RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesema kuwa licha ya
kuwepo taasisi zinazosimamia haki na sheria lakini bado tatizo la udhalilishaji
kwa wanawake na watoto limeendelea kushamiri katika jamii.
Dk. Shein ameyasema hayo leo katika hafla ya ufunguzi wa
Mahakama ya Watoto huko Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni miongoni mwa
muendelezo wa sherehe za kuadhimisha Siku ya Sheria, Zanzibar kwa mwaka huu.
Katika hotuba yake kwa wananchi, Dk. Shein amesema kuwa
vitendo vya aina hiyo ni kinyume na mafundisho ya dini, malezi pamoja na Katiba
na Sheria zilizopo ambazo baadhi yake zimepata tunzo kwa ubora wake ikiwemo
Sheria ya Mtoto Namba 6 ya mwaka 2011 ambayo imepata tunzo huko Geneva kutokana
na ubora wake duniani.
Hivyo, Dk. Shein amezitaka taasisi zinazosimamia haki na
Sheria kuitumikia Serikali yao kwa uwazi na ukweli kwa lengo la kufikia malengo
yaliowekwa pamoja na kuitaka jamii kutoa mashirikiano katika kuipatia ufumbuzi
changamoto hiyo.
Dk. Shein amesema kuwa Jamii ina dhamana kubwa ya kulea
vyema watoto kwani ni dhahiri kwamba kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha haki
za watoto zinalindwa na maslahi yao yanazingatiwa kuanzia kwenye ngazi za
familia na siyo kwenye vyombo vya sheria pekee yake.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa taarifa za Kitengo cha
Urajisi cha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, zinathibitisha kuongezeka kwa
kesi za aina mbali mbali katika jamii zinazovunja haki za watoto ambazo
zimeripotiwa katika mwaka 2016 ikilinganishwa na mwaka 2015.
Alieleza kuwa katika mwaka 2016, idadi ya kesi za watoto
waliopewa ujauzito zilizoripotiwa ni 26, ikilinganishwa na kesi 19
zilizoripotiwa mwaka 2015 ambapo wamo watoto wa darasa la sita hadi Kidato cha
Nne.
Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein alisema kuwa kuwepo kwa
chombo kinachoonesha vimelea vya urithi vya wazee (DNA) katu sio sababu ya
kumaliza tatizo hilo katika jamii kwani chombo hicho kinasimamiwa na
mwananadamu ambapo jambo kubwa linalotakiwa ni kubadilika na kutofanya kazi kwa
mazoea.
Dk. Shein alisema kuwa fedha nyingi zimetumika katika
ujenzi wa jengo hilo ikiwa ni kwa lengo la kutekeleza haki za watoto sambamba
na kupiga vita udhalilishaji wa watoto kwa kuuondoa kabisa kadhia hiyo huku
akieleza kuwa taasisi husika zitawekwa pamoja katika kutafuta ufumbuzi wa
changamoto hiyo kama alivyofanya kwenye changamoto ya takwimu hivi karibuni.
Nae Jaji Mkuu wa Zanzibar
Omar Othman Makungu alieleza kuwa tayari taratibu zote za kuanzishwa kwa
Mahkama hiyo zimekamilika, zikiwemo za kutoa Tangazo la Kisheria katika gazeti
rasmi la Serikali ikiwa ni pamoja na kumteua Hakimu wa Mkoa wa kuendesha
Mahkama hiyo Nayla Abdulbasit.
Post a Comment