\
MKUU wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, ametoa wiki mbili kwa wakazi wa
Jimbo la Ruangwa ambalo mbunge wake ni waziri mkuu wa Jamhuri ya
muungano wa Tanzania Kasim Majaliwa kuhakikisha wanajenga vyoo
kujiepusha na ugonjwa wa kipindupindu.
Pamoja na hatua hiyo, Zambi amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Joseph
Mkirikiti afanye msako wa nyumba kwa nyumba ifikapo Januari 15, mwakani
na endapo atakuta kuna mkazi wa kijiji chochote hajajenga choo, basi
atozwe faisi ya Sh 50,000 mara moja.
Kauli hiyo aliitoa jana wilayani hapa wakati akizungumza na wananchi wa
vijiji vya Namilema, Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera, Muhuru, Chikundi
na Chibula wakati akiwasalimia wananchi kabla ya kumkaribisha Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa azungumze na wakazi wa vijiji hivyo.
Waziri Mkuu yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka
na ameamua kutumia muda huo kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na
kuhimiza kazi za maendeleo.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema wakulima wengi wamevuna korosho msimu huu na
baadhi yao wamelipwa vizuri, hivyo hawana budi kutumia sehemu ya fedha
hizo kujenga vyoo ili kujiepusha na magonjwa ya mlipuko na hasa
kipindupindu.
“Hili ni agizo la Serikali siyo langu binafsi, kwa hiyo ni amri halali. Kikilipuka kipindupindu naanza na Mkuu wa Wilaya kabla na mimi sijaulizwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu au Mheshimiwa Rais,” alisema.
Katika hatua nyingine, Zambi amewahimiza wakazi wa vijiji hivyo wapande
miche ya mikorosho katika msimu huu wa kilimo pindi mvua zitakapoanza
kwani iliyopo imekaa kwa zaidi ya miaka 50 na sasa haizai matunda ya
kutosha.
“Mkoa wetu una mpango wa kubadilisha miti ya mikorosho kwani mingi ni ya
zamani na imekaa kwa zaidi ya miaka 40 hadi 50 na hivi sasa haina tija
kwenye mazao yake. Mti mzuri wa korosho unazaa hadi kilo 40, lakini hii
iliyopo sasa hivi inatoa kilo 10 tu,” alisema.
Post a Comment