Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amedai Marekani ndiyo imekuwa ikiichokoza Korea Kaskazini na kuichochea kuongeza kasi mpango wake wa silaha za nyuklia.
Amepuuzilia mbali wito kutoka kwa balozi wa Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kuvunja uhusiano na Korea Kaskazini.
Hii ni baada ya Pyongyang kufanyia majaribio kombora jingine.
Urusi imekuwa ikisema kwamba vikwazo na hatua nyingine za kuiadhibu Korea Kaskazini haziwezi kufanikiwa. Badala yake imekuwa ikihimiza kuwepo mashauriano.
Marekani imetahadharisha kwamba serikali ya Korea Kaskazini "itaangamizwa kabisa" iwapo vita vitazuka.
Jumatano, Korea Kaskazini ilifanyia majaribio kombora lake la kwanza katika kipindi cha miezi miwili.
Taifa hilo lilisema kombora hilo linaweza kushambulia eneo lolote Marekani bara.
Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya ulinzi wametlia shaka uwezo wa taifa hilo kuwa na teknolojia inayowawezesha kurusha kombora lenye kichwa cha silaha ambalo linaweza kutoka nje ya anga ya dunia na kurejea tena bila kuharibika.
Lavrov amesema nini hasa?
Akiongea wakati wa ziara katika mji mkuu wa Belaruss, Minsk, Bw Lavrov ameuliza iwapo Marekani inatafuta kila sababu ya kuiangamiza Korea Kaskazini.
"Mtu anapata taswira kwamba kila kitu lazima kifanywe kuhakikisha Kim Jong-un 'anarukwa na akili' na kufanya kitendo kingine ambacho si cha busara," amesema.
Wamarekani, amesema, "wanafaa kutufafanulia sisi sote ni nini wanachokitafuta".
"Iwapo wanatafuta kisingizio cha kuiangamiza Korea Kaskazini, kama alivyosema balozi wa Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, basi nawaseme waziwazi na hebu kiongozi wa Marekani athibitishe hilo."
Huku akihimiza kufanyika kwa mazungumzo mapya na Korea Kaskazini, Bw Lavrov ameongeza: "tayari tumesisitiza mara kadha kwamba kipindi cha vikwazo kimsingi kimefikia kikomo, na kwamba maazimio ambayo yalileta vikwazo hivyo yalifaa kuwa na hitaji la kuanzishwa upya kwa mchakato wa kisiasa, hitaji la mazungumzo mapya.
"Lakini Wamarekani walipuuzilia mbali kabisa hitaji hili na naamini hili lilikuwa kosa kubwa."
Baada ya China, Urusi ni moja ya nchi kadha ambazo zina uhusiano mwema na Korea Kaskazini.
Mataifa hayo mawili yana kura batili katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Msimamo wa Marekani ni upi?
Nikki Haley, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, ameyahimiza mataifa yote kusitisha uhusiano wa kidiplomasia na kibiashara na Korea Kaskazini.
Rais Donald Trump ametoa wito kwa mwenzake wa China, Xi Jinping, kuacha kuiuzia mafuta Korea Kaskazini.
"Tunafahamu kwamba kichocheo cha Korea Kaskazini katika uzalishaji wa silaha za nyuklia ni mafuta," amesema Bi Haley.
"Na msambazaji mkuu wa mafuta (kwa Pyongyang) ni China."
Kihistoria, China imekuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa KOrea kaskazini.
- Nani alimrukia Kim Jong-un?
- Trump aionya vikali Korea Kaskazini kuhusu makombora
- Trump: Korea Kaskazini watakuwa kwenye 'shida kubwa'
Wizara ya mambo ya nje ya China imesema taifa hilo daima limekuwa "likitekeleza kikamilifu maazimio" ya Umoja wa Mataifa.
Kwenye Twitter Alhamisi asubuhi, bw Trump alizungumzia ziara iliyodaiwa kufanyika mapema mwezi huu ya mjumbe wa China nchini Korea Kaskazini na kudokeza kwamba Beijing haijakuwa ikichukua hatua za kutosha kuikabili Korea Kaskazini.
Vikwazo vya sasa vya Umoja wa Mataifa hupunguza mafuta ambayo yanaweza kuuziwa Korea Kaskazini, lakini haijazuia kabisa uuzaji huo.
Tishio la makombora limebadilika?
Kombora la Hwasong 15 lililorushwa Jumatano na Korea Kaskazini lilipaa juu zaidi kuliko kombora lolote lililowahi kufanyia majaribio awali na taifa hilo na lilianguka katika sehemu ya bahari ya Japan.
Serikali inasema lilipaa juu hadi 4,475km (maili 2,780) - mara 10 zaidi ya kilipo Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu.
Korea Kaskazini ilisema kombora hilo lilikuwa na kichwa cha silaha chenye uwezo wa kuingia tena ndani ya anga ya Dunia.
Septemba, Korea Kaskazini ilisema ilikuwa imefanyia majaribio bomu la nyuklia ambalo linaweza kuwekwa kwenye kombora la masafa marefu.
Hiyo ilikuwa mara ya sita kwa Korea Kaskazini kufanyia majaribio silaha ya nyuklia.
Post a Comment