Baadhi ya Viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar
wametakiwa kuacha tabia ya kutumia mitandao ya kijamii kujadili masuala
yanayohusu Chama badala yake watumie vikao halali vinavyotambuliwa na
Katiba ya Chama hicho.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai
wakati akifunga Mkutano wa Viongozi wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa
Kusini Unguja Kichama uliofanyika katika Shule ya Msingi Makunduchi
Mkoani humo.
Alifafanua kwamba tabia hiyo ya kujadili, kukosoa na kuwatuhumu baadhi
ya viongozi wa ngazi mbali mbali wa Chama na Jumuiya zake kupitia
Mitandao ya kijamii ni utaratibu unaokwenda kinyume na miongozo ya chama
hicho.
Alisema Katiba ya CCM inaelekeza Kwamba mambo yote yanayogusa maslahi
mapana ya Chama yajadiliwe Katika Vikao halali vinavyotambuliwa na
kanuni za Chama, kwani jukwaa hilo ndiyo sehemu rasmi ya kukosoana na
kupeana maelekezo.
Vuai alisikitishwa na tabia hiyo na kueleza kuwa njia pekee ya kumaliza
Changamoto hiyo ni Wanachama na Viongozi kujenga utamaduni wa Kusoma na
kuelewa Kanuni, Katiba na miongozo mbali mbali ya CCM ili kufahamu
wajibu, majukumu, haki na maadili yanayoongoza Chama.
Alisema tabia hiyo imekuwa ikifanyika katika Magroup ya Mitandao ya
kijamii zikiwemo Facebook, WhatsApp na mitandao mingine, jambo ambalo ni
kosa kwa mujibu wa kanuni za Chama.
“ Wanachama, Viongozi na Watendaji naomba muelewe kwamba hiki Chama
kinaendeshwa kwa utaratibu maalum ulioelezwa Kikatiba , Kikanuni na
miongozo mbali mbali, kwa nia ya kulinda hadhi na heshima ya Chama
chetu, na hakuna jambo lolote linaloshindikana kupatiwa ufumbuzi kupitia
utaratibu huo.
"Sasa panapojitokeza baadhi ya Watu miongozi mwetu wakaanza kujadili na
kuwakosoa wenzao nje ya mfumo huo basi hao tunawahesabu kuwa wana nia
ya kuanzisha Majungu, Fitna na mpasuko katika taasisi yetu.”, alieleza
Vuai na Kuongeza kuwa CCM ni Chama imara na kinachoheshimu Demokrasia
katika kujadili mambo yake na kuyatolea maamuzi stahiki katika Vikao
rasmi na sio vichochoroni au vibarazani.
Aliongeza kuwa sio kwamba kuna viongozi na wanachama wanaogopa ama
hawataki kukosolewa lakini lazima heshima na nidhamu iwepo katika
kutekeleza matakwa ya Demokrasia ndani ya Chama hicho kwa kuheshimu
utaratibu uliowekwa Kikatiba.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho ya mwaka
2015/ 2020 katika Mkoa huo aliwapongeza Viongozi wa Majimbo wakiwemo
wabunge, wawakilishi na Madiwani huku akiwasisitiza Viongozi wa Chama
kuhakikisha wanakagua kikamilifu miradi inayotekelezwa na viongozi hao
ili kujiridhisha kama inawanufaisha wananchi wote.
Aliwataka viongozi wa Chama na Jumuiya zake kuwa wa kwanza kutambua kero
na changamoto za wananchi wa maeneo mbali mbali na waziwasilishe kwa
Wakuu wa Wilaya (DC) ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na
Serikali.
“ Huu sio wakati wa kusubiri taarifa zinazohusu Changamoto za Chama,
Jumuiya na Serikali ziletwe Ofisini, badala yake mtoke na kuzitafuta
wenyewe ili kuwasaidia wanachama na wananchi kutatuliwa kero zao kwa
haraka kupitia Mamlaka husika.”, alisisitiza Vuai.
Alisema Viongozi wanatakiwa kufahamu kwamba suala la kuwatumikia
wananchi sio jambo la hiari bali ni lazima watekeleze kwa vitendo ahadi
walizotoa wakati wa kampeni kwani wasipotekeleza Wajibu wao vizuri kwa
jamii mwisho wa siku kitakacho hukumiwa ni Chama na sio kiongozi husika.
Aidha aliwakumbusha viongozi hao kwamba Chama na Jumuiya zake
wanatarajia kufanya Uchaguzi mwaka 2017, hivyo waanze mapema
kuwaelimisha, kuhamasisha na kuwaandaa kisaikolojia wanachama wa Chama
hicho juu ya matumizi sahihi ya kanuni za UChaguzi ili kuepuka lawama
zisizokuwa za lazima.
Alisema Wanachama wanatakiwa kuwachagua viongozi wenye sifa na wasiokuwa
na Mukhari( kuoneana haya) katika kusimamia mambo ya msingi ya CCM na
waumini wa kweli wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Muungano wa
Serikali mbili wenye vigezo hivyo ndio wanaofaa kuwa viongozi.
Hata hivyo aliwapongeza Rais wa Zanzibar, Dkt. Shein na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt. Magufuli kwa juhudi na kasi zao za
kufanikisha mipango ya maendeleo ya nchi kwa ufanisi mkubwa hali
inayoongeza hamasa kwa jamii kuendelea kuwaamini.
Post a Comment