0


MWILI wa marehemu Andrew Daffa aliyefariki dunia Jumatano ya wiki iliyopita katika Hospitali ya Amana Dar es Salaam, umezikwa juzi katika makaburi ya Yombo Vituka chini ya ulinzi wa Polisi huku ndugu wa marehemu wakisusa msiba huo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mahakama ya Wilaya ya Ilala, kutupilia mbali maombi ya ndugu wa marehemu ya kutaka kuzikwa kwa Daffa mkoani Tanga badala ya Dar es Salaam kama alivyoomba mke wa marehemu huyo, Glory Charles.

Aidha, kuwepo kwa ulinzi huo ni kutokana na ndugu wa upande wa mwanamume kuweka zuio mahakamani kuomba kibali cha kupewa mwili huo kwa ajili ya kuuzika mkoani Tanga.

Hata hivyo, mwili huo ulizikwa katika makaburi hayo ya Yombo Vituka baada ya misa iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Tandika wilayani Temeke.

Awali, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Adelf Sachore, alisema kuwa mahakama imeamua kuwa mwili wa marehemu huyo uzikwe eneo walikozikwa watoto wao watano.

Hakimu Sachore alisema Wakili wa utetezi kwa upande wa mdai Daniel Buma alidai kwamba marehemu akazikwe mkoani Tanga kwa madai mila na desturi zao lazima mtu akifa azikwe kwao.

Alisema mtoa hoja alidai marehemu asizikwe hapa kwani hana makazi ya kudumu ambapo katika kutoa maelezo yake hata huko Tanga hana makazi kwa kuwa hajajenga. Mlalamikiwa pia alitoa vielelezo vyake mahakamani hapo na kupokewa ambavyo ni cheti cha ndoa pamoja na picha za marehemu, watoto wao na vyeti vya watoto wa marehemu ambao anaishi nao.

Post a Comment

 
Top