MAAFA
zaidi yameripotiwa katika janga la tetemeko la ardhi, lililotokea juzi
mkoani Kagera, ambapo imeripotiwa idadi ya vifo kuongezeka na kufikia
watu 16, huku wengine 253 wakijeruhiwa na kusababisha simanzi na
masikitiko kwa familia nyingi. Katika tukio hilo, pia nyumba 840 za
makazi zimeanguka, nyumba 1,264 zimepata nyufa kubwa na majengo 44 ya
taasisi mbalimbali zikiwemo shule yameanguka.
Tukio
hilo limemfanya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kulazimika kufanya ziara
ya ghafla ya kuwatembelea waathirika wa tetemeko hilo, ambalo limedaiwa
kusababisha tafrani pia katika nchi jirani za ukanda wa Afrika Mashariki
za Kenya na Rwanda.
Katika
hatua nyingine, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela
kilichopo eneo la Tengeru, mkoani Arusha kimeeleza mpango wa kuanza
kufunga vifaa vitakavyotoa ishara ya matukio ya matetemeko ya ardhi
kabla majanga hayo kutokea.
Katika
mradi huo maalumu chini ya Kitengo cha Utafiti wa Miamba na Volcano,
chuo hicho kitashirikiana na taasisi mbalimbali za elimu ya juu zilizopo
Ulaya na Marekani, hasa Chuo Kikuu cha Glasgow kilichopo Scotland, kwa
mujibu wa Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Burton Mwamila. Ziara ya
Waziri Mkuu
Akitoa
taarifa kwa Waziri Mkuu jana katika Uwanja wa Kaitaba ulioko mjini
Bukoba ambapo umeandaliwa maalumu kwa ajili ya kuaga miili ya watu
waliopoteza maisha katika tukio hilo la kusikitisha, Mkuu wa Mkoa, Meja
Jenerali mstaafu Salum Kijuu alisema tukio hilo ni la kwanza kutokea
mkoani humo na kwamba limeleta madhara makubwa kwa wananchi na kuacha
majonzi makubwa.
Kijuu
alisema mpaka taarifa inaandaliwa watu 16 waliripotiwa kupoteza maisha
na kusababisha majeruhi 253, huku 170 wakiwa wamelazwa katika Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa huo na 83 wakitibiwa na kuruhusiwa.
Alisema
pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 840 za makazi kuanguka, nyumba
1,264 kupata nyufa kubwa na majengo 44 ya taasisi mbalimbali zikiwemo
shule kuanguka.
Alisema
tetemeko hilo lenye ukubwa wa alama 5.7 uliopimwa kwa kipimo cha
Ritcher cha kisayansi cha kupima matetemeko, limeleta madhara makubwa
ambapo Serikali ya Mkoa inaendelea kutathmini kwa kina athari zaidi
zilizosababishwa na tetemeko hilo na pia uharibifu uliojitokeza kisha
kupeleka katika Ofisi ya Waziri Mkuu waone jinsi ya kusaidia.
Alisema
hatua zilizochukuliwa na mkoa mpaka sasa ni kuwaokoa na kuwapeleka watu
hospitali kwa ajili ya matibabu na kuwapatia makazi ya muda baadhi ya
wananchi wenye nyumba zilizoathirika, wakati mipango mingine
ikiandaliwa.
Taarifa
hiyo ya Mkuu wa Mkoa, ilimfanya Waziri Mkuu kueleza masikitiko yake na
serikali kutokana na janga hilo na kutoa salamu za pole kwa wananchi
waliopatwa na madhara na kuwatembelea wagonjwa waliolazwa katika
Hospitali ya Mkoa na pia maeneo yote yaliyoathirika.
"Leo
si siku nzuri kwetu, nimekuja kumwakilisha Rais wetu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ambaye anawapa pole sana wana Kagera wote na
Watanzania kwa ujumla. Pia Makamu wa Rais anawapa pole kwa msiba huu
mkubwa, lengo la safari yangu ni kuja kuwapa pole, tukio hili ni kubwa
na halijawahi kutokea Tanzania, tumekuwa tukisikia kutoka mataifa ya nje
lakini leo limetupata nchini kwetu," alisema Majaliwa.
Aliwasihi
na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu, kuonesha umoja na ushirikiano,
lakini pia kujitokeza kuwafariji wenzao wakati wote wa majonzi, huku
akisema Watanzania kwa miaka mingi wamekuwa wakishuhudia mitikisiko
midogo, lakini juzi tumeshuhudia mtikisiko mkubwa kabisa ambao umeleta
madhara makubwa kwetu.
"Mpaka
sasa hatuna uhakika mtikisiko huu utakuwa endelevu kwa kiasi gani,
nataka niwahakikishie Watanzania wote, Serikali tunafanya mawasiliano na
taasisi zenye uwezo wa kubaini mtikisiko huu ili tuweze kujua jambo
hili litakuwa endelevu kwa kiasi gani na kuona dalili na ukubwa wake
utakuwaje ili tujipange katika kutoa elimu lakini pia tahadhari pindi
jambo kama hili linapoweza kutokea au tunapoona viashiria au dalili za
jambo hili," alisema Waziri Mkuu.
Alisema
kuwa Mkuu wa Mkoa katika taarifa yake alimweleza kwamba tathmini
inaendelea na kwamba ameiagiza Kamati ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu
kufika mkoani Kagera mara moja na kuzunguka mkoa mzima kwa kushirikiana
na uongozi wa mkoa kwa lengo la kufanya tathmini ya jumla.
