TUMECHOKA kuvumilia! Ni kauli ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kudai kusakamwa na Serikali .
Chama
hicho kimetoa kauli hiyo leo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam, baada ya Jaji Mstaafu, Salome Kaganda ambaye ni Kamishna wa
Maadili na Mtendaji Mkuu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
kuwaandikia barua viongozi wa chama hicho akiwatuhumu “kukiuka
masharti ya Hati ya Ahadi ya Uadilifu wa Viongozi wa Umma.”
Jaji
Kaganda aliwaandikia barua viongozi hao tarehe 4 mwezi huu ambapo
Chadema wameitaka sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kuacha
vitisho kwa viongozi wa chama hicho.
Walioandikiwa barua hiyo ni Freeman Mbowe Mwenyekiti wa Chadema na Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho.
Vincent
Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema amesema, kwa mujibu wa barua ya Jaji
Kaganda, katika tarehe, muda na siku ambayo haijulikani, viongozi hao
wa Chadema walitoa matamshi ambayo yanachochea wananchi kutotii sheria,
kufanya vurugu, kudharau misingi ya demokrasia iliyopo nchini na
kutishia usalama wa nchi.
“Hata
hivyo, Jaji Kaganda hakuyataja matamshi hayo wala kuyafafanua. Aidha,
alidai kwamba matamshi hayo yanatokana na maazimio yaliyofikiwa na
kikundi cha watu wachache nje ya Bunge,” amesema Dk. Mashinji.
Licha
ya kudai kwamba, maazimio ya kikundi hicho yanapuuza utangamano,
utulivu na usalama wa wananchi wengine kinyume na dhana ya maslahi
mapana ya umma, Jaji Kaganda hakukitaja kikundi hicho cha watu wachache
nje ya bunge huku pia akidai matamshi ya viongozi hao yalilenga
‘kushamirisha ‘ maslahi yao binafsi na maslahi ya Chadema.
“Mheshimiwa
Mbowe ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama kikuu cha upinzani hapa nchini.
Ni kiongozi wa chama ambacho mgombea urais wake alipata zaidi ya kura
milioni sita kati ya kura 15 milioni zilizopigwa kwenye uchaguzi mkuu wa
urais mwaka jana.
“Ni
mbunge wa kuchaguliwa na kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Katika
Bunge. Ni mtu na kiongozi anayejulikana na kuheshimika ndani na nje ya
Tanzania. Kusema kuwa kiongozi huyo anaongoza kikundi cha watu wachache
nje ya Bunge kwenyewe ni kuonesha maadili yenye mashaka kwa mwandishi
wa barua hiyo,” amesema Dk. Mashinji.
Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki ameeleza kushangazwa na barua ya Jaji Kaganda akisema;
“Ni
vigumu kuamini kwamba, barua hii imeandikwa na mwanasheria na mtu
ambaye amewahi kushikilia madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
“Barua ambayo haina maelezo yoyote ya kile kinachodaiwa kuwa kosa; haitaji tarehe, siku, muda au mahali kosa hilo lilipotendeka.
“Haitaji
vifungu vya sheria yoyote iliyokiukwa na wala kuonyesha kama
sekretarieti ya maadili ya Viongozi wa Umma ina mamlaka kisheria ya
kushughulikia kosa hilo, in onyesha mapungufu makubwa ya kitaaluma na
kiuandishi ya kamishna wa maadili na katika mazingira ya kawaida,
ingestahili kupuuzwa,” amesema Lissu.
Kwa
mujibu wa Lissu ambaye ni mwanasheria wa chama hicho, Chadema haiwezi
kuipuuza barua hiyo na kwamba, inaashiria kuwepo kwa njama za
kuwafungulia mashtaka katika Mahakama ya Maadili Viongozi hao ambao ni
wabunge kwa lengo la kuwavua ubunge.
Aidha,
mojawapo ya vigezo vya kikatiba vya mtu kukosa sifa ya kuwa mbunge ni
pamoja na kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo kwa kosa
linaloambatana na utovu wa uaminifu au kwa kuvunja sheria ya maadili ya
viongozi wa umma.
Kwa
mujibu wa sheria hiyo, kamishna wa maadili ana mamlaka ya kuchunguza
tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma na kuunda mahakama
(Tribunal) ya kusikiliza tuhuma hizo na kupeleka taarifa ya mashauri
hayo kwa kamishna ambaye atapaswa kuwasilisha nakala za taarifa hiyo kwa
rais na spika wa Bunge.
“Rais Magufuli na washauri wake wanafahamu ugumu wa kutumia mahakama za kawaida kwa lengo la kukandamiza wapinzani.
“Licha
ya matatizo yake mengi, Mahakama ya Tanzania imedhihirisha mara nyingi
uwezo wa kulinda uhuru wake na kutokuwa tayari kutumika kwa malengo ya
kisiasa ya watawala.
“Sasa
Magufuli (Rais John Magufuli) na washauri wake wanaandaa mazingira ya
kuitisha Mahakama ya Kangaroo watakayoidhibiti wao ili kuhakikisha
wanawakandamiza viongozi wakuu wa chama chetu.
“Kama
ambavyo tumethibitisha mara kwa mara chama chetu hakitakuwa tayari
kuona viongozi wake wakikandamizwa kwa kutumia kivuli cha maadili ya
viongozi wa umma. Tutapambana na njama hizo. Kwa uthabiti na kwa weledi
ule ule ambao tumepambana na njama nyingine za aina hiyo katika siku za
nyuma,” ameeleza Lissu.
Aidha
Jaji Kaganda amenukuliwa na gazeti la Mwananchi la leo akikana kujua
kuhusu barua hiyo huku akisema “mimi sifahamu kuhusu suala hilo, sina
taarifa.”
Post a Comment