Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema mabadiliko hayo yalitangazwa Januari wakati mfumo wa GPA ulipofutwa na kurudisha wa divisheni na kwa kidato cha sita ulianza kutimika kwenye matokeo yaliyotangazwa juzi.
Katika mabadiliko hayo, kwa kidato cha sita A inaanzia alama 80-100; B ni 70-79; C ni 60-69; D ni 50-59; E ni 40-49; S ni 35-39 na F ni 0-34.
Kwa kidato cha nne, A ni 75-100; B ni 65-74; C ni 45-64; D ni 30-44 na F ni 0-29.
Dk Msonde alisema mfumo huo ni wa kudumu na hautakuwa unabadilika kama ilivyokuwa awali. Alifafanua kuwa hapo awali viwango vya alama vya kila somo vilikuwa vinabadilika kulingana na somo husika na kiwango cha ufaulu, na walikuwa wanaangalia wastani wa ufaulu kwa kila somo kwa nchi nzima na kuutumia kupanga matokeo.
Alisema mfumo uliotumika sasa hautabadilika hadi yatakapofanyika marekebisho mengine.
“Viwango havitabadilika kwa masomo yote, hakutakuwa na kutafuta wastani wa kila somo, wala wastani wa ufaulu wa nchi nzima,” alisema Dk Msonde.
Siri shule za Serikali
Shule binafsi zimetajwa kuchangia kuziinua zile za Serikali katika ufaulu kwa kuwa wengi walijiunga na kidato cha sita kutoka huko.
Wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, wazazi na walimu, walisema iwapo mazingira ya shule za Serikali yataboreshwa zaidi, shule zote zitakuwa na ushindani sawa katika kutoa elimu na ufaulu.
Mwalimu wa taaluma wa shule za Marian ya Wasichana na Wavulana, Sibes Mkenda alisema amefuatilia matokeo ya kidato cha sita na kubaini kuwa waliofanya vizuri katika shule za Serikali wengi wao ni wavulana waliomaliza kidato cha nne katika shule binafsi na kuchaguliwa katika shule za Serikali.
“Naamini kama shule za Serikali zitaboreshwa upinzani wa ufaulu utapanda, nimefuatilia wanafunzi wengi wavulana waliochaguliwa kutoa hapa kwetu waliojiunga na shule kama Ilboru, Mzumbe na Kibaha na ndiyo wamefanya vizuri kwa sababu walipata maandalizi mazuri huku na wazazi wakakubali kuwapeleka katika shule za Serikali,” alisema Mkenda.
Mzazi wa mwanafunzi Mohammed Ally aliyeshika nafasi ya pili kwa masomo ya Sayansi, Gradnes Severine alisema kupanda kwa matokeo ya shule za Serikali kunatokana na mwamko wa elimu uliopo.
Alisema kila mzazi anaamini shule binafsi na za Serikali kutokana na kusikia viongozi wanavyozinadi na kusisitiza utolewaji wa elimu bora.
“Kama watabadilika na kutoa elimu bora na wakaboresha mazingira, ushindani utakuwa nusu kwa nusu kati ya Serikali na binafsi.
“Lisiwe suala la uongozi fulani, bali liwe la kudumu ili kuwe na mazoea ya wanafunzi na wazazi kuziamini shule, lakini likiwa la muda tu hakuna watakachokuwa wamefanya,” alisema Severine.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Manyunyu iliyopo Njombe, Neema Nzowa alisema shule yake imepata matokeo mazuri kutokana na kuwa na mkakati maalumu wa kuondoa sifuri.
Alisema katika matokeo ya kidato cha sita shuleni kwake hakukuwa na sifuri wala ufaulu wa daraja la nne, hivyo wanafunzi wote wamepata daraja la tatu, la kwanza na la pili.
Alisema ili kutokomeza zero ni kuwa na idara maalumu ya kuhakiki mitihani ya kawaida ya shuleni inapotungwa na walimu, kisha ipelekwe taaluma nako ihakikiwe kabla ya kwenda kwa wanafunzi.
Alisema na mitihani hiyo hufanyika mara kwa mara huku ikifuata kanuni na taratibu za Baraza la Mitihani bila kujali ni ya kawaida; “Hapa kwetu kila siku tunafanya mitihani ya taifa, hakuna kudharau mtihani na baada ya mitihani hiyo ya kawaida tunafanya tathmini.
Mkuu wa taaluma wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Feza, Zakia Irembe alisema kitendo cha kubadili mfumo wa utoaji matokeo wakati wanafunzi wanakaribia kufanya mitihani kumechangia kuwaathiri baadhi yao. “Sipingi kutoka mfumo wa GPA kwenda divisheni, ninachotaka kusema hapa ni mabadiliko yafanyike mwanzo wa muhula ili wanafunzi wasome wakitambua wanatakiwa kufanya nini,” alisema Irembe.
Aliyeongoza ataka mafuta, gesi
Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa kwa kupata alama A kwa masomo yote ya Fizikia, Kemia na Hisabati, Hassan Gwaay amesema matarajio yake ni kuwa mhandisi wa gesi na mafuta.
Gwaay ambaye ni mkazi wa Mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro aliyekuwa anasoma katika Shule ya Sekondari ya Tabora Wavulana, alisema hiyo ndiyo taaluma anayoipenda na kila mtu kwa sasa anaizungumzia.
“Hivi sasa kila sehemu hapa nchini watu wengi wanazungumzia uchimbaji wa gesi, mafuta na petroli hivyo na mimi nimejipanga ipasavyo kuhakikisha ninakuwa mhandisi wa rasilimali hizo muhimu,” alisema Gwaay.
Post a Comment