0


MAGONJWA ya Moyo (Cardiovascular Diseases), ni miongoni mwa magonjwa yaliyoko kwenye kundi la ugonjwa usioambukiza. Haya ni magonjwa yale yote yanayoathiri moyo na mishipa yake. Kwa hiyo, magonjwa ya moyo yanajumuisha ugonjwa wa Kupanda kwa Shinikizo la Damu (High Blood Pressure/Hypertension). Hili ni tatizo sugu la kiafya linalohusisha kuongezeka kwa mgandamizo wa msukumo wa damu kwenye mishipa ya damu.

Magonjwa mengine ni Koronari za Moyo (Coronary Heart Diseases). Huu ni ugonjwa wa moyo ambapo mafuta yanaganda ndani ya ateri koronari na kuziba kwa kiasi fulani au kuziba kabisa kwa ateri ya koronari ya/za moyo, hivyo kusababisha upungufu wa damu katika sehemu ya moyo ambayo hupata damu kupitia mishipa hiyo.

Ugonjwa huu wa Koronari za Moyo hudhoofisha misuli ya moyo kiasi cha kusababisha moyo kushindwa kusukuma kiwango cha kutosha cha damu (Heart Failure). Aidha, ugonjwa huu husababisha Arithmia (Arrhythmias), kwa maana ya ugonjwa unaosababisha mapigo ya moyo yasiyo na mpangilio wa kawaida.

Kuna ugonjwa wa moyo unaoitwa Atherosklerosisi (Atherosclerosis). Hali hii ni kitendo cha mafutamafuta kuganda kwenye mishipa ya ateri. Kuganda kwa mafutamafuta huko, kunaweza kuchukua miaka mingi. Kadri miaka inavyosonga mbele, ndivyo mafutamafuta haya yanazidi kuwa magumu na kuzuia msukumo wa damu yenye oksijeni kwenye moyo.

Ikiwa mafutamafuta yataziba kabisa kwenye ateri koronari na kusababisha misuli ya moyo kukosa damu yenye oksijeni, huweza kumsababishia mtu maradhi mengine yanayoitwa Anjina (Angina), kwa maana ya maumivu makali ya kifua na Mshtuko wa Moyo (Myocardia Infarction/Heart Attack).
Anyurismu (Aneurysm) ni aina nyingine ya magonjwa ya moyo. Hiki ni kitendo cha mishipa ya ateri kuvimba kama puto kutokana na kuharibika kwa mishipa au kudhoofika kwa kuta za mishipa.

Ikitokea mishipa hii ya ateri ikapasuka, husababisha damu kuvuja kwenye ubongo, hivyo kumsababishia mtu kukumbwa na Kiharusi (Stroke). Kiharusi ni ugonjwa wa kupooza unaotokana na kuingiliwa au kupungua kwa usambazaji wa damu kwenye ubongo hali inayosababisha seli za ubongo kukosa oksijeni na virutubishi.

Ugonjwa mwingine wa moyo hujulikana kwa jina la Rhumatiki ya Moyo (Rheumatic Heart Disease). Huu ni ugonjwa unasababisha kupungua utendaji kazi wa moyo kutokana na moyo kuwa na vivimbe tangu mtoto anapozaliwa (Congenital Heart Diseases), na mara nyingi huweza kusababisha vifo wakati wa utotoni.

Peripheral Vascular Disease ni ugonjwa mwingine wa moyo kwenye mishipa ya damu. Ugonjwa huu hutokea kwenye mfumo wa usambazaji wa damu nje ya ubongo na moyo. Mara nyingi, ugonjwa huu huwapata watu wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea, hasa wavutaji wa sigara na wenye kisukari.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza kama yalivyo magonjwa ya moyo, kila mwaka huuwa watu milioni 38 duniani. Vifo vingi kati ya hivyo, hutokana na magonjwa ya moyo. Inakadiriwa kwamba watu takriban milioni 17.5 hufariki dunia kila mwaka kwa magonjwa hayo ya moyo, ikifuatiwa na magonjwa ya Saratani yanayouwa watu takriban milioni 8.2 kwa mwaka, wakati magonjwa ya njia ya hewa yanauwa watu milioni nne na Kisukari watu milioni 1.5 kila mwaka.

