wametumika kuwarubuni watumishi wa umma, nao
warejeshe kodi waliyokwepa na ikiwa watabainika kuwa na kosa la jinai,
wafikishwe mahakamani na kushitakiwa ikibidi na mali zao zifilisiwe,”
alisema.
Majina
mengine Naye, Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson
Bana alitaka maofisa hao wa TRA wachunguzwe kwa kina kwani watu kama hao
mali zao nyingi wanaziandika kwa majina mengine ili wasijulikane.
Alisema
hatua ya Serikali kuagiza mali za maofisa hao zichunguzwe kama
zinaendana na kipato cha mtumishi wa umma ni nzuri, kwani mara nyingi
watu walikuwa wakilalamika kuwepo kwa watumishi wanaojitajirisha kwa
kukwepa kodi. Kwa mujibu wa Profesa Bana, wafanyakazi wa TRA wanalipwa
vizuri zaidi katika sekta za umma kwa lengo la kuwatosheleza, ili
wasishawishike kuingia katika ukwepaji kodi utaratibu ambao ni mzuri,
lakini wameshindwa kutumia vema fursa hiyo ya kuthaminiwa na Serikali.
Alitaka
taasisi za udhibiti wafanye kazi zao, badala ya kusubiri Rais au Waziri
Mkuu kugundua masuala mazito kama hayo, huku akitaka wananchi kusaidia
kubaini mali walizonazo na kuwachukulia hatua.
Akizungumzia
wafanyabiashara wanaomiliki makontena yaliyokwepa kulipa kodi, Profesa
Bana alisema haitoshi kuwataka kulipa kodi, bali ni lazima baada ya
kulipa, waadhibiwe kwani wao ndiyo walioharibu mifumo ya ukusanyaji kodi
ya Serikali. Profesa Bana alisema baadhi ya wafanyabiashara hao,
wamekuwa wakiweka mitandao inayotengeneza mifumo ya kushawishi watendaji
wa Serikali, ili wakwepe kulipa kodi.
Mjumbe wa
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na mchambuzi wa masuala ya
siasa, Profesa Mwesiga Baregu alisema hatua hiyo inaonesha kusonga mbele
katika mapambano ya ufisadi, lakini inatakiwa kuwa endelevu na kuacha
kuwa sehemu ya matukio.
Katibu wa
Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholas Mgaya,
alisema anaunga mkono maofisa hao kuchunguzwa na kutaka kuwe na mtindo
wa kuchunguza mali za watendaji wote wa sehemu nyeti serikalini.
Mgaya
alisema ni vema kufahamu watendaji hao, wanapata wapi fedha za kujenga
majengo ya fahari, wakati hawana mkopo ili kuleta usawa kwa kupata kitu
alichofanyia kazi na si nje ya utaratibu.
Aliitaka
Serikali kuendelea kuchunguza taasisi na sekta nyingine za umma, kwani
bado zipo sehemu nyingine zenye matatizo kama hayo. Akizungumzia wenye
makontena, Mgaya alisema ni vema Serikali ifanye hesabu upya za
wafanyabiashara wote wanaokwepa kodi.
Alisema
ni vema wafanyabiashara wote wanaoingiza vitu kutoka nje, wafanyiwe
ukaguzi wa vitu walivyoingiza kwa miaka mitano iliyopita na kodi
waliyolipa na kama wanadaiwa, walipe, lakini wakishindwa mali zao ziuzwe
na kufilisiwa kisheria, kwani kodi hizo zitasaidia kutoa elimu bure na
kufanya nchi kuendelea kiuchumi.
Post a Comment