|
WIZARA ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewahakikishia Watanzania wote
kwamba watapatiwa hati halali ya umiliki wa ardhi, nyumba na mashamba
ili kujinufaisha na mikopo katika taasisi za fedha, kujikwamua kiuchumi
na kuingizia serikali mapato.
Aidha,
wawekezaji watakaopatiwa hati na kubainika kutoendeleza mashamba yao kwa
miaka mitatu, watapokonywa na kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya
kuyaendeleza.
Akizungumza
katika uzinduzi wa Programu ya Kuwezesha Umilikishwaji Ardhi (LTSP) Dar
es Salaam jana, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William
Lukuvi alisema lengo la programu hiyo ni kupunguza migogoro ya ardhi
iliyokuwepo nchini.
Programu
hiyo itaanza kwa mkoa wa Morogoro katika wilaya za Ulanga na Kilombero,
ambayo itadumu kwa miaka mitatu na kugharimu Dola za Marekani milioni
15.2, ambazo zimefadhiliwa na Washirika wa Maendeleo zikiwemo nchini za
Denmark, Uingereza na Sweden.
Lukuvi
alisema kwa sasa ni asilimia 10 ya Watanzania wanaomiliki ardhi
kihalali, hivyo inachangia migogoro ya ardhi kwa kuwa ardhi iliyokuwepo
haijulikani nani mmiliki wake, na kutokana na changamoto hiyo, ardhi
inakosa tija katika kuchangia kupunguza umasikini na ongezeko la uvamizi
katika maeneo yaliyohifadhiwa.
Alisema
programu hiyo ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa kila
Mtanzania, itamsaidia kumiliki kihalali ardhi yake kupitia sheria ya
ardhi ikiwemo ya kimila na makazi na kubainisha ni nani anayemiliki
shamba na nyumba.
Balozi wa
Denmark nchini, Einar Jensen alisema programu hiyo itasaidia Watanzania
kuona usalama wa ardhi yao na itatoa fursa nyingi kwa masuala ya kilimo
na uwekezaji; na kuwa Watanzania wataweza kuhakiki taarifa za ardhi na
matumizi yake yanahifadhiwa kwa matumizi ya baadaye.
Post a Comment