Kwa upande wa Tanzania, takwimu kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto nchini (PAT), zinaonyesha kwamba takriban watoto 13, 600 huzaliwa kila mwaka wakiwa na magonjwa aina mbalimbali ya moyo, huku watoto takriban 3, 400 kati yao, wakihitaji kupatiwa matibabu kwa kufanyiwa upasuaji.

Ni nini chanzo cha magonjwa ya moyo?
Kutozingatia kanuni za ulaji bora, ni moja ya mambo yanayoongeza uwezekano wa mtu kupata magonjwa ya moyo. Kwa mfano, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, vyakula vyenye sukari nyingi, chumvi nyingi na lehemu nyingi, huku ulaji wa mbogamboga na matunda ukiwa ni wa kiwango cha chini, huongeza uwezekano wa kupatwa na magonjwa ya moyo.

Aidha, hali ya kuwa na uzito uliozidi kiasi au kuwa na unene uliopitiliza pamoja na kutofanya mazoezi ya mwili na viungo mara kwa mara, huchochea pia uwezekano wa magonjwa ya moyo.
Wakati mwingine magonjwa ya moyo huweza kutokana na historia ya ugonjwa huo katika familia. Umri unapozidi miaka 50 kuna uwezekano pia wa kupatwa na magonjwa haya ya moyo, huku wanaume wakiwa kwenye hatari zaidi ya kupatwa na tatizo hili mapema zaidi ikilinganishwa na wanawake.

Tafiti mbalimbali ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kuwa magonjwa ya moyo huanza kumwandama mtu pale mambo fulani yanaposababisha sehemu ya ndani ya kuta za mishipa ya damu kuharibiwa. Mambo hayo fulani, ni pamoja na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha aina fulani za mafuta na lehemu katika damu. Hali hiyo inapompata mtu, mishipa ndani ya moyo huweza kufungamana kwa mafuta. hivyo kuleta Mshtuko wa Moyo (Heart Attack) au Kupooza, kwa maana ya Kiharusi (Stroke).

Aidha, ongezeko la lehemu huongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo. Kiujumla, wingi wa lehemu unakadiriwa kusababisha vifo vya watu takriban milioni 2.6 duniani kila mwaka. Kuwepo kwa sukari nyingi katika damu, husababisha ugonjwa wa Kisukari, ambao unamweka mtu katika hatari ya kupata ugonjwa wa Moyo au Kupooza/Kiharusi mara mbili zaidi ya asiye na Kisukari.
Aidha, kuwa na sukari nyingi kwenye damu kwa muda mrefu, husababisha kuganda kwa mafutamafuta kwenye mirija ya damu. Kuganda huku kunaweza sababisha kupungua kwa mtiririko wa damu kwenye mishipa.

Shinikizo Kubwa la Damu, maana yake ni kwamba moyo unalazimika kusukuma damu kwa nguvu ili kutosheleza mahitaji ya mwili. Kuulazimisha moyo kufanya kazi kuliko kawaida yake, kunasababisha moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure).

Uvutaji wa sigara au utumiaji wa tumbaku kwa kutafuna au kunusa (ugoro), husababisha pia sehemu ya ndani ya kuta za mishipa ya damu kuharibiwa, hivyo kuongeza hatari ya magonjwa ya moyo. Kemikali zinazopatikana kwenye tumbaku, huweza kuharibu seli za damu. Uharibifu huo wa seli, huingilia muundo na utendaji mzuri wa mishipa ya damu. Aidha, kuharibika kwa mishipa ya damu, kunachochea mafuta kuganda kwenye mishipa ya damu (Atheroskerosisi).

Unywaji pombe kupita kiasi na utumiaji wa dawa za kulevya ni hatari tena kwa hili. Unywaji pombe mara kwa mara huongeza uzito wa mwili, hali inayoweza kusababisha Shinikizo la Damu kupanda. Aidha, pombe na dawa za kulevya hudhoofisha misuli ya moyo na mishipa ya damu. Misuli na mishipa ya damu ya moyo ikishadhoofika, huweza kusababisha moyo kutofanya kazi katika ubora wake (Heart Failure).

