WASOMI,
wadau wa elimu na wananchi wa kawaida wamekosoa tamko la Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, wakisema kwamba
halijafanyiwa utafiti na halitekelezeki kisheria.
Mwishoni
mwa wiki, akiwa kwenye mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT),
Profesa Ndalichako alisema kuanzia mwakani mwanafunzi yeyote hatajiunga
na masomo ya Shahada bila kupitia kidato cha sita.
Alisema mfumo wa elimu huria umechangia kuzalisha wasomi butu kwa kupokea wanafunzi dhaifu kitaaluma.
Wakizungumzia
tamko hilo kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali nchini, baadhi
ya wasomi walisema kabla ya waziri kuanza kutoa amri na matamko,
alitakiwa kufanya utafiti kujiridhisha juu ya agizo lake hilo.
“Profesa
Ndalichako hajasema ametoa wapi ujasiri wa tamko lake, ni kwa utafiti
upi aliofanya yeye au hata kukasimu taasisi kwa niaba yake ili ifanye
utafiti na kuja na majibu kuwa kidato cha sita ndicho kiwango bora cha
kumpitisha mtu kusoma shahada ya kwanza?
“Binafsi
naona haya ni matamko ya kisiasa yasiyoweza kutekelezwa kisheria,
arekebishe sheria kwanza ndio aje kutoa tamko la kurekebisha mfumo wa
elimu, vinginevyo anaweza kuharibu kuliko waliomtangulia,” alisema mkuu
wa chuo kikuu maarufu mkoani Arusha ambaye hakutaka kutajwa jina lake
gazetini.
Naye
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Tawi la Makumira, Mchungaji Profesa
Josef Parsalao, alisema pamoja na lengo zuri la kurekebisha mfumo wa
elimu, badala ya kuanza na amri na matamko, Serikali ilitakiwa
kurekebisha kasoro zilizopo hatua kwa hatua.
“Sijui
yeye Ndalichako alipitia hatua zipi za elimu, lakini upo ushahidi wa
kuwapo kwa wasomi wengi wakiwamo wale wanaofundisha vyuo mbalimbali
nchini, kupitia ngazi ya chini kabisa ya cheti na sasa ni maprofesa na
walifundisha hawa wanaobeza ngazi hizo.
“Wapo
majaji ambao walianza kazi ya ukarani mahakamani, wakajiendeleza kwa
kusoma Chuo cha Mahakama Lushoto ngazi ya cheti, sasa ni madaktari na
maprofesa wa sheria tunawategemea,” alisema Profesa Parsalao.
BANA
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, yeye alisema haamini
kama alichosema Waziri Ndalichako ni tamko na uamuzi wa Serikali, kwani
suala hilo haliko kwenye sera ya elimu na kuonya kuwa alifute haraka
kwani hiyo si njia sahihi ya kuboresha elimu nchini.
Dk.
Bana alikwenda mbali zaidi kwa kutoa mfano wa jinsi yeye alivyosoma
kupitia mfumo huo unaopingwa na Ndalichako hadi hapo alipofikia.
“Kama
kachukua uamuzi huo, nafikiri amekurupuka, kama anafikiria kidato cha
sita ndiyo njia pekee, ameshauriwa vibaya na huo uamuzi aufute haraka
sana na ni kinyume na utaratibu wa elimu kote duniani… utakuwa ni uamuzi
wa dhambi ya asili na dhambi ya ubaguzi. Kama anataka njia ya kuboresha
elimu aje tumfundishe.
“Mimi
binafsi sikupitia kidato cha sita na kuna maprofesa zaidi ya 20 au 40
ninaowafahamu, yupo Profesa Baregu (Mwesiga Baregu) hakusoma kidato cha
sita, kuna Profesa Mathew Luhanga ambaye alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa miaka 14, yupo pia Profesa Cuthbert
Kimambo ambaye alikuwa Mkuu wa Taaluma UDSM na wengine wengi, ni watu
wanaoheshimika kote duniani,” alisema.
PROFESA BAREGU
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu,
hakutofautiana na Dk. Bana. Yeye alisema mfumo uliopo unakubalika
duniani kote na ndio ulioleta msemo wa ‘elimu haina mwisho’.
“Kauli
ya waziri imeonyesha umuhimu wa kuwa na tume ya kitaifa ya
kushughulikia suala la elimu, kwa sababu kweli kuna tatizo la ubora wa
elimu yetu na halipaswi kunyamaziwa, lakini hii si njia sahihi ya
kulitatua.
“Sijamwelewa
waziri kwanini ameona diploma kwenda chuo kikuu ndiyo tatizo na kusema
kuwa watu wote wana haki ya kujengewa mazingira ya kujiendeleza
kielimu,” alisema Profesa Baregu.
PROFESA MPANGALA
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa (RUCO), Profesa Gaudence
Mpangala, alisema anapinga uamuzi huo wa Profesa Ndachako kwani
utawanyima watu uhuru wa kujiendeleza.
Profesa
Mpangala naye aliwataja baadhi ya maprofesa anaowafahamu ambao
hawakupitia kidato cha sita na akasema wamekuwa msaada mkubwa kwa taifa.
