
Na: Meshack Maganga – Iringa. Go Big or Go Home
Ndugu zangu, juzi Ijumaa nilikuwa kwenye maongezi ya kawaida na Dada
yangu, mwalimu na mshauri wangu Dada SUBIRA, ambae ndiye mmiliki wa
Blogu ya WAVUTI. Tulikuwa kwenye maongezi ya kifamilia, kisha
nikamshirikisha harakati zangu za ufugaji wa samaki, akapata hamasa,
akaniomba niwashirikishe na Watanzania wenzangu kwa maandishi. Na mimi
nikakubaliana na ombi hilo.
Unaweza kufanikiwa sana tu, unaweza kuwa billionaire ama milionea.
Chunguza marafiki zako na watu unaoshinda nao waliofanikiwa, jifunze
kwao na usipojifunza utaendelea kuwa mlalamikaji.Fursa ya ufugaji wa samaki, kilimo cha miti, kilimo cha nyanya na vitunguu ishakudondokea, usijjite myonyenge, ama maskini maana ‘victim mentality isn’t going to get you anywhere’ GO BIG OR GO HOME.
Ninachokiamini katika maisha yangu ni kwamba, kila mtanzania
anayonafasi kubwa sana ya kuendesha maisha yake ya kila siku bila tatizo
endapo atajitambua na kuugundua ukuu wa Mungu ndani yake. Mwanadamu
yeyote anaetambua uthamani wake na bahati aliyopewa na Mungu ya
kuendelea kuishi na kuzaliwa Tanzania hawezi kuishi maisha ya
kubangaiza.

Katika Makala yangu ya wiki hii ningependa kuwashirikisha kitu kidogo
sana nacho ni UFUGAJI WA SAMAKI KATIKA MAZINGIRA YA KIJIJINI KWA MTAJI
MDOGO SANA… kipindi cha nyuma, nilikuwa nikiwaona watanzania wenzangu
hasa huku Iringa, wakijishughulisha na ufugaji wa samaki, ni miaka
miwili imepita sasa, lakini nilikuwa ‘bize’ na mambo yangu sikutaka
kujifunza Zaidi kuhusu fursa hii. Mwanzoni mwa mwezi wa nane (8) mwaka
jana 2014 rafiki yangu Nicolaus Kulangwa,
ambae huko nyuma alinifundisha kilimo cha Matango,alinipigia simu
akinitaka nikataembelee mradi wake wa kufuga samaki. Nilienda kijini
kalenga hapa Iringa. Nilichokiona nilianza kukifanyia kazi hapohapo na
siku ileile. Wakati rafiki yangu akiwa na jumla ya mabwawa saba ya
samaki aiana ya sato na pelege mimi ndio kwanza nilijutia muda ambao
niliambiwa kuhusu fursa ile halafu nikazembea kuifanya.
Kama tunavyofahamu, lengo la uajasirimali ni kupata faida ya
unachokifanya na kugusa jamii inayo mzunguka mjasirimali. Na kama ilivyo
kwa mifugo mingine yeyote ile, kabla ya kuanza kufuga kuna mambo muhimu
yanayopaswa kuzingatiwa ili ufugaji wako uweze kuwa tija iliyokusudiwa
na hivyo kufikia malengo ya mfugaji huyo. Lakini kutokana na mazingira
ya ufugaji wa huku Iringa hasa Kalenga, nitayataja mambo hayo kwa kifupi
sana, mambo haya huenda yakatofautiana kutoka eneo moja la nchi hadi
jingine, na kwa vile mimi sijasomea chuo cha ufugaji wa samaki, maelezo
haya ni yale niliyoyapata kwa uzoefu tu, siyo ya kufundishwa chuo,
mapungufu yatakayogundulika na ‘wasomi’ wataniandikia email ili
nikawashirikishe wenzangu.
