Kufuatia zoezi la serikali la kupanua na kuboresha miundo mbinu
mbalimbali nchini hususan ya barabara katika jiji la Dar es Salaam
ambapo imelazimu baadhi ya maeneo kubomolewa ili kupisha zoezi hilo la
upanuzi, Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima nalo
limekumbwa na kadhia ya kubomolewa.
Kanisa hilo lililoko jirani kabisa na Barabara ya Morogoro ambayo
serikali imepanga kuipanua ili kurahisisha usafiri na kupunguza foleni,
lilitakiwa kubomolewa kutokana na kuwa ndani ya eneo la hifadhi ya
barabara hiyo.
Mchungaji Biyagaza wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko chini ya Askofu
Gwajima, ameeleza kuwa serikali iliwapatia notisi ya siku 30 ili
wabomoe kipande cha jengo la kanisa hilo kilichopo ndani ya eneo la
hifadhi ya barabara.
“Ni kweli tunayo notice ya mwezi mmoja ya kuhakikisha kwamba eneo ambalo
ni hifadhi ya barabara tunaliacha. Na hifadhi ya barabara ni mita 90
kuanzia katikati. Bahati nzuri wale waliokuja kuweka alama zao
walipofika hapa na wahandisi , mafundi na baadhi ya watu wa kanisani
walikuwepo. Basi tukawaambia wapime mita 90 zinapoishia. Kwa hiyo
wakapima mita 90 zilipoishia wakaweka alama, wakasema basi nyie mnaweza
mkabomoa upande huu na upande huu mkauacha kwa ajili ya hifadhi ya
barabara,” alisema Mchungaji Biyagaza.
“Sisi baada ya hapo tukaona tujipange kwa ajili kuachia eneo la barabara
ili shughuli nyingine ambazo ni mpango wa maendeleo ya serikali ziweze
kuendelea na sisi tuweze kuendelea na eneo letu vizuri. Kwa hivyo kile
kipande chote ambacho ni cha barabara na tukaongeza ndani kidogo chote
tumekiondoa. Na hili eneo linalobaki tunapaimarisha ili nyumba ya Bwana
iweze kufanya kazi yake ya kutoa huduma za kiroho,” aliongeza.
Mchungaji Biyagaza alieleza japokuwa eneo la jengo limepungua, eneo
lililobakia linaimarishwa ili kanisa hilo liweze kuendelea kutoa huduma
za kiroho kwa waumini wake.
Aidha kufuatia zoezi hilo la upanuzi wa barabara ya Morogoro ambalo
linaenda sambamba na ujenzi wa barabara za juu (fly-over) katika
makutano ya barabara eneo la Ubungo, umepelekea kubomolewa kwa majengo
mbalimbali ikiwemo majengo ya wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na
jengo la Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania ambayo yamebomolewa
kufuatia agizo la Rais Dkt. John pombe Magufuli.

Post a Comment