0

WAKAZI wa Kijiji cha Mindola, Kata ya Ilindi Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma wamewatimua wenyeviti wa vitongoji vitatu kwa tuhuma za wizi wa mbao 108 za kutengeneza madawati.

Uamuzi huo wa wananchi ulifanywa katika mkutano wa hadhara ambapo walidai viongozi hao waliiba mbao zilizotengwa maalumu kwa ajili ya kutengeneza madawati ya shule.

Katika mkutano huo ulioketi chini ya Mwenyekiti wa Kijiji Denisi Ndolosi, wananchi walikataa kutoa msamaha kwa viongozi hao baada ya serikali ya kijiji kutaka wasamehewe na wasitajwe.

Sakata hilo lilifanya wananchi kuanza kufanya vurugu huku wakitaka uongozi wote wa serikali ya kijiji ijiuzulu. Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho Talita Njamasi, awali alitoa taarifa kuwa viongozi hao walikiri kosa lao walikuwa wamerejesha mbao 105 ambazo zilikuwa kwa fundi kwa ajili ya kutengeneza madawati.

Alitaja uamuzi wa kupelekea mbao hizo kwa fundi hata kabla ya kuitisha mkutano, ulitokana na msukumo aliokuwa akipewa kutoka halmashauri kuhusu utengenezwaji madawati ambayo shule yao inadaiwa madawati 67.

Kauli hiyo ilionekana kupingwa na wajumbe na hasa kitendo cha kiongozi wa sungusungu, Joel Mbona alipokuwa akiwatetea wahalifu na kukataa kuwataja kwa majina huku akiwatishia wanaohoji kwamba angewaweka ndani.

Mkazi wa kijiji hicho, Magreth Madelemu, alitaka wezi wa mbao hizo watajwe kwa majina hadharani na wasimame kutubu kabla ya uamuzi wa wanakijiji, jambo ambalo lililoungwa mkono na wajumbe wa mkutano.

Mwenyekiti wa Kijiji aliamua kuwataja wenyeviti wa vitongoji walioiba mbao kuwa ni William Mguji (Kawawa), Jackson Mazoya (Azimio) na Hamisi Nhembo wa kitongoji cha Miganga A’ na mjumbe mmoja wa serikali na mwananchi wa kawaida ambao majina yao hayakupatikana.

Mkutano huo ulielezwa kuwa, watuhumiwa walichukua mbao hizo na kugawana wenyewe badala ya kuelekeza katika mpango uliokuwa umelengwa wa madawati.

Ndipo wananchi waliamua kuwatimua viongozi hao kwa kitendo cha kukosa maadili kwa kuiba mbao ambazo zilikuwa maalumu kwa ajili ya kutengenezea madawati na kuwataka wakatafute kazi nyingine za kufanya kwani uongozi umewashinda.

Post a Comment

 
Top