KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm,
amesema hatakuwa na msamaha kwa wachezaji ambao watashindwa kuripoti
mapema kambini kujiandaa na michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka
Afrika (CAF CC) hatua ya makundi.
Kikosi cha Yanga juzi kilianza mazoezi
kikiwa na wachezaji wachache wa kikosi cha kwanza wakichanganyika na
wale wa timu ya vijana kwenye Uwanja wa Chuo cha Maofisa wa Polisi,
Kurasini Dar es Salaam.
Pluijm alisema atakuwa mkali kwa wachezaji wote watakaochelewa kuripoti
kambini pasipokuwa na sababu za msingi. “Tunaanzia ugenini na timu
ambayo hatuijui sana, hivyo ni lazima kufanya maandalizi ya kutosha ili
tukaweze kupambana, hatutaki kwenda kuwa wasindikizaji bali kutafuta
taji ambalo ndiyo jambo la msingi kwangu,” alisema Pluijm.
Kocha huyo alisema haoni sababu ya
mchezaji yeyote kuchelewa kambini kwani hata yeye amelazimika kukatisha
mapumziko yake Ghana anakoishi na kurudi Tanzania kuiandaa timu yake ili
iweze kufanya vizuri.
Alisema ana uhakika hadi leo wachezaji
wote watakuwa wamekamilika na kuanza programu maalumu kwa ajili ya
michuano inayowakabili mbele yao. Yanga imepangwa Kundi A katika
michuano hiyo na TP Mazembe ya DRC, Mo Bejaia ya Algeria na Modeama ya
Ghana na itaanza ugenini nchini Algeria wiki ijayo. Kwa upande wa Kundi B
zipo timu za Kawkab Athletic, Fath Union Sports zote za Morocco, Etoile
du Sahel ya Tunisia na Ahly Tripoli ya Libya.
Post a Comment