MBUNGE
wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, amesikitishwa na wizi wa
dawa na uharibifu wa baadhi ya vifaa katika Kituo cha Afya cha Murangi,
wilayani Musoma na kuagiza wahusika wachukuliwe hatua.
Muhongo
alitoa agizo hilo mapema wiki hii wakati akikabidhi msaada wa vifaa
mbalimbali vya afya, vikiwamo vitanda maalumu 10 na baiskeli za wagonjwa
vilivyotolewa na wafadhili kutoka Australia kwa ajili ya kituo hicho.
Kabla
ya makabidhiano ya vifaa hivyo, alipokea taarifa kutoka kwa wananchi
kuhusiana na wizi wa dawa uliomhusisha mlinzi wa kituo hicho na
kuharibiwa kwa gari la wagonjwa alilokabidhi Machi, mwaka huu.
Taarifa
hizo zilimkasirisha Profesa Muhongo, ambaye pia ni Waziri wa Nishati na
Madini, hivyo kuagiza wahusika wote wachukuliwe hatua ili iwe fundisho
kwa wenye tabia za namna hiyo.
Akizungumzia
gari hilo, Profesa Muhongo alisema lililotolewa na serikali ya Japan
kwa ajili ya wananchi wa jimbo la Musoma Vijijini ili kusaidia
kuondokana na usumbufu waliokuwa wakiupata.
Mbali
na gari hilo, alisema serikali ya Japan ilimwahidi magari mengine zaidi
ikiwa gari hilo litatunzwa vizuri na kutumika kwa shughuli
iliyokusudiwa.
“Hii
ni aibu kubwa. Hata wafadhili watatushangaa na kutucheka, dawa nyingi
tulipewa na wafadhili na gari lile tulikabidhiwa likiwa bado jipya na
kwa Tanzania magari ya namna hiyo yapo mawili tu, ni hapa na Muhimbili,”
alisema.
Aliongeza
kuwa serikali ya Japan ilitoa Sh. milioni 170 kwa ajili ya kuboresha
kituo hicho cha afya na kuongeza kuwa atamwomba Balozi wa Japan nchini
kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha hizo.
Profesa
Muhongo aliwaagiza madiwani kufuatilia ili kubaini hatua iliyofikiwa ya
matumizi ya fedha hizo na kwamba endapo itadhihirika kuna ubadhirifu wa
aina yoyote, hatua za kisheria zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kurejesha
fedha hizo.
Alisema
anashangazwa kupewa taarifa hizo na wananchi huku viongozi wakiwa kimya
bila kuonyesha hatua walizochukua, hivyo kuwataka madiwani kutokuwa
waoga katika kuwachukulia hatua wanaofanya ubadhirifu.
Pia
aliwaagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk. Thadeus Makwanda,
na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Murangi, Dk. Josephat
Karambo, kuhakikisha hadi Januari 15, mwakani, gari hilo liwe
limetengemaa.
Post a Comment