0



SURA YA PILI.

__________
Kimya kilitawala kwa dakika kadhaa, ghafla hali ilibadilika na kuwa ya kuogopesha zaidi, sauti za ajabu ajabu zilianza kupenya kwenye kila sikio la vijana wale waliofika nje ya nyumba ya Mzee Shabani kwa lengo la kumuua yeye pamoja na familiya yake.
Kibaya zaidi sauti hizo zilivyozidi kupenya ndani ya ngome za masikio ya kila Mwanakijiji, hali zao ilizidi kubadilika. Mikono, vichwa, miguu yao ilikuwa mizito kama vile wamegandishwa, mbele hawaendi nyuma hawaendi. Walipiga kelele za kuhitaji msaada, ila mwangwi wa sauti uliwarudia. Hakuna mtu aliyeweza kuwasikia, hata wale ambao walikuwa wakizisikia kelele za mkusanyiko ule hawakuzisikia tena.
Upeo wa mboni zao ulibadilika, mara moja walijikuta wapo kwenye bahari yeye kina kirefu wanatapata. Baridi kali lilichonganyika na barafu ndani ya bahari ile, ilizidisha maumivu makali ya vijana wale. Tofauti na mwanzoni kabla ya mboni za macho yao kubadilika na kujikuta wapo ndani ya bahari ile,
Zilisikika sauti tu!
“Nakufa! Nakufa! …nakufa!!!”
Radi ilipiga ikifatiwa na mvua kubwa ya kuogopesha kabisa. Wanakijiji wote, kila mmoja alijifungia ndani kwake hata hamu ya kujua nini kinaendelea kwa wale baadhi ya vijana walioamua kwenda kutaka kuisambaratisha himaya ya Mzee Shabani kimewasibu, hakuna aliyejali. Kila mtu alijali roho yake tu.
Mvua kubwa iliyochanganyika na radi zisiokuwa na idadi, iliendelea kunyesha kwa nguvu bila hata kupunzika kwa zaidi ya masaa matatu. Wanakijiji walijifungia ndani hakuna hata mmoja aliyethubutu kutoka nje.
****
Saa kumi na moja alfajiri, zilisikika sauti upande ule ulipokuwa nyumba ya Mzee Shabani, sauti za kuomba msaada. Ziliwatisha baadhi ya wanakijiji walikuwa tiyari wameshaamka kwa ajili ya pirikapirika za siku. Cha kushangaza zaidi, licha ya mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia siku hiyo ila kulioneka kukavu kabisa. Jambo liloleta sintofahamu, kuongeza hali ya kugofya miongoni mwa Wanakijiji. Hivyo sauti zile zilizo kuwa zikisika dhahiri kuwa zinatoka maeneo kwa Mzee huyo, ziliwafanya watu warudi ndani kujifungia kusubiri papambazuke.
Jua lilipoaanza kuchomoza ndani ya kijiji cha Tangeni kuikalibisha siku mpya huku bado sintofahamu ilikuwa imetanda. Balaa kila kukicha, hakuna aliyefurahia namna hali ilivyo. Jana tu! Inasadikika wale vijana walioenda Nyumbani kwa Mzee Shabani wamepotea, hawajulikani walipo. Baadhi ya watu walisema kuwa sauti zao zilisikika alfajili ya leo wakiomba msaada ila hakuna aliyeonekana kujitokeza.
Hali ilizidi kuwa mbaya. Zilipita siku tatu hakuna kijana yoyote aliyeonekana. Vilio na simanzi vilitanda kila kona ya Tangeni. Mambo yalizidi kuwa magumu sana ndani ya kijiji. Watu walizidi kuogopa, hakuna hata moja aliyethubutu kulitaja jina la Mzee Shabani au kutoa njia yoyote ya kukabiliana nae.
Mvua zilikunya wiki nzima. Hawakujua hata zilikuwa zimetokea wapi. kibaya zaidi, zilinyesha eneo lile tu. Hakuna mtu aliyepata kutoka wala kuingia ndani ya kijiji. Mvua hizo ziliambatana na radi kali sambamba na sauti za kutisha sana, na kuogofya. Hakuna hata Mwanakijiji moja aliyethubutu kutoa mguu wake kuendelea na kuwatafuta wale vijana.
