0
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameunga mkono jitihada za kupambana na dawa za kulevya nchini kama hatua ya kuliokoa taifa na janga hilo ambalo limesababisha madhara makubwa katika jamii.
              

Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya ILEMELA mkoani Mwanza.
  
Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yatakuwa ni endelevu lengo likiwa kukomesha kabisa uuzaji, usambazaji na utumiaji wa dawa hizo kama hatua ya kuokoa kizazi cha sasa na kijacho nchini.

Kuhusu tatizo la uvuvi haramu, Makamu wa Rais amewaagiza viongozi wa mikoa ya kanda ya Ziwa wakiwemo viongozi wa Mwanza na mikoa mingine nchini kuanzisha mara moja oparesheni kali ya kupambana na wavuvi haramu katika Ziwa Victoria ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa samaki katika Ziwa hilo.

Wakati huo huo halmashauri ya wilaya ya ILEMELA, imetekeleza maagizo  14 yaliyotolewa na Makamu wa Rais aliyoyatoa mwaka jana alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo likiwemo suala la watumishi wa halmashauri kukaa karibu na maeneo ya ofisi ambapo mpaka sasa wakuu wa idara 23 wanaishi ndani ya wilaya ya ILEMELA ikilinganishwa na hapo awali ambapo watumishi hao walikuwa wanakaa nje ya wilaya hiyo hali ambayo inatajwa ilichangia kuzorotesha utendaji kazi kwenye halmashauri hiyo.


Kufutia hali hiyo, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mlezi wa halmashauri hiyo amepongeza viongozi wa wilaya hiyo pamoja na watendaji wa halmashauri kwa kutekeleza maagiza yake kwa haraka na kwa wakati.

Post a Comment

 
Top