Jeshi
la polisi mkoa wa Singida, linamshikilia askari mgambo mwajiriwa
hospitali ya mkoa, MG 7822 Emmanuel Daghau (42) kwa tuhuma ya kutoa
taarifa za uongo juu ya maiti kufufuka ikiwa kwenye chumba cha
kuhifadhia maiti cha hospitali ya mkoa.
Imedaiwa
kuwa uongo huo ulizua mtafaruku mkubwa kwa ndugu na jamaa wa merehemu
Rahel Erasto (28), aliyekuwa mkazi wa Minga manispaa ya Singida.
Kaimu
kamanda wa polisi mkoa wa Singida, SSP Mayala Towo, alisema tukio hilo
limetokea Septemba, 30 mwaka huu, majira ya alasiri huko katika
hospitali ya mkoa mjini hapa.
Akifafanua,
kaimu kamanda huyo alisema kuwa Septemba, 29 mwaka huu Rahel (marehemu)
alifikishwa katika hospitali hiyo ya mkoa, kwa ajili ya kupata huduma
za kujifungua salama.
“Kutokana
na sababu za kitabibu Rahel, alishindwa kujifungua kwa njia ya kawaida
na hivyo ililazimika kufanyiwa upasuaji ambapo mtoto wa kiume alitolewa
akiwa hai, Lakini mama kwa bahati mbaya alifariki dunia usiku saa saba
Septemba, 30. Mimba hiyo ilikuwa ya kwanza kwa marehemu Rahel,” alisema kaimu kamanda huyo.
Akifafanua
zaidi, alisema kuwa baada ya Rahel kufariki dunia, mwili wake
ulipelekwa mochwari ambapo kesho yake, ndugu walijikusanya eneo hilo
wakijadiliana namna kuuchukua mwili kwa ajili ya kwenda kuzika.
Alisema
kuwa wakati ndugu wakiendelea kuzungumzia masuala ya mazishi,
alijitokeza mlinzi Daghau na kuwaeleza kuwa ndugu yao huyo, alifariki
kutokana na uzembe na kwamba usiku akiwa kwenye doria za kawaida,
alisikia marehemu akipiga chafya na aliposogelea dirishani, alimwona
akiwa amefufuka.
Towo
alisema kuwa awali mgambo huyo baada ya kuhojiwa na Polisi, alikiri
kumwona marehemu huyo akiwa amefufuka na alisikia akipiga chafya.
Alikiri kwa maandishi na kuweka saini yake.
Alisema
lakini baada ya Emmanuel kubaini kuwa baadhi ya ndugu wa marehemu na
watoa huduma za afya hospitali ya mkoa kudai kuwa Rahel amefariki dunia
kutokana na matatizo ya kawaida ya uzazi na wala hakufa na kufufuka,
alipohojiwa mara ya pili, alikana maelezo yake ya awali aliyotoa kwa
Polisi.
Wifi
wa marehemu Rahel, Mary Mpaki, alikiri kuwa alimsikia mlinzi Emmanuel
wakati akiwatangazia waombolezaji kuwa marehemu amefariki dunia kutoka
na uzembe wa madaktari, na kwamba alipelekwa chumba cha kuhifadhia maiti
akiwa hai.
“Kama
ndugu wa marehemu ambao baada ya kufanyiwa upasuaji kuna ndugu ambao
walitaka kulala wodini lakini hawakuruhusiwa.Tuliposikia maneno ya
mlinzi huyo, tuliamini kwa asilimia mia moja maneno yake kwamba Rahel
alipelekwa mochwari akiwa bado yu hai,” alisema kwa masikitiko.
Mary alisema baada ya taarifa ya mlinzi huyo, walienda moja kwa moja kituo cha Polisi kutoa taarifa hizo za kusikitisha.
Ndugu
wa marehemu ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema taarifa
iliyotolewa na mlinzi kuwa Rahel alifufuka na kupiga chafya, zitakuwa ni
za ukweli kwa sababu Ni mtu mwenye akili, hawezi kudanganya jambo hilo.
“Tunasikia
kwamba mlinzi kala matapishi yake kwa kitendo cha kukanusha taarifa
alizotoa awali kituo cha Polisi. Kama amefanya hivyo, itakuwa kuna
shinikizo amepata hivyo anatafuta njia ya kujiokoa,” alisema.
Kaimu
mganga mkuu wa mkoa, Dk.Ramadhani Kabala, alikiri kuwepo kwa taarifa
hizo na kudai kwa sasa mwili wa marehemu unaendelea kufanyiwa uchunguzi,
ili kutambua kama kweli Rahel alifufuka na kupiga chafya akiwa ndani ya
chumba cha kuhifadhia maiti.
“Ingawa
si rahisi binadamu kufufuka baada ya kufariki dunia, lakini hatuwezi
kuzipuuza taarifa hizi za mlinzi. Ipo timu inaongozwa na daktari bingwa
kutoka wiraza ya mambo ya ndani, Dk.Ahmed Makata inaendelea na uchunguzi
wa kina. Kwa hiyo baada ya kumalizika kwa uchunguzi, tutawaita
waandishi wa habari kuwaeleza ukweli ili muweze kuitaarifu jamii,” alisema Dk.Kabala.
Kwa
upande wake mkuu wa mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe, alikiri
kupokea taarifa hiyo ya aina yake, na kwamba zipo timu mbili zinaendelea
na kuchunguzi ili ukweli uweze kubainika.
Na Nathaniel Limu, Singida
Post a Comment