AJALI
na kero zinazosababishwa na usafiri wa bodaboda sasa umefika kikomo,
hii ni kutokana na mageuzi makubwa yanayofanywa na Serikali kwa
kushirikiana na madereva wa vyombo hivyo vya usafiri. Miongoni mwa
mageuzi hayo ni kuandaa kanzi data maalumu kwa ajili ya kuwasajili
madereva wote wa bodaboda ambao watapewa namba ya utambulisho.
Namba
hiyo pamoja na jina la dereva ndio watakuwa kwenye kanzi data hiyo.
Madereva pia watalazimika kuvaa sare muda wote wawapo kazini na namba
yake ya utambulisho itakuwa kwenye hiyo sare.
Hiyo
ni kurahisisha dereva huyo wa bodaboda kufahamika kirahisi pale
atakapofanya kosa ili asiweze kuwakimbia polisi kama inavyofanyika sasa.
Abiria
kabla ya kubebwa na bodaboda kupitia simu yake ya mkononi ataweza
kuhakiki uhalali wa dereva wa bodaboda aliyemkodi kwa kutumia namba yake
ya simu ya mkononi. Atafanya uhakiki huo kwa kuingiza namba iliyoko
kwenye sare na matokeo yake ataletewa jina na picha ya dereva
aliyemkodi.
"Lengo
la kufanya hivyo ni kuondokana na vitendo vya baadhi ya madereva
wenzetu kuwafanyia vitendo vya kihuni abiria wao ikiwemo kuwaibia.
Lakini pia tunataka kila dereva apitia mafunzo ya udereva na awe na
leseni yake.
"Lengo
la kuleta mageuzi hayo ni kutaka kuhalalisha usafiri wa bodaboda ili
uwe rasmi, lakini pia uwe wa heshima kuliko ilivyo sasa. Uzinduzi rasmi
wa mfumo huu mpya utafanyika Oktoba 18 mwaka huu," amesema Mwenyekiti wa
Umoja wa Madereva wa Bodaboda mkoani Dar es Salaam, Michael Masawe.
Masawe
alikuwa akizungumza mwishoni mwa wiki kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa
Jumuiya ya Madaktari wanaofanya kazi katika hospitali za makanisa ya
Kikristo (TCMA). Katika mkutano huo suala la ajali za bodaboda
lilijadiliwa kwa kina na madaktari hao.
Masawe pia alisema hatua hiyo itapunguza madereva wa bodaboda kutumika kwenye vitendo vya ujambazi.
Mageuzi
hayo ya usafiri wa bodaboda yanafanywa kwa ushirikiano kati ya Chama
cha Bodaboda mkoani Dar es Salaam, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na
Majini (Sumatra), Kikosi cha Polisi cha Usalalama Barabarani kwa
kushirikiana na manispaa tatu za jijini Dar es Salaam.
Masawe
alisema katika mageuzi hayo, kila kijiwe au kikundi kitasajiliwa rasmi
kwenye manispaa husika na kwenye kanzi data na itakuwa inaonesha idadi
ya madereva waliopo kwenye kijiwe hicho na majina yao. Pia alisema kila
kijiwe kitakuwa na viongozi ambao watahakikisha taratibu mpya
zilizoandaliwa zinatekelezwa na madereva wote.
"Kazi
ya kiongozi ni kuhakikisha madereva wote wako kwenye sare zenye namba
na pia amevaa mavazi yote yanayotakiwa wakati wa kuendesha bodaboda,"
alisema Masawe na kuongeza kuwa hakuna dereva wa bodaboda ambaye
ataruhusiwa kuvaa ndala au makubadhi.
Mkurugenzi
wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano alisema mpango huo
wanaoufanya kwa kushirikiana na Chama cha Bodaboda mkoani Dar es Salaam
uko katika hatua za mwisho kukamilika na sasa kuna baadhi ya mambo yako
katika hatua za mwisho. Alisema wanaanzia Dar es Salaam na baadaye
mpango huo utapelekwa pia mikoani.
Alisema
wanakamilisha kusajili vituo vya bodaboda vyote vya jijini Dar es
Salaam pamoja na kuandaa kanzi data ya vituo vyote vya bodaboda ili
asiwemo dereva ambaye watamwacha nje ya mfumo huo ambao unalenga pia
kuhakikisha kila dereva anapitia mafunzo na kupatiwa leseni.
"Dereva
ambaye atajifanya mjanja na akashindwa kujisajili kwenye vikundi kazi
ambayo tunaifanya kwa sasa, huyo hataruhusiwa kuendesha pikipiki,
tunamshauri akatafute kazi nyingine," alisema Kahatano.
Mkuu
wa Usalama Barabarani mkoa wa Temeke, Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa
Polisi, Solomon Mwangamilo alisema trafiki wanalazimika kuwakamata
bodaboda kwa kutumia nguvu kwa vile hawataki kusimama pale
wanaposimamishwa.
"Kama
polisi wasingekuwa wanafanya hiki kinachoitwa harrasment (nguvu)
nadhani hali ingekuwa mbaya zaidi, sisi tunafanya ukamataji kutokana na
usalama wao," alisema ASP Mwangamilo.
Mwangamilo
alisema ni vizuri mfumo huo wa usafiri ubadilike, kwani ilivyo sasa ni
bodaboda wenyewe wanawalazimisha polisi wawakamate kwa nguvu kwani
hawataki kutii hata kama kuna msafara wa kiongozi.
|
Post a Comment