*Aibukia
kitengo cha mita za kupimia mafuta Kurasini
*Akuta
mafundi wakizitengeneza, akuta zimejaa kutu
*Ataka
barua ya maelezo ifikapo saa 11 leo jioni
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara ya
ghafla kwenye kitengo cha upimaji mafuta bandarini (Oil Flow Metres) na kukuta
zimejaa kutu baada ya kutelekezwa kwa miaka zaidi ya mitano. Pia alitembelea
mita za kupimia mafuta zinazoendelea kujengwa Kigamboni.
Aidha, Waziri Mkuu amempa saa nne tu Mtendaji Mkuu
wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa aandike barua ya
kujieleza ni kwa nini aliamua kufunga mita hizo zisitumike kwa zaidi ya miaka
mitano iliyopita na amletee barua hiyo ofisini kwake ifikapo saa 11 leo jioni.
“Nataka unieleze ni kwa nini ulitoa maelekezo ya
kufunga mita hizo, na kwa nini jana uliamua kubadili uamuzi huo? Ni kwa nini
umeamua kuchukua maamuzi haya baada ya kupokea ujumbe wa simu ya mkononi (sms)
wakati mita zimekaa bila kufanya kazi kwa miaka mitano? Ni kwa nini umeamua
kufanyia kazi ujumbe wa sms wakati unajua Serikali inafanya kazi kwa maandishi
rasmi?” alisema Waziri Mkuu.
“Umesema mlikuwa mnatumia utaratibu wa kupima kwa
kijiti. Huu hauna uhakika na huwezi kutegemea taarifa ya mtu mwingine au
kuingia kwenye meli ya mtu na kuanza kuchukua vipimo hadi ujiridhishe. Nataka
kujua ni kwa nini mlikuwa na utaratibu wa ku-bypass mafuta ili yasipite kwenye
mita za kupimia mafuta? Ni kwa nini umetoa amri zianze kutengenezwa jana na
siyo mwaka 2012 au 2013?” alihoji Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alisema mita hizo za Kurasini
zilinunuliwa na Serikali kwa gharama za dola za marekani milioni 1.2 (wakati
huo) na haiwezekani kuacha kuzitumia wakati watu wanachezea mifumo na kuongeza
mianya ya kupoteza mapato kwa Serikali. Ameagiza mita hizo zianze kufanya kazi
mara moja.
Wazir Mkuu alisema matumizi ya mita hizo
yaliafikiwa na Serikali baada ya kubaini upotevu mkubwa wa kodi kwenye mafuta
yanayoingizwa nchini na baada ya kuona hakuna tija ya kuendelea na ukadiriaji
au kupokea taarifa za waagizaji peke yao.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili Kurasini leo saaa 4:
30 asubuhi (Alhamisi, Februari 11, 2016) kwenye kitengo hicho kilichopo
Kurasini (Kurasini Oil Jetty), alikagua mita hizo na kisha kwenda kukagua meli
iliyokuwa ikishusha mafuta bila kutumia mita hiyo ya kupima mafuta
yanayopokelewa kwa sababu mafundi walikuwa bado wanaendelea na ukarabati.
Akiwa Kurasini, Waziri Mkuu alielezwa na Bibi Chuwa kwamba mita
hizo zilianza kufanyiwa ukarabati jana na leo asubuhi moja imekamilika ambayo
ni ya kupokelea mafuta ya petroli. Ya dizeli ilikuwa inafunguliwa na mafundi na
kukutwa imejaa kutu sababu ya kutotumika kwa muda mrefu.
“Hii ya dizeli imefunguliwa leo na ile ya mafuta
ya kula, haijawahi kufanya kazi tangu ilipofungwa mwaka 2011,” alielezwa Waziri
Mkuu na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari, Eng. Aloyce Matei.
Alipoulizwa ni kwa nini aliamua kuzifungia mita
hizo ziisifanye kazi, Bi. Chuwa alijibu kuwa alifikia uamuzi huo baada ya
kupokea malalamiko kwamba zinawapunja wateja. Hata hivyo, hakufafanua ni wateja
gani au wa aina gani.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa,
ametembelea na kukagua mita mpya za kupimia mafuta ambazo zinajengwa Kigamboni.
Mita hizo zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/-
za sasa).
Akiwa hapo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba ujenzi
huo ambao ulianza miezi nane iliyopita, unatarajiwa kukamilika ifikapo katikati
ya mwezi Machi, 2016. “Tunajitahidi kazi hii ikamilike ifikapo katikati ya
mwezi ujao,” alisema Eng. John Bura, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya BQ
Contractors Ltd ambayo inasimamia ujenzi wa mita hizo.
Vilevile, Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia
mafuta yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo
ya kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko
Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia bainaya Serikali na kampuni ya Oryx Energies.
Katika ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER
imejiunganishia bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta
linalotoka bandarini hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo
litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.
“Natoa mwezi mmoja hili bomba liondolewe kwenye
mfumo huu na kama yapo mabomba mengine pia yaondolewe,” alisema huku akionyesha
karatasi iliyokuwa mfukoni kwake yenye mchoro unaobainisha kuwa kuna bomba
jingine la inchi 10 limeungwa kinyemela kwenye bomba kuu.
“Kila mmoja anapaswa aje kuchukua pale kwenye manfold
ili tujue nani kachukua nini. Msajili wa Hazina hili ni eneo lako na wewe
unamiliki TIPER kwa asilimia 50, hebu simamia hili. Ninyi TPA leteni
mapendekezo yenu Serikalini ili tuone tunaweza kudhibiti vipi vitendo kama
hivi,” alisema Waziri Mkuu.
Pia alimtaka Msajili wa Hazina, Bw. Lawrence
Mafuru awasiliane na Mwanasheria Mkuu ili waangalie upya mkataba na umiliki wa
matenki hayo uwe chini ya Serikali kwa asilimia 100 ili mafuta yanayoagizwa na
Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency) yaweze
kuhifadhiwa huko.
Mapema, Waziri Mkuu ambaye alifuatana na Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alikagua eneo la manfold
ya Mamlaka ya Bandari iliyopo Kigamboni na kukuta ni kampuni nne tu zenye
matenki Kigamboni ambazo zinachukua mafuta yao hapo.
Kampuni hizo ni HASS, WORLD OIL, LAKE OIL na MOIL.
TIPER haikutaka kufuata mfumo huo licha ya kuwa nafasi ya kufanya hivyo ipo.
Kampuni nyingine zenye matenki yake nchi kavu, zinachukulia mafuta kwenye manfold
ya Kurasini.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
ALHAMISI,
FEBRUARI 11, 2016.
Post a Comment