Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde |
MBUNGE wa
Mtera mkoani Dodoma, Livingstone Lusinde (CCM) amehojiwa na Polisi kwa
madai amekuwa na tabia ya kuwachochea wananchi wake, kujichukulia sheria
mkononi katika mambo wasiyokubaliana nayo, jambo lililosababisha kuuawa
kwa watafiti watatu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Selian Arusha
(SARI) ndani ya jimbo lake.
Pia
imebainika kuwa watafiti hao, ambao waliuawa na wananchi kwa kucharangwa
kwa rangwa kwa mapanga na shoka katika Kijiji cha Iringa Mvumi,
walikuwa na barua ya kuwatambulisha kutoka kwa Halmashauri ya Wilaya ya
Chamwino kwenda kwa mtendaji wa kijiji hicho.
Habari za
uhakika zilizopatikana kutoka ndani ya Polisi Mkoa wa Dodoma,
zilithibitisha kwamba mbunge huyo aliitwa jana kuhojiwa kutokana na
kudaiwa huwa anashiriki kuwachochea wananchi wake, kuchukua sheria
mkononi kwa mambo ambayo hawakubaliani nayo.
“Ni kweli
mbunge tumemwita asubuhi na kumhoji kuhusu taarifa hizo, tunashukuru
ametupa ushirikiano, na kikubwa tulichokuwa tunahitaji kutoka kwake ni
hizi taarifa za yeye kuhamasisha wananchi wake kujichukulia sheria
mkoanoni,” kilisema chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Polisi Dodoma.
Mbunge akanusha kuchochea Lusinde alipoulizwa kuhusu kuhojiwa na polisi
jana alikataa. “Nihojiwe kwa jambo gani? alihoji mbunge huyo.
Hata
hivyo alibanwa kwamba alionekana kituo ha polisi asubuhi na kuulizwa
alienda kufanya nini, alikiri kwamba alienda kituo cha polisi. “Ni kweli
nilienda polisi asubuhi, lakini nilienda pale kuwaona viongozi
wanaoshikiliwa na polisi, maana kuna diwani na mwenyekiti wa kijiji,
hawa ni viongozi wenzangu lazima niwaone, lakini sikwenda kuhojiwa na
polisi,” alisema Lusinde.
Kuhusu
tuhuma za yeye kushiriki kuwachochea wananchi wake, kujichukulia sheria
mkononi kwa mambo wasiyoyakubali, Lusinde alisema tangu uchaguzi mkuu wa
mwaka jana uishe, hajawahi kufanya mkutano wowote kijijini hapo wala
kwenda kushiriki kwenye ibada.
“Tangu
uchaguzi uishe sijawahi kukanyaga kijijini hapo huo uchochezi nimeufanya
saa ngapi? Aliongeza, “Kuna wataalamu wa maji na miradi mingine
wanafika kijijini hapo hawajawahi kupigwa. Mimi ni mbunge nitaanzaje
kuwachochea wananchi wangu? Kwa kweli huo ni uongo na uzushi dhidi
yangu.”
Alitoa
mwito kwa wananchi ambao wamekimbia makazi yao kurudi kijijini na
kushirikiana na vyombo vya dola ili waweze kuwataja walioshiriki kwenye
mauaji hayo.
“Mauaji
yalifanyika mchana, ina maana waliofanya mauaji wanafahamika, wananchi
warudi wawataje bila kuwaonea haya.” Akielezea tukio hilo alisema tukio
la umwagaji damu kwa watu wasio na hatia ni laana, hivyo yeye kama
mbunge anasubiri polisi wakishakamilisha taratibu za upelelezi,
atamwomba Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Kati (DCT), Dk Dikson
Chilongani ili akafanye ibada katika eneo hilo. “Ni lazima tukamlilie
Mungu na kumwomba samahani kwa mauaji haya yaliyofanyika pale,” alisema
mbunge huyo.
