RATIBA ya msimu wa ukeketaji unaotarajia kufanyika mwishoni mwa mwaka huu imevuja katika wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Mkuu
wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga amesema hayo wakati alipozungumza
katika mkutano maalumu ulioandaliwa na Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto
(CDF) kwa ufadhili wa Shirika la Foundation for Civil Society mjini
Tarime juzi.
Luoga amewataka wadau wote kushiriki katika kutokomeza tatizo la ukeketaji katika wilaya hiyo.
“Ni
jambo la aibu sana kuona watu wanatoa ratiba ya ukeketaji Tarime. Kila
mdau akitimiza wajibu wake tutamaliza tatizo la ukeketaji Tarime,”
alisema Luoga katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na vingozi wa dini,
wazee wa mila na maofisa wa serikali ambao wanahusika katika masuala ya
ulinzi wa mtoto.
Amesema
ameagiza Jeshi la Polisi kuwa katika hali ya tahadhari katika kuzuia
vitendo vya ukeketaji na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha.
“Baada
ya kupata taarifa kuwa ratiba imetoka, tumefanya kikao na
tumewashirikisha wazee wa mila, lakini pia nimemuagiza OCD kuhakikisha
tunazuia watoto wa kike kukeketwa,” amesema Luoga.
Mkurugenzi
Mtendaji wa CDF, Koshuma Mtengeti alitumia fursa hiyo kutambulisha
mradi mpya ambao unalenga kuimarisha ulinzi wa mtoto wa kike katika kata
tatu za wilaya ya Tarime ambazo ni Turwa, Bomani na Nyamisangura.
Mradi huo wa miaka mitatu utafadhiliwa na Shirika la Foundation for Civil Society, kwa mujibu wa Koshuma.
Post a Comment