Mojawapo ya tatizo linalowakwamisha watu wengi kufanikisha malengo na
mipango yao kila mwaka, ni kwa sababu bado wanaona wanao muda mwingi wa
kufanya hivyo huku wakijitia moyo pengine watafanikisha mambo hayo
kwani wana nafasi ya kutosha wa kufanya hivyo. Hili ni tatizo kwa watu
wengi na haliwezi kuondoka kwa muhusika kama mtu mwenyewe hatokuwa
tayari kubadilika na kuamua kubadilisha mwelekeo wa maisha yake
anayoyataka mapema zaidi.
Leo hii nataka nikushauri juu ya jambo hili na uamue kubadilika na
kufanya uamuzi wa kutimiza malengo na mipango yako uliyokuwa umejiwekea
ndani ya mwaka huu. Ushauri wangu kwako ndani ya miezi hii iliyobaki
kumaliza mwaka huu ni kuwa, Anza kutumia “kanuni ya kuruka kama chura na si kutembea tena kama kinyonga.”
Kwa nini? Unaweza kuona bado una siku nyingi na muda mrefu wa kutimiza
malengo na mipango yako yote uliyojiwekea mwaka huu, ila nataka
nikuambie si kweli kabisa kama unavyofikiri kwani tumebakiza miezi minne
mbele yetu ukitoa huu mwezi wa nane ili tumalize tena mwaka 2016.
Usikubali kuishi kwa kujitia moyo na matumaini kwamba unazo siku
nyingi za kutimiza malengo na mipango yako yote uliyopanga kuifanikisha
ndani ya mwaka huu, huku bado unacheza na muda ulionao; umebaki kusema
kusema utafanya kesho, unaamua kughairi kutimiza wajibu wako kila siku
kwa visingizio visivyo na maana yoyote. Nataka kukuambia haikupasi
kufanya hivyo kama unahitaji kweli mafanikio makubwa juu ya ndoto yako.
Acha tabia ya kughairisha mambo mazuri unayopanga kufanya kila mwaka na
badala yake amua leo kuanza kuyachukulia hatua kama ulivyokuwa
umejipangia kabla ya mwaka huu kuisha.
Unahitaji kukimbia, unahitaji kuongeza spidi, unahitaji kufanya mambo
kwa uharaka na tena kwa ufanisi zaidi, ili kuziba nafasi na mwanya wa
muda ulioupoteza na kuhakikisha unafanikisha hata nusu au asilimia 50%
au 70% ya malengo yako yote uliyojiwekea kufanikisha mwaka huu.
Usikubali kumaliza mwaka na asilimia ndogo ya malengo uliyoyafanikisha.
Amua kutimiza malengo yako leo hii na ukubali kuishi pasipo kughairi
tena ili uweze kuvuka kiwango kingine ifikapo mwisho wa mwaka huu.
Hebu jiulize maswali haya yafuatayo:
Ni nini ulichokuwa umekipanga kipindi mwaka huu unaanza ambacho hadi sasa hujakitimiza?
Ni malengo gani ya kifamilia, biashara, kikazi, mahusiano, fedha na
uwekezaji, nakadhalika, katika hayo ulikuwa umejiwekea ili kuyatimiza
kabla ya mwaka huu kuisha na hadi sasa hata nusu yake hujafanya kama
ulivyopanga. Umebaki kusema nitafanya kesho, wakati mwingine umekuwa
ukikifanya kitu hicho lakini kwa “mkono mlegevu au kwa mwendo wa kinyonga.”
Nataka nikuambie kuwa, tambua wakati haukusubiri, na wakati ndio huu
unayoyoma na kamwe wakati huu hautorudi tena. Kila mwaka umebeba mission
yake, hujatimiza mission ya mwaka huu unataka kwenda wapi!