Alisema
yeye binafsi hajawahi kusikia kuwepo kwa wanyonya damu katika vijiji vya
jimbo lake. Watafiti walifuata taratibu Akizungumza na gazeti hili
jana, Kaimu Mkurugenzi Utafiti na Maendeleo wa Wizara ya Kilimo, Mifugo
na Uvuvi, Dk Hussein Mansoor alisema watafiti hao walipitia taratibu
zote za kujitambulisha kuanzia mkoani, wilayani na kwa watendaji wa
vijiji na kata.
“Bahati
nzuri hata kwenye gari kulikuwa na nakala ya barua yao ya kuwatambulisha
iliyokuwa imetumwa na halmashauri kwenda kwa watendaji wa vijiji ambako
walitakiwa kwenda kufanya kazi na hata pale walipouawa uongozi wa
kijiji ulikuwa na taarifa,” alisema Dk Mansoor.
Chanzo
cha polisi Dodoma pia kilikiri kuwa eneo la tukio waliokota barua kutoka
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kwenda kwa mtendaji wa kijiji hicho,
kuwatambulisha watafiti hao. “Hawa walifuata taratibu zote, yawezekana
hatua waliyoiruka ni kwenda kujitambulisha ofisi ya kijiji na kupewa
wenyeji wa kuwaongoza kufanya kazi zao, hilo tunahisi hawakulifanya,”
alieleza.
Akifafanua
kuhusu watafiti hao, Dk Mansoor alisema watafiti hao walikuwa wanafanya
kazi chini ya mradi ujulikanao kama Tanzania Soil Information System
(TANSIS) ambao unaendeshwa na Wizara ya Kilimo kwa lengo la kupata
ramani ya udongo nchi nzima ili kuwashauri wakulima kwa kutoa ushauri
sahihi kwa kutumia taarifa za udongo za sasa.
Akielezea
taratibu zinazotumiwa na wizara hiyo pindi watafiti wake wanapoenda
mikoani, Dk Mansoor alisema wanaandika barua kwa mkoa na wilaya husika
kuwatambulisha watafiti hao na kazi watakayoifanya na muda wa siku
watakaokuwepo humo.
“Kwa hili
la Chamwino, wizara tulipeleka barua mkoani na wilayani, na pia taarifa
zilipelekwa na wilaya kwa watendaji wa kata na vijiji ambako walikuwa
wamepangiwa kwenda kufanya kazi. “Huwa tunawashauri wawe na nakala za
barua kwa kile eneo ambako wanaenda, na bahati nzuri nakala ya barua ya
kwenda kwa mtendaji wa kijiji kile ambako waliuawa walikuwa nayo kwenye
gari na ilidondoka katika purukushani zile na polisi wameiokota,”
alisema Dk Mansoor.
Alisema
utafiti waliokuwa wanaufanya watafiti hao ni muhimu kwa mkulima kwani ni
utafiti huo ndio ambao unatoa fursa ya kuwashauri wakulima aina ya
mbolea wanayotakiwa kutumia na kiwango cha mbolea hiyo kutokana na hali
ya udongo. Katibu Tarafa awakana Hata hivyo, Katibu Tarafa ya Makang’wa,
Hanifa Diemerwa alisema wakati tukio linatokea yeye alikuwa likizo
hivyo hana taarifa yoyote.
Hata
hivyo alipoulizwa kama ameshafuatilia kama ofisi za kijiji zilikuwa na
taarifa za ujio wa watafiti hao, alijibu kuwa hakukuwa na barua yoyote
ya kuwatambulisha watafiti hao.
“Mimi
nimejaribu kufuatilia wanasema hakukuwa na barua, hata hivyo kama
walikuwa na hiyo barua, basi walikuwa hawajafika kujitambulisha kwenye
ofisi ya kijiji na kusaini kitabu cha wageni,” alisema Hanifa.
Post a Comment