RAIS Dk. John Magufuli anauma na kupuliza. Ndivyo unavyoweza kutafsiri
mwenendo wa uamuzi wake wa kutengua uteuzi watendaji mbalimbali
serikalini na baadaye kuwapa baadhi yao nafasi nyingine za uongozi.
Baadhi ya watumishi waliwajibishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, huku wengine wakichukuliwa hatua na mawaziri.
Rais Magufuli hakuishia serikalini tu, akiwa Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), pia ameanza kukisafisha chama hicho kwa lengo la
kufanya mabadiliko makubwa.
NDANI YA SERIKALI
Kwa upande wa watendaji serikalini, wapo baadhi aliotengua uteuzi wao na
kuwaahidi kuwapangia kazi nyingine na wengine pasipo kuwaahidi
chochote, wakiwamo wale aliowatumbua kwa makosa mbalimbali ya uzembe na
ubadhirifu.
Pamoja na kuwatumbua watendaji hao kwa nyakati tofauti, Rais Magufuli
ameamua kuwarudisha mmoja baada ya mwingine kwa muda wake ili kutumikia
nafasi nyingine za utumishi wa umma.
Mmoja wa watendaji wa Serikali waliokumbwa na machungu ya kutenguliwa
kabla ya kupozwa ni Profesa Yunus Mgaya aliyekuwa Katibu Mtendaji wa
Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
Profesa Mgaya alirejeshwa kundini wiki iliyopita kwa kuteuliwa kuwa
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Tiba na Magonjwa ya Binadamu
(NIMR) akichukua nafasi ya Dk. Mwele Malecela ambaye Rais Magufuli
alitengua uteuzi wake.
Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa akitoa taarifa za kutumbuliwa watendaji
mbalimbali serikalini, naye alionja machungu baada ya mapema mwaka huu
Rais Magufuli kutengua uteuzi wake katika nafasi yake ya Katibu Mkuu
Kiongozi.
Lakini baada ya miezi kadhaa kupita, Rais Magufuli aliamua kumpoza kwa kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Diplomasia.
Rais Magufuli alifanya uamuzi kama huo kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Ramadhan Dau.
Dk. Dau aliyetumikia nafasi hiyo kwa takriban miaka 19, aliondolewa katika nafasi hiyo mapema mwaka huu kabla
miezi michache baadaye kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia.
Mwingine ni Diwani Athuman aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa
ya Jinai (DCI), ambaye alitenguliwa uteuzi wake na Rais Magufuli.
Lakini maumivu hayo yalipozwa ndani ya wiki chache tu baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.
Sylvester Ambokile ambaye Rais Magufuli alitengua wadhifa wake wa
Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, naye amepozwa kwa kuteuliwa kuwa balozi.
Pia Balozi Peter Kallaghe aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza,
naye nafasi yake ilitenguliwa na Rais Magufuli mwanzoni mwa mwaka huu,
lakini hivi karibuni alimpoza kwa kumteua tena kuwa Ofisa Mwandamizi
Mwelekezi–Mambo ya Nje katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC).
Ado Mapunda ni miongoni mwa watendaji wa Serikali walioumwa na Rais Magufuli na kisha kupulizwa.
Awali Mapunda alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, lakini akajikuta
akiwa mmoja kati ya makatibu tawala 10 walioachwa katika uteuzi mpya wa
Rais Magufuli alioufanya Aprili mwaka huu, akiahidiwa kupangiwa kazi
nyingine.
Septemba mwaka huu, Mapunda alijikuta akiteuliwa tena kushika nafasi
hiyo, lakini safari hii akipelekwa Mkoa wa Mara kuchukua nafasi
iliyoachwa wazi na Benedict ole Kuyan ambaye amestaafu.
NDANI YA CHAMA
Duru za siasa zinasema, uamuzi wa Rais Magufuli kumwondoa Rajabu Luhwavi
katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara na kumteua kuwa balozi,
ni kiashiria kimojawapo kinachojenga taswira ya uamuzi wake wa kuuma na
kupuliza.
