|
MWAROBAINI
wa uwepo wa watumishi hewa katika sekta ya umma umepatikana ambapo
kuanzia Oktoba 3, mwaka huu, utambuzi wa watumishi wote wa umma kwa
kutumia mfumo mmoja wa kukusanya na kuhifadhi taarifa, utaanza huku
watumishi wote wa umma, wakitakiwa kupeleka nyaraka muhimu ndani ya wiki
mbili.
Utambuzi
huo, utafanywa na serikali kwa kushirikisha Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa (NIDA) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) huku uhakiki na utambuzi
huo ukiwalenga watumishi wote wa umma walio kwenye wizara, idara za
serikali zinazojitegemea na tawala za mikoa.
Wengine
ni mamlaka za serikali za mitaa, wakala za serikali, taasisi na
mashirika ya umma, ambapo watumishi wote wa umma wametakiwa kupeleka
taarifa zote muhimu zinazowatambulisha katika mamlaka zilizotajwa.
Hayo
yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu usajili wa vitambulisho vya
taifa kwa watumishi wa umma.
Akifafanua
lengo la utambuzi huo, Kairuki alisema lengo ni kuwa na mfumo mmoja wa
taarifa sahihi za watumishi wa umma, ili kuondoa uwepo wa watumishi
hewa, unaoigharimu serikali mabilioni ya fedha, ambazo zingetumika
kufanya kazi nyingine za maendeleo.
“Tulikaa
na NEC na NIDA, na tukaona tunaweza kuboresha mfumo wetu wa taarifa na
tukaona tuchukue ile kanzi data ya NEC na tumeiingiza kwenye mfumo wa
NIDA na kuangalia taarifa za watumishi wetu wa umma, na sasa tuna alama
zao za vidole, tunahakikisha tuna taarifa zao sahihi hadi anuani yake,”
alisema Kairuki.
Alisema
kupitia mfumo huo wa utambuzi, watumishi wote wa umma wanaopaswa
kupeleka taarifa zote muhimu kama vile hati ya malipo ya mshahara, cheti
cha kuzaliwa, vyeti vya kitaaluma, kitambulisho cha kazi, kitambulisho
cha Mzanzibari mkaazi, hati ya kusafiria na kadi ya mpiga kura.
Kufuatia
uhakiki huo, Kairuki alizitaka ofisi zote na taasisi za serikali
zilizobainishwa kuwasiliana na NIDA ili kupanga mpango kazi wa kufanya
shughuli hiyo na kuandaa ratiba itakayowawezesha watumishi wa umma
kufanya usajili bila kuathiri utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha,
ofisi na taasisi hizo zimetakiwa kuandaa mazingira wezeshi ya
kufanikisha kazi hiyo kwa kuandaa ofisi mahususi zitakazotumika
kuendesha kazi hiyo na kuteua Ofisa Mwandamizi atakayeshirikiana na
maofisa kutoka NIDA, na Ofisi ya Rais Utumishi katika kutekeleza hayo.
Pia
taasisi na ofisi hizo zimetakiwa kuainisha magari na madereva kwa ajili
ya kufanya kazi hiyo kwenye mamlaka ya serikali za mitaa na kwamba kwa
ofisi ambazo makao makuu yake yako mkoani Dar es Salaam, watumishi wake
watasajiliwa katika ofisi hizo.
Waziri
Kairuki alisema kwa watumishi ambao wako katika ofisi za matawi mikoani
watafanya usajili katika vituo vya usajili kwenye halmashauri zilizopo
ofisi husika.
Akizungumzia
hatua zitakazochukuliwa kwa watumishi watakaokaidi agizo hilo ndani ya
muda uliopangwa, Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma , Dk Lauren
Ndumbaro alisema hilo ni kosa na adhabu zake zimeainishwa kwenye kanuni
za utumishi wa umma.
“Kwa wale
watakaokaidi kutekeleza agizo hilo ndani ya muda uliowekwa, wanafahamu
kwamba ni kosa kisheria na wanaweza kujifukuzisha kazi wenyewe,” alisema
Dk Ndumbaro.
Hata
hivyo alisema kabla ya hatua hizo hazijachukuliwa nafasi ya utetezi
itatolewa kwa watumishi walioshindwa kutekeleza ndani ya muda
uliopangwa, ili kubaini wenye sababu za msingi na kwa wale wasio na
sababu za msingi, sheria itachukua mkondo wake.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mifumo ya Tehama wa NIDA, Muhammed
Hamis, alisema baada ya usajili huo kufanywa kwa watumishi wa umma
watapewa vitambulisho vyenye saini, tofauti na vile vya awali ambavyo
havikuwa na saini.
“Lakini
tumeanza kusajili Septemba 14, mwaka huu kwa wale ambao hawakuwa na
vitambulisho vya taifa, ila waliokuwa navyo ila havina saini watapewa
baada ya wale ambao hawakuwa navyo kabisa kupata,” alisema Hamis.
Katika
hatua nyingine, Waziri Kairuki alisema serikali itachukua hatua kwa
watumishi hewa waliobainika katika Mamlaka ya Usimazi wa Bandari (TPA),
ambao wameambiwa na mwajiri kuacha kazi wenyewe. “Nimesikia taarifa
hiyo, ila sisi serikali hatuwezi kuliacha, ni lazima hatua zichukuliwe,”
alisema Waziri Kairuki.
Post a Comment