Kama kuna kitu bora ambacho mtu yoyote anayehitaji kufanikiwa
anatakiwa akichague na kukisimamia ni kuwa na msimamo wa kuishi katika
ndoto yake pasipo kuyumbishwa na upepo wa aina yoyote ule unaokuja mbele
yake. Ni muhimu sana kuishi katika ndoto yako, kwa kuiamini na kuifuata
kwa ujasiri ndio nyenzo tosha ya kukuletea mafanikio makubwa katika
maisha yako.
Utafiti unaonesha watu wengi waliofanikiwa na kuwa na mafanikio
makubwa katika hii dunia tangu enzi na enzi, ni wale walioamua kuchagua
kufanya jambo moja kwa kujitoa na kuliamini pasipo kusikiliza mazingira
ya nje yalikuwa yanatoa mchango hasi wa kuwazuia kuendelea mbele.
Ukisoma vizuri katika kitabu cha Think and Grow Rich Book kilichoandikwa
na mwandishi mahiri na mashuhuri wa enzi hizo Bwana Napoleon Hill.
Bwana Hill anajaribu kutoa kanuni kubwa na ya kwanza ya mtu anayehitaji
kufanikiwa ni kuwa mwenye uhitaji (Desire of Something).
Uhitaji wako ndio unaokusukuma kutegemea mafanikio katika eneo fulani
unalohitaji uone mafanikio hayo kwa hali ya uhalisi. Hebu fikiria kwa
muda huu ni kitu gani unachohitaji ukipate au ukifanikishe katika maisha
yako kabla ya kuondoka hapa duniani. Wakati ukifikiria hivyo, hebu
tazamia kama hakuna jambo lolote linaloweza kukuzuia kufanya hivyo na
ukiweka imani kuwa inawezekana kutokea na wewe kufikia katika eneo hilo
kwa haraka.
Hebu jiulize binafsi wewe kama wewe katika Maisha yako una ndoto
gani? Una jambo gani unalotamani kulifanikisha na likaleta matokeo
chanya na makubwa kwenye maisha yako na ya watu wengi waliokuzunguka?
Kama una ndoto ya kuwa mfanyabiashara au mwekezaji mkubwa kama Dangote
unazani ni rahisi; ni lazima ujitoe kikweli kweli ili kufikia katika
eneo hilo, lakini fahamu kuwa inawezekana kabisa kufikia hapo.
Hizi ndio njia 4 ambazo unaweza kuzitumia kwa ajili ya kukusaidia
kufikia ndoto yako kwa uharaka zaidi hasa kwako wewe uliyekwisha
kutambua ndoto na maono ya kuishi kwako duniani ni nini. Tumia njia hizi
katika maisha yako ya kila siku naamini utaona matokeo makubwa ambayo
hukuwahi kuyategemea kutokea.
1: Chukua hatua ya haraka kuifuata ndoto yako.
Kwa nini uogope kuifuata ndoto yako? Yawezekana ndoto yako ni
kuanzisha kampuni kubwa ya uzalishaji wa vyakula kama bakhresa, lakini
bado hujiamini kama utaweza kufanya hivyo. Mimi nataka kukuambia UNAWEZA
kama ukiamua kuchukua hatua kidogo kidogo hakika utaona matokeo makubwa
muda si mrefu na dunia itakutambua kwa hilo.
Watu wengi wanatamani mambo makubwa na kuwa wenye maono makubwa
maishani mwao, ila watu hawa si wenye kutaka kuchukua hatua madhubuti ya
kivitendo katika kufikia katika maono na ndoto zao. Hofu na mashaka
ndio imekuwa chanzo cha wengi kushindwa kuchukua hatua; hebu amua leo
kuondoa hofu na mashaka ndani yako na amua kuchukua hatua ya kuifuata
ndoto yako, utafanikiwa.
2: Ondoka katika Mazingira Hasi.
