0


Kamishna wa oparesheni na mafunzo wa Jeshi la Polisi, CP Nsato Marijani  
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limekanusha taarifa kuwa linakipendelea chama tawala cha CCM, bali limesema  litaendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha luninga cha  TBC usiku huu, Kamishna wa oparesheni na mafunzo wa Jeshi hilo, CP Nsato Marijani amesema Polisi ni taasisi inayofanya kazi kwa mujibu wa sheria bila kushinikizwa na mtu, watu au taasisi yoyote ile.

Amesema taarifa mbalimbali zimekuwa zikienezwa na watu wasio na uelewa kuhusu kazi za jeshi hilo kinyume na hali iliyopo.

“Polisi hatuko juu ya sheria na hata tunapofanya kazi tunakuwa makini ili kuepuka kukiuka miiko ya kazi yetu,” amesema.

Amesema jeshi hilo linaweza kushtakiwa Mahakamani kama litakuwa limetenda  kinyume cha Sheria.

“Kazi yetu ni kuhakikisha tunawalinda raia na mali zao, na hatuwezi kwenda kinyume na hapo.”

Amesema polisi hawezi kuua watu au kuwanyanyasa eti kwa lengo la kukipendelea chama tawala.

Amesema kile kinacho endelea katika Kisiwa cha Pemba, Zanzibar  kwa sasa, hakiwezi kufumbiwa macho na jeshi hilo kwani kinaashiria uvunjifu wa amani.

Kamishna Marijani amesema:

“Polisi hawawezi kukaa kimya pale wanapobaini mali za raia zinaharibiwa na kundi la watu fulani kwa makusudi, hiyo ni hujuma, lazima tufanye kazi ya kulinda mali hizo kama kanuni yetu inavyotutaka, kulinda usalama wa raia na mali zao.”

Post a Comment

 
Top