|
MDHIBITI
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) leo anawasilisha bungeni
ripoti ya mwisho ya ukaguzi wa hesabu za serikali ya mwaka 2014/15.
Ingawa haijajulikana rasmi nini kilichomo ndani yake, baadhi ya watu
waliohojiwa wanatarajia CAG kubaini mchwa wanaotafuna fedha za umma na
namna ya kukabiliana nao.
Aidha
wengine wanatarajia taarifa ya hali bora zaidi ya usimamizi wa fedha za
umma kuliko kipindi cha nyuma. Ripoti hiyo awali ilikuwa imepangwa
kuwasilishwa bungeni mwishoni mwa wiki (Aprili 22) kabla ya kuahirishwa
hadi leo.
“Ni kweli
CAG atawasilisha ripoti kesho (leo) bungeni, ”Naibu Katibu wa Bunge na
Utawala, Joel Joel aliithibitishia HabariLeo juu ya kuwasilishwa kwa
ripoti hiyo leo. Miongoni mwa wabunge waliozungumza na mwandishi wa
habari hizi, wamesema wanatarajia CAG kuonesha mambo mazuri kwa maana ya
taasisi zilizofanya vizuri katika usimamizi wa fedha za umma lakini pia
mambo mabaya.
“Lazima
ripoti itaibua madudu maana walizoea (watendaji serikali) kana kwamba
hapakuwapo na serikali,” alisema Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy
na kusisitiza kuwa pamoja na wabunge wenzake, watamsaidia Rais John
Magufuli kupambana na ubadhirifu serikalini.
Keisy
alisema akiwa mbunge, anaamini pamoja na wenzake, wanachosubiri ni kuona
ripoti hiyo na kuhakikisha wanaohusika na kuchezea fedha za serikali,
kabla ya kufikishwa mahakamani, wanarudisha fedha hizo. “Atakachosema
CAG sisi tutakuwa tayari kusimama kusaidia Rais aendelee kupambana na
ubadhirifu,” alisema.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Mbinga Vijijini, Martin Msuha, alisema ripoti
hiyo ni muhimu katika usimamizi wa serikali na inategemewa kuwa na mambo
mazuri na mabaya kwa maana ya majipu ambayo yatapaswa kutumbuliwa.
Mbunge wa
Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza alisema matarajio waliyo nayo ni
kwamba ubadhirifu na wizi utakaoibuliwa na ripoti hiyo utashughulikiwa
mara moja. “Kama kuna ubadhirifu, mishahara hewa na wizi vyote
vishughulikiwe...kama kuna ubadhirifu na wizi wowote, mwizi mahali pake
ni jela,” alisema Rweikiza akishutumu uwapo wafanyakazi hewa katika
halmashauri yake.
Post a Comment