Yawezekana malengo mengine uliyojiwekea ulisema utayatimiza kabla ya
mwezi wa sita kuvuka, lakini mwezi wa sita umepita na sasa umegeuza
unasema kabla mwezi wa kumi na mbili; na ukivuka wa kumi na mbili
utasema tena kabla ya mwezi wa sita. Mwaka hadi mwaka unatembea na
malengo yale yale uliyotoka nayo mwaka mwingine, kwa lugha nyingine
unaishi 2017 lakini moyo wako umeuacha au upo 2016. Hujakamilisha
misheni ya 2016 unakimbilia kuingia 2017 hatimaye miaka nenda miaka rudi
unalalamika maisha magumu haupigi hatua upo pale pale. Badilika rafiki.
Hebu jiulize ile biashara uliyosema utaanzisha, umeanzisha?
Hebu jiulize mtu uliyesema utaunga ushirika naye (connection), Je, hadi sasa umefanya hivyo?
Hebu jiulize ile kozi fupi uliyosema utachukua kabla ya mwaka huu kuisha, Je, hadi sasa umefanya hivyo?
Je, ulisema utapatana na ndugu yako kabla ya mwaka huu kuisha, mbona
hadi sasa hujatimiza jambo hili hadi mwaka huu unakimbilia tena
mwishoni?
Unakaa na kinyongo moyoni mwako mwaka mzima halafu unategemea
mafanikio ya kiwango kikubwa, haiwezekani! Sahau katika hilo. Unapaswa
kujifunza kusamehe na kusahau watu wanaokukosea ili kujisaidia wewe
mwenyewe binafsi na si kumsaidia tu mtu husika uliyekosana naye.
Kusamehe ni hatua nzuri ya kujiweka katika nafasi ya kusababisha
mafanikio yachipue katika maisha yako. Jifunze kusamehe na kusahau watu
wanaokukosea kila siku.
Hebu jiulize ulisema utasoma vitabu 50 ndani ya mwaka huu, mbona hata kitabu cha 5 hujamaliza?
Angalia ni wapi unakosea rafiki. Badilika. Hauwezi kuvuka kiwango
kingine cha maisha kama bado unangangania kiwango kimoja cha ufahamu
ulionao, inakupasa kubadili mwelekeo wa maisha yako kwa kukubali
kujifunza kila siku iitwapo leo ili kuongeza kiwango na hatua mpya
katika maisha yako.
Ulisema mwaka huu hautoisha utakuwa umeanza kutumia kipaji chako. Je,
umefanya jambo hili? mbona unakwepa jambo hili kila unapoulizwa?
Kila siku unasema nitaanza kuimba, nitaanza kuandika kitabu changu,
nitaanza kutumia kipaji changu cha uchoraji ili nifikie viwango vya
kimataifa, nitaanza kufundisha, nitaanza kutengeneza video zangu za
kuhamasisha watu kuishi ndoto zao, nitaanza kutoa elimu ya ujasiriamali
kwa watu, nakadhalika. Neno “nitaanza” limekuwa kama wimbo wa taifa
kwenye maisha yako. Leo nakutaka ubadili wimbo huo na uanze kuimba wimbo
mpya wa “ninafanya leo.” Na amua kufanya leo hii jambo hilo
ulilolisema, usisubiri ufanye kesho bali amua kufanya muda huu na si
kesho au mwakani, bali ni sasa.
Nataka nikuambie unayo nafasi hadi sasa ya kugeuza matokeo mabaya juu
ya maisha yako na kuleta matokeo chanya dhidi ya malengo na mipango
yako uliyojiwekea ndani ya mwaka huu, hasa kama ukiamua kubadilika na
“kuongeza spidi na kasi” ya kutimiza mipango yako yote uliyojiwekea
ndani ya mwaka huu. Amua kuruka kama chura na amua kutokupoteza muda
tena kwenye mambo yasiyo na msingi wowote juu ya ndoto yako, na kubali
kuishi kwa kuzingatia faida ya maisha yako ya badae. Usikubali kubaki
nyuma kila mwaka na kutembelea kiwango kimoja hadi miezi na tarehe zote
za kila mwaka zimeshakuzoea. Badilika!
Amua leo kuruka kama chura na si kutembea tena kama kinyonga.
JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO.
Post a Comment