Mazingira hasi yawezekana ni mazingira hasa ya watu; mazingira
yasiyotoa mchango wowote wa kukusaidia kutimiza ndoto yako. Kuwa mbali
na watu wenye mawazo hasi (marafiki wataabishaji) wakati wote dhidi ya
kile unachotaka kukifanya na kukiamini kwenye maisha yako. Jifunze
kuchuja mchele na mawe ili uwe bora katika eneo lolote lile; usikubali
kuvunja meno yako kwa kula mawe kisa watu.
Wapo watu kazi yao kubwa ni kuwarudisha wengine nyuma badala ya
kuwatia moyo kwa kila hatua nzuri wanayochukua. Usikubali kukatishwa
tamaa iwe na watu waliokuzunguka au hata mazingira mengine binafsi
yanayokupa picha ya kushindwa katika kuitumikia ndoto yako. Amini katika
ndoto yako na shikilia ndoto hiyo hadi mwisho utafanikiwa kwa wakati
wake.
3: Tafuta mchango wa watu wengine.
Jifunze kuwa karibu na watu wenye mawazo chanya na wale wenye uwezo
wa kutoa mchango mkubwa kwenye ndoto ya maisha yako. Tengeneza kundi
lako maalum mnaoendana (mastermind group) kimawazo na wenye wivu wa
mafanikio na pia mnaoweza kushirikiana katika kufikia mafanikio makubwa.
Hapa mtatiana moyo kila wakati na kupeana mbinu mpya kila siku kwa
ajili ya kufikia ndoto mlizonazo.
Hii ni njia nzuri na nyepesi sana katika kukusaidia kufanya mambo kwa
uharaka na kufikia katika hatua nzuri ya mafanikio makubwa ya ndoto
yako. Wapo watu ambao watafurahi kama ukiamua kuwashirikisha jambo zuri
ulilonalo au unalotaka kulifanya na watakua tayari kukusaidia kwa hali
na mali ili uweze kufanikiwa; amua kuwa na watu wa namna hii na ambatana
nao kila siku ili waweze kuwa msaada tosha kwako wa kutimiza ndoto
yako. Ukikutana na watu wa namna hii husiwe msiri kwao bali waambie
ukweli wa kile unachokitegemea kukifanya maishani mwako.
4: Jifunze kusoma vitabu na kutafuta ushauri.
Hii ndio tabia muhimu sana kwa mtu mwenye shauku kubwa ya kuhitaji
kufikia ndoto yake. Ni vizuri ujenge tabia ya kujifunza kutoka kwa watu
wengine waliofanikiwa na kukutangulia katika mafanikio waliyonayo kwa
kupitia kusoma vitabu, kusikiliza Audio, kuwatizama kwa njia ya video,
nakadhalika. Mimi binafsi ni msomaji wa vitabu sana tena sana na kila
wiki ninamaliza kitabu kimoja hadi viwili au tatu ikitegemea na ukubwa
wa kitabu; na tangu nimeanza kusoma vitabu sijawahi kupungukiwa bali
nimefanikiwa kupata mbinu nyingi sana za kunisaidia kufanikiwa zaidi
katika maisha yangu.
Tafuta mtu unayemwamini pia aweze kuwa mshauri na muhamasishaji
(mentor or coach) wa mambo unayofanya ili kufikia ndoto yako. Wapo watu
unaoweza kuwatumia kwenye maisha yako ili waweze kukupa ushauri kwa kila
hatua unayotaka kuichukua mbele yako. Unaweza kunitumia hata mimi
binafsi kama mshauri wako kama utahitaji kufanya hivyo au kupata kibali
kwa jambo hilo.
Nataka nikuambie ni kweli inawezekana kufikia ndoto yako kama
UKIAMUA. Amua leo hii ili uboreshe kesho yako. Nakupenda na wote tupo
kwenye kundi moja la kutafuta kutimiza ndoto zetu. Karibu sana katika
mtandao huu na usichoke kuutembelea kila siku kwa makala zenye mafunzo
mazuri ya kukuhamasisha.
Kama unahitaji ushauri au nami kuwa mshauri wako katika maeneo
tofauti unayohitaji mafanikio. Wasiliana nami kwa mawasiliano haya
yafuatayo.
Post a Comment