Lakini pia, ikitokea mishipa ya damu ikaharibiwa, mafuta mwilini hujikusanya katika sehemu ya mishipa iliyoharibiwa, hivyo kutengeneza utando wa mafuta (plaque). Kadri muda unavyoendelea ndivyo mafuta haya yanavyozidi kujijenga katika sehemu hiyo hadi kufanya mishipa hiyo kuwa myembamba, hivyo kupunguza kiasi cha damu kinachobeba hewa ya oksijeni na virutubishi kwenda kwenye misuli ya moyo.

Kitendo hicho kitaalamu, huitwa Atherosklerosisi, ikimaanisha kukakamaa kwa mishipa ya ateri kutokana na mkusanyiko wa mafutamafuta ndani ya ateri. Hatimaye sehemu hiyo ikipasuka, sehemu ya seli za damu zinazoitwa pleteleti za damu (chembe ndogo mviringo ambazo zinahusika na kuganda kwa damu) ambazo husaidia mwili kuponya kidonda, hujigandisha kwenye mpasuko, hivyo kuanza kujikusanya.

Hali hii huongeza mkusanyiko, hivyo kuendelea kufanya mishipa hiyo kuwa myembamba zaidi, hivyo kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure) na mtu kupata ugonjwa wa Mshtuko wa Moyo (Heart Attack).

Mkusanyiko wa mafuta na pleteleti za damu wakati mwingine, huweza kumeguka katika mfumo wa mabonge na kusafiri kwenda kuziba mishipa midogo ya damu kichwani. Hali hii ikitokea, mtu hupata Kiharusi (Stroke/Cerebrovascular Accident).

Dalili kuu za magonjwa ya moyo
Kinachosikitisha hadi sasa katika tasnia ya magonjwa ya moyo, ni kwamba mtu anaweza asione dalili zozote za moja kwa moja za magonjwa ya moyo, hadi wakati mishipa ya damu ya moyo inapokuwa imeziba kabisa au kushindwa kuruhusu damu kwa kasi na kiwango kinachotakiwa.

Mara nyingi, hakuna dalili inayojitokeza moja kwa moya kwa wagonjwa wa aina hii, hadi pale moyo wenyewe unaposhindwa kufanya kazi ghafla (Heart Attack) au mtu anapopata Kiharusi (Stroke). Zaidi ya maelezo hayo ya wataalam wa magonjwa ya moyo, dalili zinapojitokeza mapema huweza kutofautiana kutegemea na aina ya ugonjwa wa moyo, ingawa dalili hizo nazo hazijitokezi mapema kama ilivyo kwa magonjwa mengine.

Hata hivyo, dalili kuu za magonjwa ya moyo ni pamoja na maumivu ya kifua (Hii ni dalili kuu ya ugonjwa wa moyo); moyo kwenda mbio na kumfanya mtu akose pumzi au kushindwa kupumua; kuvimba miguu, tumbo na mishipa ya shingoni kujitokeza nje; maumivu ya mgongo, mabega, shingo na taya; tumbo kujaa, kichefuchefu, na kutapika; kukosa usingizi; kupoteza fahamu na kikohozi kisichokwisha.

Kilicho muhimu kutambua hapa ni kwamba hadi dalili hizo zijitokeze wazi, ni kwamba mtu huyo amekuwa akiishi na ugonjwa huo kwa muda mrefu. Kwa hiyo, njia bora ya kugundua mapema dalili ya ugonjwa wa moyo ni kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara.

Inashauriwa mtu kuwa na ratiba maalum ya kumuona daktari angalau mara moja kila mwaka ili kuweza kuchunguza afya ya moyo wako na mwili kiujumla. Endapo mtu atahisi maumivu ya aina yoyote kifuani, hasa baada ya kufanya mazoezi, ni muhimu kuonana na daktari haraka.

Post a Comment

 
Top