Dar es Salaam. Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeiry bin Ally amewataka Watanzania halali ili kujipatia ridhiki.
Amesema Mwenyezi Mungu ameagiza waja wake kujitafutia ridhiki ambayo inayotokana na kazi halali hivyo kuwataka viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kuwasisitiza hilo waumini na wafuasi wao.
Mufti ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua semina elekezi inayofanyika jijini hapa kwa siku mbili mfululizo na kueleza kuwa hata: “Hapa kazi tu ni uislam.”
Amesema jitihada inayofanywa na Rais John Magufuli ni kuwataka Watanzania wajitambue na kuwataka viongozi hao na wengineo, kwa kutumia nafasi zao, kumsaidia.
Ameeleza kuwa wananchi na hasa vijana wanapaswa kufahamu umuhimu wa ustahimilivu, uvumilivu na uzalendo. Amesema vijana waelekezwe jinsi ya kuepuka na kuachana na dawa za kulevya ili waipende nchi yao na kujihami dhidi ya adui yeyote atakayejitokeza.
Amewataka viongozi hao kuzibainisha changamoto zinazolikabili baraza hilo, kuzijadili na kuzipatia majibu ili kujiimarisha kwa manufaa ya waislam na Watanzania kwa ujumla. Amesema ni vyema watu wakajiepusha na viashiria vya uvunjifu wa amani.
Semina hiyo ya aina yake imewakutanisha masheikh wa mikoa, makatibu wa mabaraza, wenyeviti wa Bakwata kutoka halmashauri, jumuiya ya wanawake wa kiislamu (Juwakita) na vijana.
Ikiwa inafanyika kwa mara ya kwanza na kuwahusisha wanawake, Mwenyekiti wa Juwakita, Shamim Khan amesema Bakwata imetoa heshima kubwa kwao na imeonyesha kuwa jumuiya hiyo itaimarishwa na kila muislamu bila kujali jinsia au dhehebu.
Amesema semina hiyo ambayo imewakutanisha wasilam wa madhehebu tofauti inatoa fursa kwao kushikamana zaidi ikiwa ni fursaya kupanga masuala yao mbalimbali.
Vilevile alipongeza utumbuaji wa majipu unaofanywa na Rais Magufuli na kueleza kuwa hatua ya kuwapa washukiwa nafasi ya kujitetea ni nzuri kwa kuwa serikali kupitia vyanzo vyake inazo taarifa za kutosha.
Amesema wote waliotumbuliwa na kashfa zao zikatajwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wanapaswa kujieleza ili kuuthibitishia umma ni kwa namna gani “hawahusiki na kilichobainishwa.”
Post a Comment