0

Shirikisho la soka barani Afrika CAF, limetangaza kuiondoa nje ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika, klabu ya Entente Setif ya nchini Algeria, kufuatia ghasia zilizoonyeshwa na mashabiki wake wakati wa mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini.

CAF, wamefuatilia mkasa huo na kujiridhisha kulikuwa na ghasia za makusudi zilizofanywa na mashabiki wa klabu ya Entente Setif, kwa kurusha vitu vyenye ncha kali, chupa za maji pamoja na miale ya moto katika sehemu ya kuchezea.

Kitendo hicho kilimlazimu mwamuzi kusimamisha mchezo kwa muda, kwa kuzingatia hali ya usalama kwa wachezaji, maafisa wa klabu zote mbili pamoja na mashabiki wengine ambao walikuwa katika hali ya utulivu.

Hata hivyo maamuzi hayo yanaipokonya ushindi wa mabao mawili na pointi tatu klabu ya Mamelodi Sundowns ambayo ilijitutumua na kufanikiwa kuibuka na ushindi katika uwanja wa ugenini.

Bado klabu ya Entente Setif ina nafasi ya kukata rufaa ya kupinga maamuzi yaliyochukuliwa na CAF dhidi yao

Post a Comment

 
Top