JESHI la Polisi visiwani Zanzibar, limesema litamchukulia hatua
za kinidhamu ofisa wake mwenyewe cheo cha Sajenti ambaye alionekana hivi
karibuni akipokea rushwa kutoka kwa raia wa kigeni.
Hatua hiyo, imekuja baada ya picha za video kusambaa katika mitandao ya
kijamii, zinazomwonyesha askari huyo akipokea fedha ambazo hadi sasa
hazijajulikana kiwango chake kutoka kwa raia huyo wa kigeni, ambaye
alikuwa na kosa la kutofunga mkanda.
Katika video hiyo, raia huyo anaokana kutoa fedha na kumkabidhi askari
huyo huku akiahidi kumsaidia ili asikamatwe mbele ya safari.
Tukio hilo lilitokea eneo la Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ingawa
askari huyo alitaja eneo la Mahonda akionyesha nia ovu ya kutenda kosa
hilo bila kujijua kama anachukuliwa video.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdani Omar Makame alisema jeshi
hilo linampongeza raia huyo wa kigeni kwa kutoa taarifa hiyo.
“Jeshi la polisi linachukua nafasi hii kulaani kosa hili, licha ya kua
ni kosa la jinai linalifedhehesha jeshi na kulitia doa kutokana na
dhamana kubwa lililokabidhiwa,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa taratibu za jeshi hilo, tayari limeanza uchunguzi mara moja na kwamba litachukua hatua zinazostahili.
Kutokana na hali hiyo, Kamishina Hamdani amewataka wamiliki wa makampuni
ya simu za mikononi kufufua mfumo wa upigaji simu kutumia namba za
dharura ambazo ni 111 na 112 ili kuwarahisishia wananchi kutoa taarifa.
Post a Comment