“Profesa
Kimambo alikuwa mwalimu wangu wa Kiswahili, yeye alikuwa na elimu ya
ualimu ‘Grade’ C wa shule ya msingi lakini amejiendeleza hadi amekuwa
Profesa yupo pia Profesa Ndunguru na wengine wengi na waliopitia mfumo
wa Cheti-Stashahada wanakuwa na uzoefu mkubwa kuliko wa kidato cha sita
na wanafanya vizuri wakifika chuo kikuu,” alisema Profesa Mpangala.
TAMONGSCO
Akizungumzia
kauli hiyo ya Profesa Ndalichako, Katibu Mkuu wa Vyuo na Shule Binafsi
Tanzania, Benjamini Nkonya, alisema hawaelewi waziri huyo kutoa tangazo
kama hilo ni kwa sababu watu wengi wamekuwa watumishi bora sana na wengi
hawajasoma kidato cha sita au vinginevyo.
“Wito
wetu kwa Serikali ikamilishe mchakato kwa kupeleka rasimu ya sheria
mpya ya elimu bungeni, ili pawepo na Baraza la Taifa la Elimu ambalo
litakuwa na wawakilishi kutoka sekta ya umma, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na sekta binafsi kama TAMONGSCO, ambayo
itaandaa nyaraka (regulations) zote kabla hazijawekewa sahihi na
kamishna wa elimu,” alisema Nkonya.
PROFESA MLAMA
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Penina Mlama, yeye
alikubaliana na mawazo ya Waziri Ndalichako, akisema mfumo huo ni wa
zamani na uliruhusiwa ili kutoa fursa kwa watu kusoma kwa kuwa nchi
ilikuwa na wasomi wachache.
“Sasa
hivi kuna wanafunzi wengi wa kidato cha sita na fursa nyingi za kusoma
kidato cha tano na sita zipo, tofauti na kipindi cha miaka ya nyuma,
hakuna ulazima sana wa watu kutegemea njia yingine wakati wanaweza
kusoma kidato cha sita na kuwa sawa na wengine darasani,” alisema.
LALTAIKA
Kaimu
Mkuu wa Idara ya Ubunifu, Usimamizi wa Teknolojia na Ujasiriamali
katika Taasisi ya Sayansi ya Nelson Mandela, Dk. Amani Laltaika,
alipongeza hatua ya Profesa Ndalichako, huku akisema amegundua tatizo
katika elimu na amethubutu kuchukua hatua ya kurekebisha kuliko
waliomtangulia ambao hawakuchukua hatua yoyote.
“Sifa
ya kwanza ya kiongozi ni ubunifu na kutatua matatizo yaliyopo,
nampongeza waziri kwa kugundua upungufu katika elimu yetu, kwa sababu
walikuwapo mawaziri wengi katika nafasi aliyopo sasa, lakini
hawakugundua,” alisema Dk. Laltaika.
SIFA ZA TCU KUJIUNGA NA VYUO
Mwezi
Juni mwaka huu, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), ilitangaza utaratibu
mpya kwa watahiniwa wa mwaka mpya wa masomo wa 2016 na 2017 wanaochukua
shahada.
Utaratibu
huo mpya ulikuja baada ya miezi miwili tangu kutumbuliwa kwa watendaji
wa tume hiyo kutokana na kudahili wanafunzi wasio na sifa na kusababisha
kupewa mikopo na Bodi ya Mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Pamoja
na sifa hizo ambazo ziliwahusu waliomaliza kidato cha sita, pia sifa
hizo zilieleza kuwa wale watakaodahiliwa kujiunga na vyuo ni pamoja na
watakaokuwa na utambulisho wa sifa za kielimu za kidato cha nne kuanzia
alama nne ambazo ni D na kupanda juu katika mchanganuo wa alama za
ufaulu wa B+, ikiwa A=75-100, B+=65-74, B=50-64, C=40-49, D=35-39 na
F=0-38.
Sifa
nyingine zinazotajwa ni wenye vyeti vya NVA daraja la tatu, wenye
ufaulu si chini ya alama nne au sifa nyingine zinazokaribiana na hizo,
ikiwa ni pamoja na zinazotambuliwa na Baraza ka Taifa la Mitihani
(NECTA) na Elimu ya Mafunzo ya Ufundi (VETA).
Watahiniwa
hao watatakiwa kuwa na angalau GPA ya 3.5 kwa stashahada ‘NTA’ daraja
la sita au wastani wa B kwa cheti cha ufundi ‘FTC’ katika mchanganuo wa
alama A=5, B=4, C=3 na D=2 au wastani wa daraja la B+ kwa wenye
stashahada za ualimu au wastani wa daraja B+ kwa kitengo cha afya kama
tabibu wa magonjwa ya binadamu na nyingine au cheti na stashahada
nyinginezo.
Sifa
nyingine zinazoangaliwa katika udahili huo ni pamoja na kuwa na ufaulu
wa daraja la pili kwa wenye Stashahada zisizokuwa za NTA.
Imeandaliwa na Abraham Gwandu (Arusha), Jonas Mushi na Mauli Muyenjwa (Dar)-Mtanzania
Post a Comment