Mambo hayo ni kama ifuatavyo:
- ENEO AMA SEHEMU YA KUWAFUGIA SAMAKI. Inasisitizwa kwamba, eneo hilo liwe na udongo mzuri ambao hautaruhusu maji kupotea hovyo. Udongo wa mfinyanzi ni mzuri na iwapo eneo lako lina udongo wa tifutifu ama udongo wake ni kichanga unashauriwa kujengea kwa simenti ama kuweka ‘kapeti gumu’ lisilo ruhusu maji kupotea.
- UPATIKANAJI WA MAJI, wote tunafahamu kwamba samaki huiishi majini, maji ndiyo roho ya masaki, samaki ni maji na maji ni samaki. Hivyo eneo la kufugia lazima liwe na maji ya kutoshana salama kwa kipindi cha mwaka mzima. Vyanzo vya maji kwa ajili ya ufugaji wa samaki ni kama chemichemi, mito, maziwa na maji ya ardhini hasa visima Kwa maeneo ya huku Iringa, tunabahati ya kuwa na mto Ruaha ambao maji yake yapo muda wote wa kipindi chote cha mwaka. Inashauriwa kwamba eneo hilo liwe salama ili kuwalinda samaki na mfugaji kwa ujumla.
- BWAWA. Bwawa la samaki linahitaji nafasi kubwa ya ardhi, yenye mwinuko pamoja na eneo la samaki kukimbilia. Hii ni njia rahisi ya ufugaji endapo ardhi na maji havina gharama kubwa. Eneo kubwa zaidi linaruhusu uzalishaji usiohitaji nguvu ya ziada na wenye tija.
- MBEGU AMA VIFARANGA, mfugaji wa samaki anashauriwa kutembelea maeneo ambayo wafugaji wakubwa wanazalisha vifaranga ili aweze kupata mbegu bora anayohitaji. Kwa wananaoishi Iringa na maeneo ya jirani, wanaweza kupata mbegu kwa bwana Nicolaus.
- UTUNZAJI WA BWAWA NA USAFI. Ili mfugaji aweze kunufaika na miradi ya kufuga samaki ni lazima uafanye usafi wa kutosha ndani nan je ya bwawa lake. Hasa kwa kuondoa majani ili kuepusha wadudu na viumbe wengine kama konokono,vyura, nyoka, na kenge wasiweze kufanya makazi na hatimaye wakawadhuru samaki. Hivyo, kila unapoona uchafu, safisha mara moja.
- ULISHAJI. Tofauti na mifugo mingine kama kuku, samaki hawahitaji kula chakula kingi sana. Katika hatua za mwanzo ulishaji wake unaweza kuwa mara tatu kwa wiki ama Zaidi.
- AINA YA CHAKULA. Samaki wanaweza kulishwa kwa kutumia pumba ya mahindi, mashudu ya pamba na alizeti, soya, mabaki ya dagaa, Karanga zilizosagwa, unga wa mahindi, mabaki ya chakula kama ugali nk.
- Kuna mambo mengi sana ya kuzingatia unapaanza kufuga samaki, mambo mengine ni kama vile kuzingatia miiundo mbinu, wafanyakazi, kuzingatia masoko, utaalamu nk.
- CHANGAMOTO KATIKA SAMAKI ni magonjwa kama vile magonjwa ya samaki yapo mengi yakiwa nayasababishwa na vimelea vifuatavyo magonjwa yanayosababishwa na bakteria, magonjwa yanayosababishwa na virusi magonjwa yanayosababishwa na minyoo, magonjwa yanayosababishwa na protozoa. na magonjwa yanayotokana na lishe duni. Chanagamoto nyingine ni kama vile, Tatizo mojawapo ni la kuvuja kwa kuta za bwawa. Tatizo hili hutokea iwapo ujengaji wa bwawa haukufuata maagizo na taratibu za ujengaji wa bwawa. Kuna ndege, kenge, fisi maji, nyoka hutokea. Iwapo bwawa lipo mbali na makazi. Kudumaa kwa samaki kutokana na kuwa wengi bwawani kupita idadi inayotakiwa.
