0

WIZARA ya Maliasili na Utalii imeridhia maombi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kubadili mfumo wa utendaji kazi kutoka wa kiraia na kuwa wa jeshi usu ili kukabiliana na tatizo sugu la ujangili wa wanyamapori, misitu na rasilimali nyingine za nchi.

Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya askari na wahifadhi wa shirika hilo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema maombi ya shirika hilo la kutaka kuendeshwa kwa sheria za kijeshi ni ya msingi katika kipindi hiki ambacho nchi inakabiliwa na tatizo sugu la ujangili wa wanyamapori.

Ufungaji wa mafunzo hayo ulifanyika jana katika Kambi ya Mlele ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi mkoani Katavi ambako mameneja wahifadhi 10 na askari 58 walihitimu mafunzo ya kijeshi ya mwezi mmoja.

Alisema taasisi zote za kiuhifadhi kwa wakati huu ziko katika mchakato wa kuingia katika mfumo wa Jeshi Usu kwa lengo la kuboresha utendaji wa kazi wa kila siku, lakini pia niwajulishe wazi kuwa mfumo tunaoingia umeelekezwa vizuri kwenye Sheria ya Uhifadhi wa Wanyama Namba 5 ya Mwaka 2009 kifungu cha 10 hadi 13.

Aliwataka askari hao pamoja na menejimenti ya Tanapa kufanya maandalizi ya kutosha kwa msingi kuwa sheria itakapopitishwa baadhi ya mambo yatabadilika na kuendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kijeshi kwa ilivyo katika majeshi mengine nchini.

Awali akiwasilisha maombi hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi alisema shirika hilo baada ya kutafakari kwa kina, walibaini umuhimu wa askari wao kutumia sheria za kijeshi kutokana na changamoto katika masuala ya uhifadhi.

Meneja wa Pori la Akiba la Rukwa/Lwafi, Joseph Mwang’ombe alisema kuwa kambi hiyo ya mafunzo inakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo uwanja wa ndege kutokarabatiwa kwa wakati, uchakavu wa majengo na miundombinu ya maji na gharama kubwa ya uendeshaji.

Post a Comment

 
Top