Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Kibaha.
VIJANA
waishio katika mazingira magumu waliohitimu Chuo cha Elimu na Mafunzo
ya Ufundi Stadi (VETA) Pwani, chini ya Mradi wa kuwawezesha Vijana
Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na Shirika la Plan International wameiomba
Serikali kuwapatia ajira ili waweze kumudu maisha yao.
Hayo
yamesemwa leo wilayani Kibaha na mmoja wa wahitimu wa mradi huo, Rajabu
Kilanga alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hii juu ya mafanikio
na changamoto anazozipata baada ya kuhitimu mafunzo hayo.
Kilanga
amesema kuwa mradi huo umemuwezesha kufahamu jinsi ya kuhifadhi fedha
kwa ajili ya maisha ya baadaye pia umemnufaisha yeye pamoja na familia
yake kwani kupitia fani ya umeme aliyoisomea ameweza kupata tenda ndogo
ndogo ambazo zinamsaidia kuyaendesha maisha yake.
“Pamoja
na faida nyingi nilizozipata kupitia mradi huu lakini ukosefu wa ajira
za kudumu ni moja ya changamoto ambazo zinatukabili vijana tuliohitimu
mafunzo haya hivyo, tunaiomba Serikali itusaidie kutupatia ajira ili na
sisi tuweze kutimiza malengo yetu na kuchangia katika kulijenga Taifa
letu”, alisema Kilanga.
Kilanga
ameishukuru EU na Shirika la Plan International pamoja na wadau wengine
kwa kuratibu mradi huo kwani baada ya vijana wengi kuhitimu na kuweza
kujiajiri na kupata vipato kupitia mafunzo waliyoyapata chini ya mradi
huo wameweza kujikwamua kutoka kwenye hatua moja ya maendeleo kwenda
nyingine.
Naye
muhitimu mwingine kupitia mradi huo, Simba Musa ametoa wito kwa vijana
wenzie kujituma na kufanya kazi kwa bidii kwani kwa kufanya hivyo
wananchi wataona kazi zao hivyo kuwapelekea kupata ajira kwa urahisi.
“Nawashauri
vijana wenzangu tujishughulishe, hata kama Mhe. Rais akitoa fedha
hawezi kukuletea nyumbani kwa hiyo, kila mmoja kwa nafasi yake ajitume
ili watu wazione kazi zake”, alisema Musa.
Aidha,
ameyataja baadhi ya malengo yake yakiwemo ya kufungua duka la vifaa vya
umeme pamoja na kuwafundisha vijana wenzie bila kuwatoza gharama yoyote
ili nao waweze kujipatia kipato kupitia ujuzi watakaoupata.
Kwa
upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Visigo, wilayani Kibaha, Aloisia
Nyelo amesema kuwa mradi huo umewasaidia vijana kutozagaa hovyo mitaani
kwani wameunda vikundi vinavyosimamiwa na watendaji wa Kata hiyo kwa
ajili ya kuwapa ushauri hivyo kuwafanya wawe na adabu na heshima.
Nyelo
ameongeza kuwa Kata hiyo iko mstari wa mbele katika kuwasaidia vijana
kupata tenda mbalimbali kwa kuwabandikia matangazo nje ya ofisi yao na
kuwataka wananchi wanaohitaji wafanyakazi kusaini mkataba na vijana
husika mbele ya Afisa Mtendaji ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa
uhakika na wanalipwa fedha zao kama walivyokubaliana.
Mtendaji
huyo alitumia fursa hiyo kuto rai kwa wananchi kuwaamini na kuwasaidia
vijana hao kwa kuwapa tenda mbalimbali zinazolingana na fani walizosomea
kwani wana ujuzi wa kutosha kufanya kazi hizo katika kiwango
kinachotakiwa.
Mmoja
wa wahitimu wa mafunzo ya ufundi chini ya mradi wa Uwezeshaji wa Vijana
Kiuchumi (YEE) unaofadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya na kuratibiwa na
Shirika la Plan International, Rajabu Kilanga (chini) akimshikilia
kijana mwenzie George Geligoali (juu) wakati wakiendelea na kazi za
kuunganisha umeme kwenye nyumba.
Afisa
Mtendaji wa Kata ya Visigo, wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani Aloisia
Nyelo, akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mchango
wa kata hiyo juu ya kuwasaidia vijana waliosomeshwa chini ya mradi wa
Uwezeshaji wa Vijana Kiuchumi (YEE) kupata ajira.
Post a Comment