Hatua
hiyo inatokana na kauli ya Makonda kuwatuhumu Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Sirro na Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi Suzan Kaganda, kulegalega
kusimamia suala hilo huku akihofia wanaweza kuwa wamehongwa na watu
waliotaka kumhonga lakini akakataa.
Waziri
Mkuu Majaliwa alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Mradi wa
Uboreshaji wa Miundombinu ya Umeme katika Jiji la Dar es Salaam.
Alisema
katika udhibiti wa suala la shisha, mkuu huyo wa mkoa amefanya kazi
nzuri, na kwamba kwa kuwa ameshatoa maelekezo, akiwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Makonda hana budi kuyatekeleza.
Alisema
alivyosikia anawaagiza wakuu wake wa wilaya wote kusimamia maagizo yake
na kama hawakusimamia atachukua hatua, basi naye atachukua hatua kwake
(Makonda) asipotekeleza suala hilo ambalo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni
tatizo kubwa.
“Sasa
mimi nasema nakuagiza wewe usimamie na kama hutasimamia suala hilo
nitakuchukulia hatua, hivyo hangaika na shisha kwa wanaopuliza wakiwa
wamelala hakikisha unawadhibiti,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa wakati
akijibu sehemu ya salamu za Makonda alipopewa fursa ya kusalimia
wananchi katika hafla hiyo.
Katika
salamu zake, Makonda alisema Waziri Mkuu alipiga marufuku matumizi ya
shisha, hivyo alimwagiza Kamanda Sirro kuhakikisha suala hilo
linatekelezwa kwa kiwango kikubwa.
“Lakini
Waziri Mkuu nimeshangaa kupita katika baadhi ya maeneo na kuona watu
wameanza tena kuvuta shisha na nilipouliza wakasema wewe ndiyo umetoa
kibali cha shisha,” alieleza Makonda na kuongeza alishangaa Waziri Mkuu
alipiga marufuku shisha, ni lini ametoa kibali kuanza kutumika.
Lakini
mkuu huyo wa mkoa alienda mbali zaidi na kudai kuna kikundi cha watu 10
waliokwenda kwake ambao anawatambua kama “maajenti wa shetani” ambao
wanapata faida kati ya Sh milioni 35 mpaka Sh milioni 45 kwa mwezi
kutokana na dawa hizo za kulevya.
Alidai
watu hao walipanga mikakati ya kumshawishi kupokea Sh milioni tano kwa
kila mmoja kwa mwezi yaani Sh milioni 50 ili asipige kelele kuhusu
shisha na wao waendelee kupata faida. “Shisha imerudi katika Mkoa wa Dar
es Salaam na nimeshamuagiza Kamishna Sirro, lakini nimeona kama ana
kigugumizi… lakini sijajua kama hizi tano tano zimepita kwake na pia RPC
wa Kinondoni nimemuona hapa, lakini hawa wana kigugumizi sijui kama
hizi tano tano zimepita kwao,” alisema Makonda.
Alisema
aliamua kufanya ziara mwenyewe na kushuhudia watoto wadogo wanavuta
shisha, hivyo uwezekano miaka 10 ijayo vijana wengi kuwa matatizo ya
afya, hivyo kumwomba Waziri Mkuu kutochoka kusimamia suala hilo na
taasisi zote ili likome katika mikoa yote.
Kuhusu
wafanyabiashara wadogo, alisema suala hilo linamnyima usingizi na kutoa
rai kwa wakuu wa wilaya kuwa, kama kuna mkuu wa wilaya atachelewa
kutekeleza yale aliyoagiza kuwapeleka machinga katika maeneo
yaliyoruhusiwa atachukua hatua kabla ya Waziri Mkuu kufanya hivyo.
Source: Habari Leo