Kutoka kushoto: Baktash Akasha, Gulam Hussein, Ibrahim Akasha and Vijaygiri Goswami
Polisi nchini Kenya inamshikilia mshukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya, Mohamed Jibril aliyekuwa safarini kuelekea Dubai.
Mshukiwa huyo amekamatwa Alhamisi usiku katika uwanja wa ndege wa
kimataifa wa Moi mjini Mombasa akisafirisha dawa za kulevya aina ya
“Heroine” alizokuwa amezificha katika viatu.
Kwa mujibu wa kikosi cha polisi cha kuzuia madawa ya kulevya thamani ya madawa hayo yanakadiriwa kuwa dola 100,000.
Rais Kenyatta aonya
Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahi ya VOA ameripoti kuwa hivi karibuni
Rais Uhuru Kenyatta akiwa Mombasa alikemea vikali ulanguzi wa dawa za
kulevya ambao umekithiri katika eneo la pwani ya Kenya.
“Na mtaona mengine na yale ambayo tumeanza, watu wajue ya kwamba
watatafuta nchi nyingine, sio Kenya kufanya biashara hiyo,” alisisitiza
Kenyatta.
Mwandishi wetu ameongeza kusema kuwa Marekani imekuwa ikiwakosoa watu
mashuhuri nchini Kenya kuhusiana na biashara za dawa za kulevya, ikiwa
pia kuna taarifa kwamba husafirishwa kwa meli.
Familia ya Akasha
Wakati hatua hizo zikichukuliwa tayari wiki hii familia ya Akasha
ambayo watoto wao wawili na washirika wao wawili raia wa nje
wanaoshukiwa kufanya biashara hiyo haramu tayari wamekabidhiwa kwa
serikali ya Marekani.
Baktash Akasha, Ibrahim Akasha, pamoja na raia wa Pakistan, Ghulam
Hussein na Vijaygiri Goswami wa India walikamatwa wiki iliyopita.
Watu hao wanne wanatakiwa kujibu mashtaka katika mahakama moja ya New
York, kwa kuhusishwa na ulanguzi wa biashara haramu ya madawa.
Mama wa watoto hao
Mama wa familia ya Akasha anadai tuhuma hizo za ulanguzi wa kimataifa
wa dawa za kulevya, ni fitina na uzushi mtupu na anaitaka serikali ya
Kenya iingilie kati akitaka watoto wake warudishwe nyumbani.
“Si kweli wanavyotangazwa ni watu wabaya, watu wanatoa maneno ya
uongo uongo, na pia kuleta fitina,” amesema mama huyo Fatma Akasha.
Ameongeza kuwa: “Sidhani kama rais wetu na naibu wake wanafurahia
hilo la kusafirishwa watoto wetu, hawa pia wanaelewa vizuri na
walituhakikishia sisi nchi yetu inajitawala. Naomba basi serikali
inisaidie.”
Post a Comment