Pia duru hizo zinasema uamuzi wake wa kuwateua wajumbe wa Kamati Kuu ya
CCM kama Dk. Pindi Chana na Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa mabalozi,
kunajenga tafsiri nyingine ya mtazamo huo wa kuuma na kupuliza.
Ni wazi kuwa kupitia uteuzi huo, kwa namna moja au nyingine kunaleta
ugumu kwa makada hao kuhudhuria vikao vya uamuzi ndani ya CCM.
Pia uamuzi wa Rais Magufuli kumteua aliyekuwa Msemaji wa CCM,
Christopher ole Sendeka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, unachukuliwa kama
sehemu ya tafsiri ya uamuzi huo huo wa kung’ata na kupuliza.
MAONI YA WASOMI
Mtazamo wa maamuzi ya Rais Magufuli ya kuuma na kupuliza kwa maana ya
kutengua na kuwarudisha baadhi ya watendaji wa taasisi za umma,
umewavuta wasomi na wataalamu wa sayansi ya siasa, ambao kwa nyakati
tofauti wametoa maoni yao.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Bashiru Ally, alisema katiba na historia ya nchi zinaipa
mamlaka makubwa taasisi ya urais.
“Huyu ni rais wa tano tangu tumepata uhuru kwa upande wa Jamhuri ya
Muungano… nguvu hizo hizo na mamlaka hayo hayo yametumiwa na marais wote
waliopita, hakuna rais ambaye hakufukuza na kurudisha, hakuna rais
ambaye hakuhamisha, hakuna ambaye hakutumbua na hakuna jambo lolote
jipya ambalo analifanya Magufuli ambalo halikufanywa na Nyerere.
“Zinaweza kuwapo tofauti za kimtazamo na mwelekeo au kwa mtindo na
itikadi na falsafa, lakini linapokuja suala la kufukuza, kuteua,
kupandisha vyeo au kushusha vyeo, marais wote watano wamefanya hivyo.
“Kwahiyo mtu anayetaka kutumia historia ya nchi, taasisi za kikatiba,
sheria na mamlaka yaliyopo kwenye hiyo taasisi ya urais, hakuna jambo
lolote ambalo amelifanya Magufuli halikufanywa na Nyerere, Mwinyi, Mkapa
au Kikwete,” alisema Bashiru.
Naye Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu, alisema hatua
zinazochukuliwa ni nzito, lakini hazina maandalizi au umakini katika
kufanya uamuzi mkubwa wa kutengua na kuteua.
Alisema hali hiyo inazalisha tatizo kubwa katika utumishi wa umma na
katika uchumi wa nchi, kwa sababu hali hiyo ni sawa na kujenga mazingira
ya sintofahamu ambayo kwa vyovyote yanaathiri utendaji na tija ya
utekelezaji, ufuatiliaji na uwajibikaji wa shughuli za umma.
“Kwa mtazamo wangu, hilo ni tatizo kubwa kwa sababu uamuzi huo
unatetemesha hali ya utendaji katika Serikali. Pia nadhani hata hii
tumbua tumbua ambayo msingi wake haueleweki, mara nyingi Watanzania
wamekuwa wanatangaziwa tu fulani katumbuliwa, fulani katumbuliwa, lakini
haionekani wazi wazi ni sababu gani, kama ni mtu mzembe au katumbuliwa
kwa sababu ya ufisadi.
“Mara nyingi hii haiwekwi wazi kama mtu katumbuliwa kwa sababu gani na
amepewa nafasi ya kujitetea akashindwa kujitetea au kaonekana anakwenda
kinyume na matakwa ya rais.
“Hii inatakiwa iwekwe wazi ili watu kwenye utumishi wa umma waweze
kujifunza na kuepuka madhambi waliyoyafanya wenzao. Lakini bila kuwa na
uwazi ni vigumu kwa wengine kujua kwamba jambo fulani ni kosa ambalo
linafanya utumbuliwe,” alisema.
Aliongeza kuwa uamuzi wa rais wenye tafsiri ya kuuma na kupuliza, unatoa
mtazamo kuwa anauma bila kutenda haki, hivyo inambidi arudi nyuma
apulize jeraha.
Post a Comment