- UVUNAJI WA SAMAKI. Hujudi za mfugaji ndio zinaweza kupelekea kuvuna samaki wa kutosha na kumletea faida kwa muda mfupi. Wakati wa kufaa kuvuna samaki bwawani hutegemea ukuaji na aina ya samaki. Ukuaji wa samaki pia hutegemea ubora wa chakula. Samaki wanaofugwa katika bwawa lenye hali nzuri watakuwa tayari kuvunwa baada ya miezi 6 hadi 8. Kuna watakao sema huu ni muda mrefu, ukiona ufugaji wa samaki wanatumia muda jaribu kingine. Ama endelea kukaa nyumbani kwako, ukiisubiri serikali na mashirika ya kijamii yakusaidie.

Nielezee kwa kifupi jinsi ufugaji wa samaki unavyochangia ajira
binafsi kwa watanzania na faida yake kwa ujumla. Changamoto mbalimbali
za kiuchumi, na ukosefu wa ajira kwa wasomi wanaotoka vyuo vikuu kwa
sasa, imesababisha watanzania wengi kuanza kuwa wabunifu na kuanza
kujishughulisha na ujasiriamali hasa kilimo na ufugaji. Kwa sasa mabwawa
mengi yanapatikana katika mikoa sita yenye rasilimali nyingi kama
Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Iringa, Mbeya na Ruvuma. Ufugaji wa
samaki umeenea kote nchini.
Kwa sasa kilo moja ya samaki huuzwa shilingi 7,000/ kwa huku Iringa
na ukiuuzia bwawani kwa jumla ni shilingi 4000/ kwa kilo. Hii ina maana
kwamba ukiwa na kilo mia 7 za samaki una uhakika wa kuwa na milioni
mbili na laki nane kila baada ya miezi sita, kama utauzia bwawani kwa
bei ya shilingi elfu 4 kwa kilo ambapo hii ni samaki watatu tu aina ya
sato, je ukiwa na samaki ama kilo elfu tano? Utagundua kwamba adui wa
mafanikio yako ni sentensi za kizamani ulizo weka kichwani kwako.

Niseme wazi tu kwamba, ufugaji wa samaki, ni fursa nyingine ambayo
ipo wazi kwa kila Mtanzania kuifanya, kuna watakao singizia mitaji, hali
ya hewa nk,lakini ukweli ni kwamba bwawalangu dogo nilitumia pesa ndogo
sana kulichimba ikiwa ni pamoja kununua vifaranga vya samaki.
Tumekuwa watu wa kujiwekea mipaka ya mafanikio vichwani mwetu.
Kumbuka kwamba ukishajiwekea mipaka ya mafaniko. Maisha yetu yataweza
kubadilika iwapo tutabadilisha namna tunavyoyatazama mambo. Kwa mfano
unaweza kuwa umejiwekea mipaka ya kimapato kwamba wewe mwisho wako ni
kupata laki moja, mtazamo huo ukikaa kichwani basi ukiambiwa bwawa moja
linaweza kukutolea shilingi milioni 25 kwa miezi sita, utakataa na hivyo
fursa hiyo itakupita.
Nilipokuwa nikisoma kitabu cha ‘THE TRUTH SHALL MAKE YOU RICH’ cha reallionaire
mdogo kuliko wote Farrah Gray kwa sasa, nimejifunza kwamba, maisha yetu
yanaweza kubadilika muda wowote na dakika yoyote iwapo tutajijengea
Imani kwamba, maisha yanawezekana popote. Na kwa Tanzania hii ambapo
kila mwananchi anaruhusiwa kulimiliki ardhi kwenye mkoa wowote umasikini
litakuwa ni swala la kujitakia.
Ninamalizia makala hii kwa kusema kwamba, kila saa katika maisha yetu
ni fursa, makala hii pia ni fursa kwako na kwangu, kuna baadhi ya nchi
duniani ambapo wananchi wake hawana bahati ya kukaa kwenye meza zao na
kujifunza mambo haya. Kwawatakao penda kuja Iringa, kujifunza ufugaji wa
samaki, tunawakaribisha sana. Nicolaus na mimi na wafugaji wengine
watakusaidia kuapata elimu Zaidi yahii niliyoandika hapa.

Post a Comment