Alisema
baada ya tathmini hiyo, utaratibu utafuatwa kwani serikali haiwezi
kuwatupa mkono wananchi hao, pia alitumia fursa hiyo kuwaambia wafiwa
kuwa Watanzania nchini kote wako pamoja nao katika janga hilo.
Akielezea
mkasa huo, majeruhi Happines Apolinary ambaye ni mkazi wa kata ya
Buyekera aliyelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera kwa kuumia
kichwani na mgongoni, alisema alishtuka kusikia mtikisiko mkubwa wakati
akiwa ndani ya nyumba yake na ghafla aliangukiwa na kuta na
kumsababishia majeraha. Pamoja na kueleza kuumia vibaya kutokana na
tukio hilo, Happines aliwashukuru wafanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa
Kagera kwa huduma nzuri waliyompatia tangu juzi alipofikishwa
hospitalini hapo.
Majeruhi
mwingine, Paulina Spilian aliyelazwa hospitalini hapo akiwa amejeruhiwa
miguu alisema akiwa ndani ya nyumba yake ghafla alisikia mtikisiko
mkubwa ulioambatana na kishindo cha kuanguka kwa kuta za nyumba na akiwa
katika harakati za kutaka kukimbia nje aliangukiwa na ukuta miguuni.
Majeruhi
huyo aliiomba Serikali kuwasaidia kwa kuwajengea nyumba na pia kuwapa
elimu kuhusiana na matukio kama hayo ili waweze kujiokoa baada ya kuona
dalili au viashiria tofauti na ilivyotokea juzi.
Advela
Respicius ambaye ni mama wa marehemu, Verdiana Respicius aliyekufa
baada ya kufunikwa na kifusi cha nyumba, akizungumza kwa niaba ya
familia za wafiwa wa tukio hilo, alitoa shukrani kwa serikali kwa kutoa
majeneza, sanda na usafiri wa kuwapeleka marehemu hao mpaka vijijini kwa
ajili ya maziko.
Vifaa
vya kutabiri kufungwa Wakati hofu ikiwa bado imetawala kutokana na
tukio hilo hasa kutokana na wananchi wa Kagera kueleza kutofahamu lolote
kabla ya kutokea kwa tetemeko kutokana na kutopewa taarifa zozote na
mamlaka za serikali, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson
Mandela kilichopo eneo la Tengeru, mkoani Arusha kimesema kinatarajia
kuanza kufunga vifaa vitakavyotoa ishara ya matukio ya matetemeko ya
ardhi kabla majanga hayo kutokea.
Katika
mradi huo maalumu chini ya Kitengo cha Utafiti wa Miamba na Volcano,
chuo hicho kitashirikiana na taasisi mbalimbali za elimu ya juu zilizopo
Ulaya na Marekani, lakini hasa Chuo Kikuu cha Glasgow kilichopo
Scotland, kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Burton
Mwamila.
Katika
mradi huo wa kwanza nchini unaolenga kutoa utabiri wa matukio ya
matetemeko na ulipukaji wa volcano nchini, vifaa maalumu vitakavyokuwa
vinapima uwezekano wa kutokea majanga hayo, vitafungwa katika maeneo
nyeti kama milima, vilima na sehemu ambazo huwa na volcano hai.
Mtaalamu
wa miamba ambaye pia ni Mkuu wa Taasisi ya 'Eco Science'
inayoshughulika na utafiti wa miamba pamoja na milipuko ya volcano, Dk
Ben Beeckmans amefafanua kuwa 'Mlima wa Mungu' (Oldonyo Lengai) uliopo
eneo la Ngaresero, wilayani Ngorongoro ndio chanzo kikubwa cha
matetemeko ya ardhi katika eneo lote la Afrika Mashariki. Mlima huo
wenye volkano hai pia umekuwa ukilipuka mara kwa mara na tukio la mwisho
lilirekodiwa mwaka 2007.
Vifaa
hivyo vya kutabiri matetemeko ya ardhi vitafungwa kuzunguka eneo la
mlima huo, Ziwa Natron, Mlima Meru na hata Mlima Kilimanjaro pamoja na
maeneo mengine nchini.
Lakini
hatua hiyo si kwamba imetokana na matukio ya tetemeko yaliyoyakumba
maeneo mengi ya nchi juzi bali ni mpango uliobuniwa na wataalamu mapema
mwaka huu na kwamba kilichobaki ni utekelezaji tu.
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya
Nelson Mandela (NM-AIST), Karimu Meshaki alisema atatoa taarifa rasmi
kuhusu maendeleo ya mpango huo wiki hii.
Hivi
karibuni Serikali ilijenga maabara kubwa kabisa ya utafiti wa kisayansi
katika Chuo cha Nelson Mandela, Arusha ambayo ilizinduliwa miezi miwili
iliyopita.
Serikali
ya India pia ilitoa mchango wake kwa kukipatia chuo hicho kompyuta
kubwa na yenye uwezo mkubwa zaidi nchini ijulikanayo kama 'Param
Kilimanjaro,' ambayo pamoja na shughuli nyingine pia inatarajiwa
kutumika katika tafiti za miamba, gesi asilia na pia kwenye huu mradi
mpya wa kufuatilia matukio ya tetemeko la ardhi na milipuko ya volkano.
|
Post a Comment