0

Baada ya wakazi wa Kijiji cha Iringa Mvumi katika  Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma kuwaua watafiti wa Kituo cha Udongo na Maendeleo cha Selian Arusha, wakazi wa kijiji hicho wamehama makazi yao wakihofia kukamatwa na Jeshi la Polisi.
Waandishi wa habari waliofika kijijini hapo jana na walishuhudia hali ya utulivu kijijini hapo tofauti na ilivyozoeleka.

Pamoja na wananchi hao kukimbia makazi yao, taarifa zinasema viongozi wote wa Serikali ya Kijiji hicho  wamekamatwa na polisi wakiwamo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji, Albert Chimanga na Diwani wa Kata ya Iringa Mvumi, Robert Chikole.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Michael Kagisi, alisema kitendo cha wananchi kukimbia kijiji hicho kimesababisha shughuli nyingi za  jamii kusimama   na maduka kufungwa.

Kwa mujibu wa Kagisi, hata wananchi   waliobaki kijijini hapo wakisema    hawakushiriki mauaji hayo, ikifika jioni wanakwenda porini kulala.

“Sehemu kubwa ya watu wameyakimbia makazi yao kwa sababu wanaogopa kukamatwa na polisi, yaani hata shule hazina wanafunzi kwa sababu wengi wamekimbia na wazazi wao.

“Yaani waliouawa waliuawa kwa makosa kwa sababu  kabla ya kuwapiga, walijitetea na kujitambulisha, lakini wananchi hawakutaka kuwasikiliza…   baada ya kuwaua, waliwawekea majani na kuwachoma moto ili wafe haraka,” alisema Kagisi.

Akifafanua, mwananchi huyo alisema siku ya tukio ulikuwapo mkutano kijijini hapo na mwenyekiti wa kijiji alipata taarifa kwamba katika eneo la kutengeneza chumvi, kuna gari ambalo walilitilia shaka kwamba huenda ni majambazi.

“Siku hiyo tulikuwa kwenye mkutano na baadaye tulimuona mwenyekiti akiwaita baadhi ya vijana na kuwaagiza waende eneo la tukio.

“Wale vijana walikwenda huko  walipiga simu kijijini kuwaeleza wananchi, kwamba kuna gari la watu ambao hawaeleweki.

“Taarifa hizo ziliposambaa, wananchi walihamasishana na kuelekea eneo la tukio.

“Walipofika tu, walianza kuwapiga, lakini wale watafiti walijieleza kwamba wao siyo majambazi, huku wakiwaomba wananchi wawapeleke katika ofisi zao za kijiji, lakini wananchi walikataa na kuendelea kuwapiga hadi walipowaua,” alisema.

Naye  Mchungaji wa Kanisa la Biblia kijijini hapo, Donald Nyambuya, alisema kwa sasa maisha kijijini hapo ni ya shida kwa sababu huduma nyingi za  jamii zimefungwa baada ya watu kukimbia makazi yao.

Mwinjilisti wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Jacob Foda, alisema kitendo cha watu kukimbia makazi yao  kimeathiri huduma ya  roho kwa kuwa huwa na kawaida kuwatembelea waumini wake.

Wakati huohuo, simanzi na majonzi, jana, vilitawala wakati wa kuaga miili ya Watafiti wa Kituo cha Utafiti wa Udongo na Maendeleo cha Selian mjini hapa.

Watafiti hao waliuawa juzi na wananchi wa Kijiji cha Iringa Mvumi, wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma kwa kukatwakatwa mapanga na kuchomwa moto.

Miili hiyo iliwasili mjini hapa jana asubuhi kwa gari ikitokea Dodoma na kuingizwa kwenye eneo la wazi la kituo hicho kilichopo pembeni mwa Uwanja mdogo wa Ndege wa Arusha kwa ajili ya wafanyakazi kutoa heshima za mwisho.

Shughuli ya kuaga miili hiyo ilifanyika asubuhi kwa wafanyakazi, jamaa na marafiki kutoa heshima za mwisho bila majeneza kufunguliwa kwa kuwa imeharibika.

Baadaye  ilipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwa ajili ya kufanyiwa maandalizi ya kusafirishwa.

