SERIKALI
imeendelea ‘kulibana mbavu’ gazeti la kila wiki la habari za
kiuchunguzi – MwanaHALISI kwa kuliagiza kuchapisha taarifa ya kumuomba
radhi Rais John Magufuli katika ukurasa wa mbele wa toleo lake lijalo, anaandika Charles William.
Agizo hilo limetolewa leo na Dk. Hassan Abbasi, Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, akisema mhariri na mchapishaji wa gazeti hilo wanapaswa kuchapa taarifa ya kumuomba radhi Rais Magufuli katika ukurasa wa mbele pasipo kukosa.
MwanaHALISI
liliingia katika mvutano na serikali mapema Jumatatu ya wiki hii mara
baada ya kuchapisha habari katika ukurasa wake wa mbele iliyokuwa na
kichwa cha habari “Ufisadi ndani ya Ofisi ya JPM.”
Habari
hiyo ilieleza mikataba mbalimbali ya kifisadi iliyoingiwa na Shirika la
Elimu Kibaha lililo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa ambapo mikataba hiyo imeifanya Serikali kuambulia
Sh. 320 milioni tu huku ikidaiwa deni la zaidi ya Sh. 9.7 bilioni.
Kilichoiudhi Serikali
Serikali
kupitia kwa Dk. Abbasi msemaji mkuu, ilieleza kusikitishwa na habari
hiyo kwa maelezo kuwa kichwa cha habari hiyo kililenga kumuhusisha moja
kwa moja Rais Magufuli katika ufisadi huo hasa kutokana na kuwepo kwa
maneno “Ofisini kwa JPM.”
Serikali
ilitoa masaa 24 kwa gazeti hilo kumuomba radhi rais kutokana na taarifa
hiyo, kwani imetengeneza taswira mbaya kwa kiongozi huyo ilihali
ufisadi husika umefanywa na Shirika la Elimu Kibaha lililo chini ya
usimamizi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na si
Ikulu.
Agizo
hilo lilitekelezwa jana na MwanaHALISI kwa kutoa taarifa kwa umma
pamoja na kuandika barua ya kuomba radhi kwenda serikalini.
Ndipo
serikali imeibuka tena leo ikilitaka gazeti hilo kuchapa taarifa hiyo
ya radhi katika ukurasa wake wa mbele kwenye toleo lijalo huku pia
ikipongeza “mwitikio chanya” wa gazeti hilo dhidi ya amri ya serikali.
Utetezi wa MwanaHALISI juu ya kuihusisha Ofisi ya Rais
Gazeti
la MwanaHALISI kupitia Mhariri wake Jabir Idrissa limefafanua kuwa
kutokana na ufisadi husika kufanywa katika miradi ya maendeleo Shirika
la Elimu Kibaha chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais Tamisemi, ndipo
gazeti hilo lilichapisha kichwa husika cha habari katika toleo lake.
Idrissa
amesema kuwa, gazeti hilo limekubaliana na ufafanuzi wa serikali kuwa
Ofisi ya Rais Tamisemi haikupaswa kupewa uzito wa kuitwa “Ofisini kwa
JPM” kwani ofisi halisi ya Rais ni Ikulu (State house) na ndipo
likafikia hitimisho la kuomba radhi.
Itakumbukwa
kuwa, Tamisemi ilikuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika serikali ya
awamu ya nne kabla ya Rais Magufuli kuamua kuihamishia katika Ofisi ya
Rais kwa kile alichokieleza kuwa ni kutaka “kuongeza ufanisi.”
Licha
ya kuhamishiwa katika ofisi ya Rais lakini utendaji wa Tamisemi
unasimamiwa zaidi na Mawaziri husika ambao ni Waziri George Simbachawene
na manaibu wake Angela Kairuki na Selemani Jafo.


Post a Comment