0

Mbunge wa jimbo la Liwale mh. Zuberi Kuchauka akijumuika kula chakula cha pamoja na watu wenye ulemavu siku ya EID julai 6 wilayani Liwale Mkoani Lindi.

 WATU wenye Ulemavu wilayani hapa wamemuomba Mbunge wao Zubeir Kuchauka awasaidie kupata mahitaji yao muhimu ikiwa ni pamoja na elimu,afya  na kuwatafutia ofisi ya kukutania.

Walemavu hao ambao julai 6 (juzi)  walikula chakula cha mchana nyumbani kwa Mbunge walilalamikia utaratibu wa kupata huduma za afya katika vituo mbalimbali ikiwa ni pamoja na hospitali ya wilaya .

Mlemavu wa kutoona  aliyejitambulisha Shabani Kiongozi alisema wamekuwa wakipata tabu sana wakati wanapoenda hospitali kupata matibabu hawaridhishwi na utaratibu wao na kwamba hawana fedha za kulipia matibabu hayo kwa kuwa hawana pia vyanzo vya kupata fedha.

Kutokana na hali hiyo  walimuomba mbunge wao awasaidie ili waweze kupata huduma stahiki kama serikali ilivyoagiza kwao kupata huduma za matibabu bure.

Naye Mwanahawa Mnyomole alimweleza mbunge huyo kuwa hawana hata utaratibu wa kutambulika hasa  pale   watoto wao wanapofikia umri   wa kwenda shule wasaidiwe kupata nafasi hiyo.

Pia alisema wanashindwa kutembeleana wao kwa wao kwa kuwa hawana ofisi ya utambulisho hivyo wapate ofisi ili waweze kuwa wanakutana kama ilivyo kwa vyama vyao vilivyopo Dar es Salaam,alilolitaja kuwa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu (Shivyawata).

Mwenye Ulemavu wa ngozi 'Albino' Ahmad Nganjikatila alimuomba mbunge huyo kuwasaidia ili wapate mitaji itakayowawezesha kufanya biashara na kupata  maendeleo yao kuliko kuomba omba
Alisema kuwa mlemavu sio sababu ya wao kuwa omba omba hivyo waweze kusaidiwa wajishughulishe katika kujitafutia ridhiki ya kila siku.

Naye Shaibu Jika alisema watu wenye Ulemavu wana haki kama watu wengine kiuchumi  kisiasa na hata kijamii hivyo Mbunge awasaidie kupata wafadhili wapate mitaji ya kuendesha maisha yao.

Alisema hawajawahi Kula na viongozi na kuzungumza nao na hiyo ndio mara Kwanza kwao hivyo utaratibu huo uendelee kwani wanafarijika sana.

Akijibu maombi yao Kuchauka alisema amepokea na kwamba atajadili na viongozi wenzake kwenye vikao vya halmashauri.

Alisema ataanza na kutafuta ofisi ili waweze kuwa wanakutana na kuzungumza na kupanga mambo yao ya maendeleo.

Alisema ni vyema wakawa katika umoja unaotambulika na si kumsaidia mmoja mmoja ili hata kama kuna shida iwe rahisi kuwafikia.

 "Kuna miradi mingi mnaweza kuifanya mkiwezeshwa ikiwa ni pamoja na ushonaji,ufugaji kuku,na biashara nyingine ndogo ndogo,"alisema Kuchauka.

Aliongeza kuwa kuna umuhimu wa kupata takwimu zao kujua wako wangapi wilaya nzima ili iwe rahisi kuwasaidia pia.

Walioomba baiskeli Mbunge pia alitaka kupata idadi yao ili aweze kuwasaidia kwa kuanza na baiskeli chache.

Post a Comment

 
Top