Siku tatu mfululizo zilitosha kukubaliana na upotevu ule na cha ajabu zaidi, hata walipofika kwenye nyumba ya Mzee shabani hawakuona kitu, si nyumba wala watu walikuwepo eneo la nyumbani kwa Mzee Shabani. Palionekana shimo, tena shimo kubwa lililozama kuelekea chini. Hata walipojaribu kuchungulia kiuwogauwoga, hawakufanikiwa kuona kitu ndani ya upeo wa macho yao. Hivyo ujio wa mvua ile ulikatisha zoezi la kuwafatilia wale vijana na hapo hakuna aliyetamani kabisa zaidi ya kujifungia tu kwenye nyumba zao.
Siku ya saba jioni, mvua ndio iliacha kunyesha huku kigiza nacho kilikuwa kinaingia hivyo hakuna Mwanakijiji aliyeweza kutoka kwake kwenda kwa mwenzake kuuliza kulikoni? Hali inavyoendelea ndani ya kijiji chao, kama ilivyozoeleka Wanakijiji wa Tangeni wamezoea kuishi kijamaa kama wingi wa vijiji nchini Tanzania. Kwa wakati huo vilivyokuwa vikiishi kwa namna yoyote ile tatizo la Mwanakijiji moja ni tatizo la Wanakijiji wote.
Kigiza kilingia muda mfupi tu baada ya mvua ile ya ajabu kukata, hata hivyo si kwamba mambo yale yalikuwa yameisha, la hasha! Bali mauzauza yaliendelea ndani ya kijiji. Usiku wa siku hiyo ulikuwa mgumu kuliko hata siku ambazo mvua ile ya ajabu ilinyesha mfulizo. Vishindo, minong'ono ya ajabu ilisika katika kila kwenye Nyumba ya Mwanakijiji wa Tangeni. Kila mmoja hali aliyekuwa nayo ilikuwa siya kawaida kabisa, vituko vilizidi katika kila pembe.
Hata jogoo wa asubuhi ya kuamkia siku iliyofata alivyowika hawakuweza kuamini kuwa usiku ule uliyojaaa vimbwanga vya kila aina kama ulimalizika salama. Miongoni mwao Wanakijiji haikuwa jambo la kawaida, ufumbuzi uliitajika haraka sana kupambana na nguvu ile ya giza ndani ya kijiji. Hali ambayo iliwakosesha raha wanakijiji wote hakuna aliyejua mwisho wa yale yote na chanzo cha yote. Kiukweli kabisa mambo mengi hutokea kwa sababu ya nini? Sababu ya mambo yale, mambo ambayo takiribani miaka kumi yalitoweka ndani ya kijiji. Basi kutakuwa na kitu tu kimejificha nyuma ya hili si bure hata kidogo.
______________
Nilifikiri sana juu ya jambo lile kiukweli nisifiche tu! Mambo kiupande wangu niliyaona magumum, ni kweli kuwa Mwajabu anataka kuolewa hilo sipingi, sawa kabisa. Vipi kuhusu upendo wangu? Inaonekana wazi Mwajabu ananipenda angalau sijawahi kumwambia kuwa nampenda. Si kwangu, hata yeye upande wake neno nakupenda, limekuwa gumu kulitamka kwangu. Ila kwa vitendo tu, ni dhahiri moyo wake ni wa kwangu, na wa kwangu ni wa kwake. Sasa hapa kuoa na kuolewa ni jambo zito na si kidogo hata kama Mwajabu hatokuwa radhi kuolewa na huyo jamaa. Kwa upande wangu pia itakuwa ngumu mimi kumuoa. Nitawezaje? Ndio kwanza najipanga kwenye maisha. Kingine sina ndugu, wazazi nilishawapoteza miaka mitatu nyuma.
Unakumbuka habari za mchawi wa Tangeni? Kijiji cha tatu kutoka hapa, pale ndipo ulipokuwa mwisho wa familia yangu. Si Mama, si Baba ndugu, wote ilikuwa kama bahati kubaki kwenye hii Dunia. Kilichonisaidia, sikupenda kuishi kule, nilipenda kukaa kwa Mjomba. Ambaye nae mwaka moja tu, nilimzika. Hivyo maisha yangu bado ya kuungaunga. Nitaweza kweli kukaa na Mtoto wa mtu? Hilo nalo tatizo, si masihara tena, ni tatizo kubwa hatari. Siwezi acha, nisubiri nione itakavyokuwa. Ila ndio hivyo, siwezi kumuacha mtoto mzuri kila mtu ananiita, Baba Mwajabu alafu eti anatokea bwege ata alipotokea aijulikani anamchukua mtoto. Hapana. Sitaki atoke kwenye mboni ya macho yangu.
