0

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) ya kufutiwa mashitaka ya uchochezi yanayomkabili na wenzake watatu.

Hakimu Mkazi Mkuu, Emillius Mchauru alitoa uamuzi huo jana baada ya kukubali pingamizi lililowasilishwa na upande wa Jamhuri waliodai mashitaka hayo yasifutwe kwa kuwa hati ya mashitaka haina makosa.

Mbali ya Lissu, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni mwandishi wa gazeti la Mawio, Jabir Idrissa, Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob. Hata hivyo, uamuzi huo ulitolewa jana bila Lissu kufika mahakamani hapo kwa kuwa anaumwa.

Akiieleza mahakama, Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alidai Lissu ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa anaumwa, lakini wadhamini wake akiwemo Ibrahim Ahmed wamefika mahakamani na kueleza kuwa Lissu anaumwa malaria. Aidha, ilielezwa kuwa mshtakiwa Idrissa anaumwa na yupo Zanzibar kwa ajili ya matibabu.

Katika maombi yao, washitakiwa kupitia kwa Wakili Kibatala waliiomba mahakama ifute mashitaka hayo kwa kuwa hati ya mashitaka imekosewa kwa kutokueleza makosa hayo wametenda wapi na pia mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza masuala yanayohusu Zanzibar.

Akisoma uamuzi, Hakimu Simba alisema baada ya mahakama kupitia hoja za pande zote mbili katika kesi hiyo imejiridhisha kuwa hati ya mashitaka haina makosa.

Aidha, alisema mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa makosa yaliyofanyika yanahusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivi karibuni, mahakama ilifuta mashitaka mawili ya uchochezi kati ya matano yanayowakabili washitakiwa hao, baada ya upande wa jamhuri kuyaondoa katika hati kwa kuwa hayana kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Katika mashitaka yao inadaiwa Januari 12 hadi 14, 2016, Dar es Salaam washitakiwa wachapisha taarifa ya uchochezi yenye kichwa cha habari ‘ Machafuko yaja Zanzibar’.

Pia inadaiwa Januari 14, 2016 Dar es Salaam walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar. Inaendelea kudaiwa siku hiyo hiyo, Lissu na wenzake bila ya kuwa na mamlaka yoyote yale waliwatisha na kuwatia hofu wananchi wa Zanzibar ili wasikubali kuingia kwenye marudio ya Uchaguzi Mkuu.

Post a Comment

 
Top