Waliouawa katika tukio hilo  walitambuliwa kuwa ni Jaffari Mafuru aliyesafirishwa jana kwenda Mara kwa mazishi, Theresia Ngume, aliyetarajiwa kuzikwa jana mjini Arusha na dereva wa gari walilokuwamo,       STJ 9570 aina ya Toyota Hilux, mali ya Kituo cha Utafiti cha Selian, Nikas Magazine, aliyesafirishwa kwenda Ifakara, Morogoro kwa mazishi.

Watafiti hao  waliuawa wakiwa katika kazi ya mradi unaoandaa taarifa za hali ya udogo kwa nchi nzima.

Akizungumza baada ya kutoa heshima za mwisho, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Januari Mafuru ambaye ni baba mzazi wa marehemu Jaffari, alisema tukio hilo limemuumiza sana.

Alisema kituo hicho kimekuwa kikiendesha mradi huo kwa lengo la kuwasilisha taarifa hizo kwa wakulima wadogo na wataalamu wa kilimo  ziweze kuwasaidia wananchi katika kilimo na hatimaye kuongeza mazao.

“Mradi huu umemaliza utafiti katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Baada ya hapo kazi nyingine ilikuwa imeanza Kanda ya Kati Dodoma na Singida.

“Wiki iliyopita, tuliandaa watafiti wanane na magari yao manne kwa ajili ya kwenda mkoani Dodoma kukusanya udongo kwa ajili ya kuuleta hapa kwenye maabara za Seliani kufanyiwa utafiti kisha kutoa matokeo yatakayowarudia wakulima,” alisema Mafuru.

Akizungumzia kuwasili kwa watafiti hao katika Kijiji cha Iringa Mvumi, wilayani Chamwino yalikotokea mauaji hayo, Mafuru alisema timu zote zilikuwa na barua za utambulisho pamoja na vifaa vya kazi.

“Timu iliyokuwa Chamwino katika Kijiji cha Iringa Mvumi, iliwakuta wanawake wakiendelea na shughuli za kukusanya chumvi  na watafiti waliwasilimia na kujitambulisha wametokea wapi.

“Taarifa tulizonazo ni kwamba, baada ya kusalimia, watafiti waliacha gari pembeni na kutembelea maeneo   kuchagua udogo.

“Huku nyuma kundi la wale wanawake lilitoa taarifa kwa viongozi wao kuwa wamevamiwa na wanyonya damu, ndipo walipotokea watu wakiwa na mashoka na mapanga na   kuwashambulia kabla ya kuwachoma moto,” alisema.

Mtafiti Mwandamizi wa Kituo cha Selian, Dk. Lameck Makoye, alilaani mauaji hayo na kusema hajawahi kuona wala kusikia watafiti wakivamiwa   wanapokuwa   vijijini.

“Naamini Serikali imeona, binafsi sijawahi kuona tukio la aina hii kwa sababu  watafiti wale walikuwa na vielelezo vyote vinavyowatambulisha.

“Hata mradi waliokwenda kufanya ulikuwa ni kwa faida ya wananchi wa Kijiji cha Iringa Mvumi kwa vile umelenga maeneo ya nchi nzima.

“Sisi Kituo cha Utafiti cha Selian ndiyo tunaoleta maendeleo ya mkulima kwa nchi nzima kwa kufanya utafiti wa udongo unaomwezesha mkulima alime vipi na atumie mbolea kwa kiwango gani na ya aina gani,” alisema Dk. Makoye.

Mume wa marehemu Theresia, Jonas Mjema, akizungumza kwa huzuni kuhusu  kuondokewa na mkewe, alisema kabla ya tukio la mkewe kuchomwa moto, alizungumza naye asubuhi kujua anaendeleaje.

“Niliwasiliana naye asubuhi Jumamosi tukatakiana kazi njema, ilipofika jioni nilimtafuta lakini simu yake haikupatikana.

“Nilijipa matumaini labda mawasiliano hayakuwa mazuri kwa vile shughuli zao ni za porini.

“Ilipofika Jumapili, nilipigiwa simu na shemeji yangu akinipa taarifa za tukio la kuchomwa moto mke wangu,” alisema Mjema aliyeachwa na watoto wawili.

Post a Comment

 
Top