Hata sikujua vitu vyote vile vinatokea wapi? Ila nilichojua kwa sababu ya upendo wangu kwake. Licha ya kuwa marafiki, ila urafiki wetu ulikuwa zaidi ya urafiki. Si masihara hata kidogo. Nilihitaji siku moja jina la rafiki na hadhi yake ipotee na kupanda kabisa katika level za wapenzi, baadae mke na mume.
Umri wangu wote huu, si mtu wa Wanawake kama vijana wengine. Kwa upande wangu Mwajabu ndio msichana haswa wa kuwa na mtu kama mimi na si mwingine. Inaonesha wazi damu zetu zinafafana. Hakuna mvulana yoyote yule anayeweza kukaa na Mwajabu hata awe wapi kama mimi, iwe kisimani, iwe wapi. Kitendo kile ndio kilifanya baadhi ya vijana kuniita Baba Mwajabu.
Mwanzoni nilipinga vikali nikihofia pindi Mzee Shabani, Baba yake na Mwajabu atavyosikia habari zile itakuwaje? Namfahamu fikra hana masihara kwa bintiye, hata kidogo!
Wakati bado nipo ndani niliwaza yote huku kibaridi kikiwa kinapenya vizuri kwenye matundu ya madirisha ya chumba changu, kati ya viwili vinavyokamilisha kijumba changu mwenyewe alichoniachia Mjomba kama urithi wangu mwaka moja tu aliponiacha kwenye majonzi. Yeye ndiye alibaki kama tegemeo langu ila hata alivyoniacha sikuamini.
Kichwa tu kilitosha kukamilisha safari yake ya maisha ya hapa duniani, aliniambia kinamsumbua muda mfupi tu alipotoka kwenye kazi zake. Hakuchukua hata masaa matatu habari yake ndipo ilipoishia. Inaniuma sana nikikumbuka dah! Acha tu.
Nilianza kusikia sauti ya kike inatokea nje ya chumba changu, sauti ambayo niliifahamu vyema ndani ya ngoma za masikio yangu si ngeni. Nilijitoa kitandani kwenda kuungalia ninachokisikia nikweli au la! Ile cha ajabu nilichokiona kilinishangaza, nilikuwa kama nimepigwa na butwaaa!
Sauti nilifahamu vema kuwa ni sauti ya Mwajabu ila cha kunishangaza sikuona mtu pale nje. Nilihisi uwenda masikio yangu hayakuwa sawa kwa muda ule, au itakuwa majini nini? Sikutaka kujiuliza sana nikarudi zangu ndani. Mara nilisikia tena nikiitwa, na safari hii haikuwa muito wa kawaida. Ilikuwa dhahiri langu jina likiitwa na sauti pekee ya muito ule ilikuwa ile ile ya Mwajabu.
Niliamua kutoka tena nje kwenda kuangalia uenda labda alijificha pindi mara ya kwanza nilipotoka. Nilifungua mlango wangu taratibu huku macho yangu nikiyatumbua vyema kuhakisha kwamba ninacho kisikia ndio ninachokiona au la! Sikuweza kuona kitu chochote, ila nilihisi kama mtu yupo nyuma yangu. Niligeuka haraka, nilishituka macho yangu yalipokutana ana kwa ana na Mwajabu, aliniogopesha sana. Namna ya ujio wake, mapigo ya moyo yalikuwa yakinienda mbio kuliko kawaida. Sikutegemea kabisa hali ile kama ingenitokea muda ule.
 Riwaya hii ni endelevu Leo sehemu ya pili kati ya sehemu 5  endelea kufuatilia ili utate kujifunza 
 
                          KAMA ULIPITWA SEHEMU YA KWANZA>>>BOFYA HAPA

RIWAYA: MTOTO WA MCHAWI WA KIJIJI
MWANDISHI: YONA FUNDI
MAWASILIANO: 0675278759

Post a Comment

 
Top