RAIS
wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila amebainisha wazi
kuwa anatamani nchi yake pamoja na ukubwa na utajiri iliyonayo,
ingekuwa na amani na mshikamano kama Tanzania.
Pia
Rais huyo amesisitiza kuwa nchi yake kwa sasa iko tayari kukuza
ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na nchi nyingine ikiwemo Tanzania,
tofauti na zamani ambako ilijikita zaidi katika masuala ya kutafuta
amani. Kabila aliyasema hayo juzi usiku wakati akizungumza kwenye dhifa
ya chakula aliyoandaliwa na mwenyeji wake Rais John Magufuli, Ikulu
jijini Dar es Salaam.
Alisema
anavutiwa na hali halisi ya amani inayoendelea kudumu nchini Tanzania,
ikiwemo jitihada za wananchi na serikali kwa ujumla katika kuitunza na
kuilinda amani hiyo na kuimarisha uchumi.
“Kila
nikipita katika mitaa mbalimbali ya DRC nakumbuka hali halisi ya amani
iliyopo Tanzania. Nikiri tu nimekuwa nikivutiwa sana na hali ya amani na
mshikamano iliyopo hapa Tanzania. DRC ni nchi kubwa na yenye utajiri,
ninaiombea sana nchi yangu na yenyewe ifurahie amani hii,” alisisitiza.
Alisema anatambua kuwa hata nchi iwe kubwa na utajiri vipi, wananchi wake hawawezi kuwa na furaha kama hakuna amani.
“DRC
ni nchi kubwa ina jumla ya makabila na lugha 225 nina imani na sisi
tutaweza kuwa na amani na umoja kama mlionao hapa Tanzania.”
Aidha,
Rais huyo, alisema amefurahi nchi yake kuimarisha ushirikiano wa
kibiashara, kiulinzi na usalama na kindugu na Tanzania na kukiri kuwa
hiyo ni mara yake kwanza kutembelea Tanzania na kuzungumzia zaidi
masuala ya kiuchumi na kibiashara ambapo zamani ziara zake zilijikita
zaidi kujadili masuala ya amani.
Awali,
wakati akizindua jengo la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), pamoja
na kuihakikishia Tanzania kuwa nchi yake imeridhishwa na hali ya
bandari ya Dar es Salaam hivyo itaendelea kupitisha mizigo yake katika
bandari hiyo, pia aliomba ushirikiano wa nchi hizo katika sekta ya anga.
Alisema
anatambua kuwa serikali ya awamu ya tano imenunua ndege mpya mbili na
kwamba imepanga kuanza kufanya safari zake maeneo mbalimbali na
kubainisha kuwa hata DRC nayo imenunua ndege mbili hivyo itakuwa vyema
serikali hizo zikiunganisha nguvu zake pia katika eneo hilo.
Kwa
upande wake, Rais Magufuli, alimshukuru Rais Kabila kwa kukubali kwake
kufanya ziara hiyo ya kibiashara nchini, ikiwa ni pamoja na
kuihakikishia Tanzania kuwa mizigo ya DRC ikiwemo shaba inayozalishwa
nchini humo, itasafirishwa kupitia bandari ya Dar es Salaam.
|
Post a Comment